2021
Kazi Kuu
Januari 2021


“Kazi Kuu,” Kwa ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Januari 2021, 20–21.

Kazi Kuu

Dhima ya Vijana kwa Mwaka 2021:
Mafundisho na Maagano 64:33–34

Bwana amekualika kujiunga katika “kazi kuu zaidi ” duniani.1

Nembo ya Dhima ya Vijana kwa Mwaka 2021

Ninyi wasichana na wavulana wa kupendeza ni sehemu ya jambo la kipekee—“mnaujenga msingi wa kazi kuu” (Mafundisho na Maagano 64:33). Kazi hiyo inamsaidia Bwana, Yesu Kristo, kutimiza jukumu Lake pale tunaposhiriki katika kukusanya Israel kwenye pande zote za pazia na kujenga Sayuni.

Kujiunga na Batalioni ya Vijana

Rais Russell M. Nelson amemualika kila mmoja wenu kujiunga katika kazi hiyo kama sehemu ya “batalioni ya vijana wa Bwana.”2 Je, ni nini maana ya batalioni? Batalioni ni kikundi maalum kilichoundwa ili kutekeleza majukumu mahsusi kwa pamoja. Hiyo inamaanisha kuwa wewe ni sehemu ya kikundi maalum kwa ajili ya kutambua na kutimiza jukumu lako katika kazi kuu ya Bwana.

Wakati nabii alipowaalika kutazama kusudi la maisha yenu mkiwa na fokasi katika kukusanya Israeli, maisha yako yalianza kuwa kama maisha ya Musa. Musa, aliyekuzwa kama mwana mfalme wa Misri, alilazimika kutoroka ili kuokoa maisha yake na baadaye aliridhika na maisha yake ya kawaida ya kuchunga kondoo. Lakini Bwana alimuita na kutangaza, “Ninayo kazi kwa ajili yako” (Musa 1:6). Baba yetu wa Mbinguni alijua kile ambacho Musa hakuwa anakijua: kwamba kwa msaada wa Mungu, Musa angeweza kuwa chombo katika kuliokoa taifa kuu—angeweza kufanya chochote.

Unaweza Kuleta Utofauti

Huenda ukajiuliza, “Mimi si Musa. Je, ninaweza kuleta utofauti wowote katika ulimwengu huu?” Hata sisi wakati mwingine tumehisi hivyo, lakini tumeishi muda mrefu kiasi cha kufahamu kuwa jibu ni ndiyo. Kila siku tunawaona vijana wa kawaida wakifanya uamuzi wa kutoishi maisha ya kawaida. Vijana hawa wana ushawishi mkubwa kwa wenzao kwa kuishi tu maisha yanayoonyesha kuwa wao ni wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Wanakuza vipawa vyao na wanasaidia familia zao kufanikiwa. Nabii anakuita uje “ujenge msingi wa kazi kuu.” Tunapomwamini Yesu Kristo na kutafuta kutenda mapenzi Yake, tunaleta utofauti!

Hauko peke yako kwenye hili. Unapojiunga na batalioni ya Bwana, unajiunga na kikundi kikubwa cha vijana kote ulimwenguni. Tunasimama nawe bega kwa bega pamoja na wazazi, viongozi, na rafiki zako, mitume na manabii, na malaika wa mbinguni, sote tukijitahidi kukamilisha kazi ya Bwana pamoja (soma Mafundisho na Maagano 84:88).

Na Kutokana na Mambo Madogo Huja Yale Yaliyo Makuu

Tutaenda hatua kwa hatua. Bwana anatualika tupige hatua rahisi za kawaida tunapojiingiza katika kazi hii kuu (ona Mafundisho na Maagano 64:33). Kutenda vitendo vya uaminifu kila wakati kutatuwezesha kusonga mbele na kutualika kuwafikia na kuwasaidia walio karibu nasi. Unaweza kufanya baadhi ya mambo haya ya kawaida kwa namna yako kwani kila mtu ana safari yake tofauti.

Omba ili ufahamu wewe ni nani na uelewe jukumu lako binafsi katika mpango wa Mungu. Omba ili ufahamu mambo rahisi na ya kawaida unayopaswa kufanya kila siku. Yawezekana itabidi kuyaacha maisha uliyozoea, lakini kadiri unavyokuwa radhi kutendea kazi ushawishi unaopokea, utaongezewa.

Kama Rais Nelson alivyofundisha hivi karibuni: “Tunapotafuta kuwa wafuasi wa Yesu Kristo, jitihada zetu za kumsikiliza Yeye zinatakiwa ziwe za dhati zaidi. Juhudi za hiari na za dhati zinahitajika kila wakati ili kujaza maisha yetu ya kila siku kwa maneno Yake, mafundisho Yake na kweli Zake.”3

Bwana Atakuza Uwezo Wako na Atakuongezea Furaha

Unapotafuta ufunuo, Bwana atakuongoza kufahamu jinsi ya kutumia vipawa vyako na nafsi yako ili kumtumikia na kuishi injili. Atapanua mawazo yako, ubunifu na uwezo wako katika njia ambazo hungewahi kufikiria zinawezekana.

Unapotoa moyo wa dhati na mawazo yako kwa Bwana, utagundua marafiki zaidi na fursa nyingi za kuhudumu. Mtazamo wako wa kusudi na utambulisho utaimarishwa, na utapata furaha.

Wakati mwingine tunaweza kujihisi kutulia na kuridhika, lakini Mungu ana mpango mwingine. Kama alivyokuwa amemwandalia Musa kazi kuu, Ana kazi kuu kwa ajili yako. Usichoke! Tuna ujasiri mkamilifu kwenu—batalioni ya vijana ya Bwana.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli” ( ibada ya vijana kote ulimwenguni, Juni 3, 2018), 3, HopeofIsrael.ChurchofJesusChrist.org.

  2. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli,” 12, HopeofIsrael.ChurchofJesusChrist.org.

  3. Russell M. Nelson, “Msikilize Yeye,” Mkutano mkuu wa Aprili 2020 (Ensign au Liahona, Mei 2020, 89).