2021
Braden Anaongoza Njia
Mei/Juni 2021


Braden Anaongoza Njia

Mwandishi anaishi California, Marekani.

Hadithi hii ilitokea huko Louisiana, Marekani.

Maisha kwenye shamba la mamba yalikuwa mazuri. Lakini kitu kimoja kilikosekana.

“Uwe kielelezo kwao waaminio” (1 Timotheo 4:12).

boy reading scriptures on dock

Braden na Baba walibeba makapu mazito ya chakula cha mamba kuelekea sehemu ya kulishia. Sehemu ya juu ya vichwa vya mamba ilijitokeza juu na kunyiririka kuwaelekea wao. Wakati Braden na Baba walipofika sehemu ya kulishia, baadhi ya mamba midomo yao ilikuwa wazi tayari.

Lakini Braden hakuogopa. Kufanya kazi pamoja na Baba katika shamba la mamba ilikuwa kitu kizuri.

“Wakati wa kulisha!” Braden alisema. Alichota upawa wa mabonge ya chakula na kuyatosa majini.

Chubwi. Chubwi. Pwaa.

Baadhi ya mamba walidaka yale mabonge ya chakula hewani. Wengine waling’wafua wakati yalipogusa maji. Braden na Baba waliendelea kutupa kile chakula majini hadi vikapu vyao vilipokuwa tupu.

“Asante kwa kunisaidia,” Baba alisema. “Twende zetu. Karibu wamisionari watakuja.”

Braden na familia yake walikuwa wameanza mazungumzo na wamisionari miezi michache iliyopita. Aliwapenda wamisionari! Na alipenda kujifunza kuhusu Kanisa. Baba alikuwa muumini wa Kanisa, lakini amekuwa haendi kanisani mara kwa mara. Mama na Braden hawajawahi kubatizwa.

“Wiki iliyopita mlijiwekea lengo la kusoma Mosia 18,” Dada Cox alisema jioni ile. “Je, hilo limeendaje?”

Mama na Baba waliangaliana na walikuwa kimya kwa muda. “Tumekuwa na shughuli nyingi wiki hii,” Mama alisema.

“Mimi nilisoma!” Braden alisema.

“Hongera!” Dada Blood alisema, akigonga mkono wa pongezi. “Ulijisikiaje baada ya kusoma?”

Braden alitoa tabasamu kubwa. “Vizuri sana. Na niliomba kuhusu kubatizwa. Hakika nataka.”

“Hiyo ni vizuri! Ninajua hilo linamfanya Baba wa Mbinguni afurahi zaidi,” alisema Dada Cox. Alimgeukia mama wa Braden. “Je, wewe unajisikiaje kuhusu hilo?”

“Mimi bado sina uhakika. Nafikiri nahitaji muda kidogo,” Mama alisema.

Braden alijisikia huzuni kidogo wakati wote uliosalia wa somo. Alitamani wazazi wake wote wangekuwa waumini wa Kanisa. Na yeye alitaka kuwa muumini wa Kanisa pia!

Wamisionari walipoondoka, aliwaambia wazazi wake kwamba alimaanisha kwa kile alichokisema pale awali. “Hakika nataka kubatizwa. Na …” Braden alivuta pumzi ndefu. “Hakika nataka Baba anibatize.”

Baada ya muda, Baba alizungumza. “Hakika nami nalitaka hilo pia.”

Mama alikuwa kimya. “Basi na tuombe kuhusu hili.”

Braden alipiga magoti pamoja na familia yake na akamwomba Baba wa Mbinguni kama yeye na Mama wanapaswa kubatizwa. Alijisikia vizuri na mwenye kupendwa.

Kwa wiki chache zilizofuata, Braden alisoma maandiko na kuomba kila siku. Mwanzoni, yeye ndiye daima aliyewaomba wazazi wake kama wangeomba na kusoma pamoja naye. Lakini mara, wakaanza kumwomba yeye. Wakati yeye na Baba walipokuwa wakiwalisha mamba, wangeongelea kuhusu maandiko au kile walichojifunza kanisani. Yeye na Mama wangezungumza kuhusu masomo ya wamisionari. Kila siku, Mama na Baba walionekana kidogo wenye furaha zaidi.

Siku moja wakati wa somo pamoja na wamisionari, Mama alisema maneno ambayo Braden amekuwa akiyasubiria: “Nataka kubatizwa.”

Kwa wiki chache zilizofuatia, Braden alijisikia kama mtu aliyekuwa akielea kwenye mawingu.

Hatimaye, ilikuwa ile siku ya ubatizo wa Mama na Braden. Braden alipotoka majini, alihisi upendo wa Baba wa Mbinguni kwa ajili yake na kwa familia yake. Alimpa Baba kumbatio kubwa.

Baba alimshikilia Braden karibu na kunong’ona, “Asante kwa kuwa mfano mwema na kwa kutusaidia sisi. Ninakupenda.”

May 2021 Friend