“Ufadhili wa Uyoga,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Jan. 2021, 6–7.
Ufadhili wa Uyoga
Je, ninaweza kujifunza yapi kutokana na kitu kisichovutia kama vile uyoga?
Sipendi uyoga. Harufu na ngozi yake—siupendi kabisa! Lakini wazazi wangu walianza kukuza uyoga nikiwa mtoto, hivyo tuliula katika mlo kila siku. Wakati wa kuvuna, nilikuwa nikiwasaidia wazazi wangu hadi usiku. Ningepima gramu 200 za uyoga, kisha nizipakie halafu nifunge kifurushi. Nakumbuka nikifurahia wakati nikizungumza na familia yangu. ilikuwa ni kama kuwa na jioni ya familia nyumbani kila siku.
Pia iliiletea familia kipato, hivyo lazima tungesaidia kufanya shughuli hiyo. Lakini kulikuwa na changamoto mbili: Kwanza, kipindi cha televisheni nilichopenda kilikuwa kikirushwa wakati nilipohitajika kufanya kazi, hivyo nisingeweza kukitazama. Na pili, baada ya kumaliza kazi, mikono yangu ilikuwa imegeuka myeusi kwa sababu ya kugusa uyoga, na ilikuwa vigumu kusafisha rangi na kuondoa harufu kwa kutumia sabuni. Nilipokuwa mtoto, ningelalamika wakati mwingine kuhusu kuhitajika kufanya kazi nyingi kila siku.
Uyoga ulitupa kipato kizuri kwa muda fulani, lakini hatimaye bei yake ilishuka baada ya wakulima wanaolima uyoga kuongezeka, na wazazi wangu wakaacha ukulima wa uyoga. Nilifikiri kuwa waliacha tu kwa sababu bei yake ilikuwa imeshuka, lakini niligundua kitu kilichonishangaza wakati nilipohitimu chuo.
Wazazi wangu walianza kukuza uyoga ili kuweka akiba ya karo ya chuo kwa ajili yangu na ndugu zangu. Waliacha kwa sababu walikuwa wamefikisha kiasi cha pesa walichokuwa wakihitaji. Nilipogundua, niliaibika kwa kulalamika siku zote. Sikujua kwamba nilikuwa nikifanya kazi ili kugharamikia malipo yangu ya baadaye ya chuoni. Na zaidi ya hayo, familia yangu ilikuwa imenisaidia!
Nilikuwa nimelalamika mara kwa mara bila kujua kuwa ukulima wetu wa uyoga ulikuwa kwa ajili ya kulipia masomo yangu. Kulalamika kwangu kulikuwa sawa na Lamani na Lemueli katika 1 Nephi 2:12: “Na hivyo Laman na Lemuel … walinung’unika kwa sababu hawakufahamu matendo ya Mungu aliyewaumba.” Nina furaha sana kuwa Bwana ananifahamu vyema na amenibariki, licha ya kulalamika kwangu.
Sidhani kama nitapenda kula uyoga. Lakini ikiwa hakungekuwepo na uyoga, ningehuzunika kidogo, kwa sababu nisingekuwa na kumbukumbu ya mambo tuliyofanya na familia yangu. Kwa sababu yao, nimejifunza kuthamini baraka zangu na kuamini mpango wa Bwana—na kutolalamika! Kwa hiyo hata ingawa sipendi uyoga, sasa ninauthamini. Ni ishara muhimu kwangu kukumbuka mahusiano ya familia yangu.
Mwandishi anaishi Mji wa Shinagawa, Japani.