2021
Joseph Smith—Nabii Wangu
Januari 2021


“Joseph Smith—Nabii Wangu,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Januari 2021, 8–11.

Njoo, Unifuate

Joseph Smith—Nabii Wangu

Yeye ni nabii wako pia. Unaweza kusoma mafundisho yake mwaka huu ili umfahamu zaidi kama nabii wako.

Picha
Joseph Smith

Kuna jambo ambalo Rais Russell M. Nelson alisema kwenye mkutano mkuu wa Aprili 2020 lililokaa akilini mwangu: “Haijalishi unakoishi au hali inayokukabili, Bwana Yesu Kristo ndiye Mwokozi wako, naye nabii wa Mungu, Joseph Smith, ndiye nabii wako” (“Msikilize Yeye” [Ensign au Liahona, Mei 2020, 88]).

Tangu nilipokuwa mdogo, nimehisi hivyo—Joseph Smith ni nabii wangu. Zaidi ya mtu mwingine yeyote, nabii huyu wa Urejesho amenisaidia kumjua Yesu Kristo na injili Yake. Nimesoma kuhusu ufunuo unaopatikana kwenye Mafundisho na Maagano. Na nilipokuwa kijana, baba yangu alinipa kitabu cha mafundisho ya Joseph Smith na nikakisoma chote. Kusoma mafundisho hayo kumenisaidia kuwa shahidi wa injili ya urejesho.

Tangu wakati huo nimekuwa nikiwaza: ni kipi kwenye mafundisho ya Joseph Smith kilichonishawishi namna hii? Kipi kilichopelekea Roho wa Mungu kunifunulia ukweli kwa nguvu? Ninaweza kusema ni mambo matatu: (1) alisadiki alichofahamu, na alikisema kwa ujasiri; (2) alifafanua vyema ukweli ambao alikuwa amepokea kupitia ufunuo; na (3) sifa na tabia yake daima vilidhihirika wazi.

Alisadiki Alichofahamu, na Alikisema Kwa Ujasiri

Tangu alipoona Ono la Kwanza, Joseph Smith aliteswa kwa kueneza habari za mambo aliyokuwa amejifunza kuptia ufunuo. Lakini alifahamu kuwa hangekata tamaa: “Kwa nini wanitese kwa ajili ya kusema ukweli? Hakika nimeona ono; na je, mimi ni nani hata niweze kupingana na Mungu, au kwa nini ulimwengu wafikiria kunifanya mimi nikane kile ambacho hakika nimekiona? Kwani nimeona ono; nami najua hivyo, nami nilijua kwamba Mungu alijua, na sikuweza kukataa, wala kuthubutu kufanya hivyo” (Joseph Smith—Historia 1:25).

Japo alijua kuwa angepitia mateso na kuchukiwa zaidi kwa kufanya hivyo, Joseph Smith alitangaza kwa ujasiri ukweli ambao alikuwa amejifunza kutoka kwa Mungu kwa kipindi cha maisha yake yote yaliyosalia.

Mfano:

Japo watu wengi katika ulimwengu wa Kikristo waliamini kuwa mwanadamu aliumbwa na Mungu pasipo kutumia kitu chochote, Joseph Smith alifundisha kitu tofauti kwa ujasiri:

“Mwanadamu pia alikuwepo mwanzoni pamoja na Mungu. Akili, au nuru ya ukweli, haikuumbwa wala kutengenezwa, kamwe haiwezekani kuwa” (Mafundisho na Maagano 93:29).

“Nafsi—mawazo ya mwanadamu—roho isiyokufa. Ilitoka wapi? Wasomi na wanatheolojia wote wanasema kuwa Mungu aliiumba mwanzoni; lakini sivyo: wazo lenyewe linashusha hadhi ya mwanadamu katika makadirio yangu. Siamini mafundisho haya; ninajua zaidi. Sikiliza, e mataifa yote ya ulimwengu; kwa maana Mungu amenifunulia hivyo; na msiponiamini, hiyo haitabatilisha ukweli” (Mafundisho ya Marais wa Kanisa: Joseph Smith [2007], 209).

Picha
Joseph Smith akifundisha

Alifafanua Ukweli kwa Uwazi

Wakati mwingine Joseph Smith alidokeza kuwa alikuwa anajua mambo mengi mno ya maajabu ya Mungu kiasi cha kutoweza kuyashiriki yote na ulimwengu. Lakini alipofundisha, alijua jinsi ya kufanya kweli za Mungu ziwe rahisi na wazi.

Mfano:

Tangu alipoona Ono la Kwanza na kuendelea, Joseph Smith alijifunza ukweli mwingi kuhusu asili ya Mungu Baba wa Milele. Na katika mafundisho yake alifafanua umuhimu wa ukweli huu. Kwa mfano, alisema:

“Watu hawawezi kujitambua ikiwa hawajamtambua sifa ya Mungu” (Mafundisho: Joseph Smith, 40). Hii ni kauli ya wazi inayoonyesha kiini cha ukweli kumhusu Mungu, kutuhusu sisi, uhusiano wetu Naye na uwezo wetu.

Alifuatiliza kauli hiyo kwa maneno haya: “Mungu Mwenyewe aliwahi kuwa jinsi tulivyo, na ni mwanadamu aliyetukuka” (Mafundisho: Joseph Smith, 40). Kwa ufafanuzi zaidi.

