2021
Kusudi Kuu la Urejesho
Januari 2021


“Kusudi Kuu la Urejesho,” Kwa ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Januari 2021, 3–5.

Kusudi Kuu la Urejesho

Kazi iliyoanzishwa na Joseph na Hyrum Smith, pamoja na watu wengine waaminifu, inaendelea katika Kanisa hii leo.

Joseph na Hyrum Smith

Joseph Smith akiwa kijana alipokwenda kuomba msituni, aliona ono la kustaajabisha, linalojulikana leo kama Ono la Kwanza.

Katika ono hili, Mwokozi alimwambia Joseph kuwa dhambi zake zimesamehewa. Pia alijibu maswali ya Joseph na akasema kuwa hakuna kanisa la wakati huo lililokuwa “limetambuliwa na Mungu kuwa kanisa lake na ufalme wake.”

“Wakati huo huo,” Joseph akakumbuka, “[mimi] [nilipokea] ahadi kuwa utimilifu wa injili katika wakati fulani ujao utajulishwa kwangu.”1

Ono la Kwanza

Kufuatia ono hili lenye utukufu, Joseph aliibuka kutoka kwenye Kijisitu Kitakatifu kuanza matayarisho yake kuwa nabii wa Mungu.

Moroni na Kitabu cha Mormoni

Miaka mitatu baadaye, mnamo 1823, mbingu zilifunguka tena kama sehemu ya Urejesho unaoendelea wa injili ya Yesu Kristo katika siku za mwisho. Malaika aliyeitwa Moroni alimtokea na kusema “kwamba Mungu alikuwa na kazi ya kufanywa [naye] … [na kwamba] kulikuwepo na kitabu kilichohifadhiwa, kilichoandikwa kwenye mabamba ya dhahabu” ambacho kilikuwa na “utimilifu wa Injili isiyo na mwisho” (Joseph Smith—Historia ya 1:33–34).

Joseph Smith akipokea mabamba ya dhahabu

Hatimaye, Joseph alipokea, akatafsiri kisha akachapisha kumbukumbu ya kale, inayojulikana leo kama Kitabu cha Mormoni.

Ndugu Waaminifu

Joseph aliungwa mkono kila wakati na Hyrum kaka yake. Katika maisha yao, Joseph na Hyrum walikabiliwa na magenge na kupitia mateso pamoja. Kwa mfano, walidhoofika katika hali mbaya zaidi ndani ya Gereza la Liberty huko Missouri kwa miezi mitano wakati wa baridi ya mwaka 1838–39.

Wakipitia mateso, Hyrum alionesha imani katika ahadi za Bwana, ikiwa ni pamoja na hakikisho la kuwaponyoka maadui zake ikiwa angechagua hilo. Mnamo Juni 1844, Hyrum alipewa chaguo la kuishi au kuyatoa maisha yake ili kumtukuza Mungu na “kutia muhuri ushuhuda wake kwa damu yake”—bega kwa bega pamoja na kaka yake mpendwa Joseph (ona Mafundisho na Maagano 136:39).

Wiki moja kabla ya wao kuuliwa kinyama, Joseph alimwambia Hyrum aondoke pamoja na familia yake. Bado napatwa na hisia kuu nikikumbuka jibu la Hyrum: “Joseph, siwezi kukuacha.’’2

Hivyo Joseph na Hyrum walikwenda Carthage, ambapo waliuwawa kwa kusudi la injili na jina la Kristo. “Katika maisha hawakugawanyika, na katika mauti hawakutenganishwa!” (Mafundisho na Maagano 135:3; msisitizo umeongezwa).

Hyrum na Joseph Smith

Mwito wa Kutenda

Tunapaswa daima kukumbuka gharama ambayo Joseph na Hyrum Smith walilipa, pamoja na wanaume, wanawake na watoto wengine wengi waaminifu, katika kuanzisha Kanisa ili mimi na wewe tuweze kufurahia baraka nyingi na kweli hizi ziliofunuliwa kwetu leo. Uaminifu wao haupaswi kamwe kusahaulika!

Kabla ya kifo chake mnamo 1844, Joseph aliandika barua iliyojaa ujasiri kwa Watakatifu. Ulikuwa ni mwito wa kutenda, ambao unaendelea katika Kanisa leo:

“Akina Kaka [na akina dada], je, si lazima sisi tuendelee katika kazi hii iliyo kuu? Twende mbele na siyo nyuma. Ujasiri, akina kaka [na akina dada]; na mbele, mbele kwenye ushindi! …

“… Kwa hiyo, sisi, kama kanisa na watu, na kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, tumtolee Bwana dhabihu katika haki” (Mafundisho na Maagano 128:22, 24; msisitizo umeongezwa).

Fikiria ni dhabihu ipi utakayomtolea Bwana kwa haki katika ziku zijazo. Kuwa na ujasiri—ishiriki na mtu unayemwamini na muhimu zaidi, tafadhali tenga muda kuitimiza!

Ninajua kwamba Mwokozi anapendezwa tunapomtolea Yeye dhabihu kutoka mioyoni mwetu kwa haki, kama vile Yeye alivyopendezwa na dhabihu ya uaminifu ya hao ndugu wa kipekee, Joseph na Hyrum Smith, na Watakatifu wengine wote waaminifu.

Muhtasari

  1. Joseph Smith, “Historia ya Kanisa,” Nyakati na Majira, Machi. 1, 1842, 707; ona pia josephsmithpapers.org.

  2. Joseph Smith, “Historia ya Joseph Smith,” Nyota ya Milenia ya Watakatifu wa Siku za Mwisho, Aprili. 19, 1862, 248; msisitizo umeongezwa.