Kufungiwa Nje!
Mwandishi anaishi Utah, Marekani.
Hadithi hii ilitokea huko Central Hangari, Hungary.
Pengine Emma angeweza kusaidia!
”Weka imani yako katika Roho yule ambaye huongoza kufanya mema” (Mafundisho na Maagano 11:12).
Emma aliruka juu ya nyufa katika njia ya mawe ya pembeni. Ilikuwa ni siku angavu, yenye jua kali. Yeye na Mama walikuwa wakitembea kwenda kwenye duka la vyakula.
“Mama, ni mbali kiasi gani liliko jua?” aliuliza.
“Mimi sina hakika,” Mama alisema.
Emma akaelekeza macho yake juu angani. “Je, unafikiri ndege itaweza kwenda kwenye jua? Je, unafikiri joto lake ni kali kuliko radi? Je, unafikiri …”
Mama alicheka. “Maswali yako yanazidi kuwa magumu zaidi na zaidi!”
Emma naye alicheka pia. Alikuwa na maswali mengi. Mama daima alifanya kadiri alivyoweza kuyajibu. Hiyo ndiyo sababu kwa nini Emma alipenda kwenda matembezi pamoja na Mama.
Emma aliangalia kuzunguka maeneo ya ujirani. Teksi zilindeshwa kushuka njia ile ya mawe. Watu waliendesha baiskeli. Watu wengi walikuwa wakitembea kwa miguu pia.
Kisha Emma aliangalia upande wa pili wa mtaa. Msichana mdogo alikuwa amekaa kwenye ngazi nje ya jengo la makazi. Ilionekana kana kwamba alikuwa akilia.
Emma alipunguza mwendo. Je, anapaswa kusimama asaidie? Pengine msichana alitaka aachwe peke yake. Nyakati zingine Emma alitaka aachwe peke yake wakati alipokuwa na huzuni.
Emma aliacha kutembea. Mara nyingi Emma alitaka mtu wa kuongea naye wakati alipohitaji msaada. Na pengine yeye angeweza kusaidia!
Aliukamata mkono wa Mama. “Tazama, Mama. Nafikiri yule msichana anahitaji msaada.”
Mama aliangalia ule upande wa pili wa mtaa. “Nafikiri uko sahihi.”
Emma aliushikilia mkono wa Mama walipokuwa wakivuka kuelekea ule mtaa. Alitembea kupanda zile ngazi kwenda pale msichana alipokuwa amekaa. “Halo,” Emma alisema. “Unahitaji msaada wowote?”
Msichana yule mdogo alivuta kamasi na kuwaangalia. Mikono yake ikiwa imezungushwa kwenye magoti yake, na macho yake yalikuwa mekundu na yamevimba.
“Mimi … nimefungiwa nje ya nyumba yangu.” Alivuta pumzi kwa nguvu. Sauti yake ilikuwa ikitetema na tulivu. Emma alimwinamia ili apate kumsikia vizuri zaidi.
“Siwezi kusoma,” msichana alisema. “Sijui kitufe cha kubofya ili nirudi ndani tena.”
Emma aliuangalia ule ukuta nje ya lile jengo. Palikuwa na vitufe vingi vidogo vidogo. Kila kitufe kilikuwa na jina juu yake. Pembeni mwa vitufe kulikuwa na kipaza sauti.
“Je, jina lako la mwisho ni nani?” Emma alimwuliza.
“Schneider,” yule msichana mdogo alisema.
Mama akasoma vile vitufe vyote hadi akapata kile kilichosema “Schneider.” Akakibonyeza
Bazz!
Kile kitufe kikatoa sauti kubwa. Kisha sauti ikasikika kupitia kipaza sauti.
“Hapa ni Schneiders. Je, nikusaidie nini?”
Mama akaongea kwenye kile kipaza sauti “Habari! Binti yangu na mimi tuko hapa nje pamoja na msichana mdogo ambaye anasema amefungiwa nje.”
Yule msichana akasimama haraka na kukimbilia kwenye kipaza sauti. “Mama,” alisema, “Sikuweza kusoma kitufe ili kurudi ndani, na watu hawa wamenisaidia!”
Sauti kwenye kipaza sauti ilisikika kushangazwa. “Leni! Mimi nilidhani uko chumbani mwako! Usiogope. Ninashuka huko chini sasa hivi.”
Baada ya sekunde chache, mwanamama alikuja akikimbia. Yule msichana naye akamkimbilia na kumkumbatia.
Yule mwanamama akamgeukia Emma. “Asante sana kwa kumsaidia Leni wangu mdogo.”
Emma alitabasamu. “Ilikuwa rahisi kumsaidia.”
Walipungiana kwa heri na wakashuka chini ya ngazi. Mwili wote wa Emma ulihisi vizuri. Akafikiria swali moja zaidi kwa ajili ya mama.
“Kumsaidia msichana yule ilikuwa rahisi. Kwa nini ninahisi furaha sana kuhusu hilo?”
Mama aliufinya kidogo mkono wa Emma. “Huyo ni Roho Mtakatifu anakuambia kwamba ulifanya uchaguzi sahihi.”
Emma alitabasamu. Alifurahi kuwa alisimama ili kusaidia.