Kisha akafundisha hili: “Mungu mwenyewe, alipojikuta katikati ya utukufu na viumbe vya kiroho, kwa sababu alikuwa mwenye akili zaidi, aliona inafaa kuweka sheria zitakazowawezesha wengine kuendelea na kuwa kama yeye” (Mafundisho: Joseph Smith, 210). Joseph Smith ametaja jambo fulani hapa ambalo ni la muhimu katika mpango wa Baba wa Mbinguni: Baba wa Mbinguni angependa tuwe kama Yeye.

Picha
Joseph Smith akizungumza

Sifa na Tabia Yake Zinajitokeza Wazi

Jinsi Joseph Smith alivyofafanua mambo inatupa taswira kuhusu hulka yake na alivyokua kama mtu na pia kama nabii. Hii ni muhimu, kwa sababu muunganiko na watu kwa kiasi fulani hurahisisha muunganiko kwenye mawazo. Sifa ya Joseph inajitokeza wazi katika mafundisho yake.

Mfano:

Japo Joseph Smith kiasili alikuwa mchangamfu (ona Joseph Smith—Historia ya 1:28), lilipokuja suala la alichoagizwa na Bwana, alikichukulia kwa uzito. Kutokana na uzoefu alifahamu matokeo yanayoweza kutokea kwa kutotii amri kama hizo (ona, kwa mfano, Mafundisho na Maagano 3:4–9). Uchangamano huu wa uchangamfu na ufuasi wa kuchukulia mambo kwa uzito unanivutia—na binafsi, ninaweza kutambulishwa nao.

Picha
Joseph Smith akicheza

Naam, kama nabii wa Urejesho, Joseph Smith aliamrishwa kufundisha kweli za Mungu alizofunuliwa, nyingi za hizo zilikuwa ngeni kwa kila mtu. Joseph alilazimika kuwasaidia watu kufahamu kweli hizi mpya. Lakini wakati mwingine ilikuwa inafadhaisha. Alisema siku moja:

“Imekuwa vigumu mno kwa watu wa kizazi hiki kuelewa mambo. Imekuwa kama kupasua gogo kwa kutumia keki ya mahindi [kipande cha mkate ulioandaliwa kwa unga wa mahindi] ili kupata kipande cha mbao, na boga kwa nyundo kubwa [ya mbao]. Hata Watakatifu si wepesi wa kuelewa” (Mafundisho: Joseph Smith, 540).

Hili lilikuwa muhimu kwa Joseph Smith. Kulikuwa na mengi ambayo alitaka watu wajue, waelewe, wakubali na wazingatie na waishi—lakini walikataa. Lakini analojia rahisi iliyotolewa na Mmarekani katika karne ya kumi na tisa inatuonyesha taswira kidogo ya kufurahisha kuhusu sifa ya Joseph Smith.

Kuna mambo mengi mengine kuhusu sifa ya Joseph Smith yanayojitokeza katika mafundisho yake. Kwa mfano, alipenda marafiki: “Moyo wangu utawapenda, na mikono yangu itawashughulikia, wanaonipenda na wanaonishughulikia, na daima nitakuwa mwaminifu kwa rafiki zangu” (Mafundisho: Joseph Smith, 462).

Au ukarimu na wema wake: Wakati fulani ambapo watu walisema wanamhurumia mtu ambaye nyumba yake ilikuwa imechomwa, Joseph alisema papo hapo, “Huruma yangu kwa kaka huyu ni ya dola tano; je, nyote mnamhurumia kiasi gani?” (Mafundisho: Joseph Smith, 460).

Kisha kuna upendo wake kwa familia yake, uadilifu, unyenyekevu, ujasiri, haki na usawa, imani wakati wa majaribu na mateso. Yote yako hapo, yanajitokeza pamoja na kweli na sheria za milele za kuzingatia maishani.

Yeye Ni Nabii Wangu

Joseph Smith bado anapingwa na kukashifiwa hadi leo, bila shaka. Lakini kama alivyosema, “Kamwe sikuwaambia kuwa mimi ni mkamilifu; lakini hakuna kosa katika maono ambayo nimewafundisha” (Mafundisho: Joseph Smith, 522). Tunaweza kushuhudia kwa ujasiri kuwa alikuwa nabii. Ni rahisi kwangu kushuhudia kumhusu Joseph Smith—sio kwa sababu nina jibu kwa maswali yote yanayoulizwa na watu kumhusu, lakini kwa sababu nimesoma kuhusu ufunuo na mafundisho yake ya kinabii na nikahisi Roho Mtakatifu akishuhudia kuwa ni ya kweli. Kama vile Joseph mwenyewe alivyosema wakati mmoja:

“Ninaweza kuonja sheria za uzima wa milele, hivyo nanyi pia mnaweza. Nimepewa sheria hizi kupita ufunuo wa Yesu Kristo; na ninajua kuwa nitakapowaeleza maneno haya ya uzima wa milele kama nilivyopewa, kisha myaonje, ninajua kuwa mtaamini. Mnasema kuwa asali ni tamu, nami ninakubali. Ninaweza pia kuonja roho wa uzima wa milele. Ninajua kuwa ni nzuri; na ninapowaeleza kuhusu mambo haya niliyopokea kupitia ufunuo wa Roho Mtakatifu, utayapokea kama kitu kitamu, na utafurahi zaidi na zaidi” (Mafundisho: Joseph Smith, 525).

Nimeonja utamu huo. Ilishirikishwa kwangu na nabii wangu, Joseph Smith. Na kama Rais Nelson alivyosema, ni nabii wako pia. Unaweza kufahamu kwa kina kuhusu maisha na mafundisho yake mwaka huu kwa kusoma Njoo, Unifuate. Kisha utakuwa shahidi wa utamu wa kweli alizokufanya uzionje.

Chapisha