Soka na Sabato
Hadithi hii ilitokea huko Hondurasi
“Jumamosi ni siku maalumu. Ni siku tunayofanya maandalizi kwa ajili ya Jumapili” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 196).
Jumamosi ya Samweli iliingiliana na Jumapili yake.
Samweli alipenda kuangalia runinga pamoja na baba, hasa siku za Jumamosi. Baba alifanya kazi kwa bidii wiki nzima. Lakini Jumamosi, Mamá alipika pastelitos de piña (mikate iliyochanganywa na nanasi) na wote waliangalia runinga pamoja.
Jumamosi moja usiku, waliamua kuangalia partido de fútbol (mchezo wa soka). Lakini mechi ilianza ikiwa imechelewa, na ingechukua muda mrefu. Wakati nusu ya kwanza ilipokwisha, magoli yalikuwa 0-0. Samweli alitaka kuendelea kuangalia. Lakini hakuweza kuacha kupiga miayo.
“Wakati wa kulala, Samuelito,” Mama alisema kwa upole. “Unahitaji kupata usingizi ili uweze kukaa macho Kanisani kesho.”
“Lakini Mama,” Samweli alisema. “Ni mbili kati ya timu bora zaidi katika Honduras!”
Baba aliangalia saa. “Sawa sawa. Unaweza kuendelea kuangalia. Lakini unahitajika kuamka kwa wakati kesho.”
Mchezo ukawa wa kusisimua zaidi katika nusu ya pili. Samweli alikuwa macho zaidi sasa! Yeye na Baba wote wawili walikuwa wakishangilia. Kwanza ulitokea mkwaju wa kona. Halafu golikipa akaokoa vizuri sana. Timu moja ikafunga, na kisha nyingine ikarudisha. Kabla Samweli hajajua, mchezo ukawa umekwisha. Uliisha kwa sare ya 1-1.
Asubuhi iliyofuata, Samweli alikuwa amechoka sana kiasi kwamba hakutaka kuamka kitandani. Lakini alijua kwamba kwenda Kanisani ilikuwa muhimu.
Wakati wa mkutano wa sakramenti, Samweli alianza kusinzia. Kichwa chake kiliendelea kujigonga gonga. Mama alimtingisha ili kumsaidia kukaa macho. Lakini alikuwa amechoka sana kiasi kwamba hakuwasikiliza wazungumzaji. “Nafikiri Jumamosi yako inaingilia Jumapili yako,” Baba alisema.
Katika Msingi, mwalimu wa Samweli alizungumzia kuhusu kuitakasa siku ya Sabato. Aliuliza watoto wanaweza kufanya kitu gani ili kuifanya Jumapili kuwa maalumu. Samweli lifikiri kwa dakika chache. Kisha akasema,“Nenda kalale kwa wakati siku ya Jumamosi!”
Walipofika nyumbani baada ya kutoka kanisani, Samweli alizungumza na Mama na Baba. “Niliburudika kuangalia ule mchezo usiku wa jana,” Samweli alisema. “Lakini nilipaswa kuwa nimekwenda kulala mapema. Nafikiri tunapaswa kutumia sehemu ya Jumamosi ili kujiweka tayari kwa ajili ya Jumapili.”
“Ninakubali,” Baba alisema.
Mama aliitikia kwa kichwa. “Mimi pia.”
Jumamosi iliyofuata, palikuwa na mechi nyingine kwenye runinga.
“Tunapaswa kufanya nini usiku wa leo?” Baba aliuliza. “Mchezo unachezwa usiku sana tena.”
“Tunaweza kuangalia filamu badala yake,” Mamá alisema.
“Au tunaweza kwenda kutembea,” alisema Samweli.
“Matembezi ni sawa kwako?” Baba alimwuliza Mama.
“Ndiyo,” Mama alisema. “Ni vizuri tu kuwa pamoja kama familia.”
“Na tutakapokuwa tumefika nyumbani,” Samweli alisema, “sote tunaweza kupata usingizi mzuri wa usiku. Ndipo tutakuwa tayari kwa ajili ya Jumapili!”