“Mafundisho na Maagano: Muhtasari,” Kwa ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Januari 2021, 14–15.
Njoo, Unifuate
Mafundisho na Maagano: Muhtasari
Ni nini?
Mafundisho na Maagano ni mkusanyiko wa ufunuo wa siku hizi kutoka kwa Mungu kupitia hasa kwa Nabii Joseph Smith. Wingi wa ufunuo huu ulitolewa kama majibu ya maswali ambayo Joseph na waumini wengine wa awali wa Kanisa walimuuliza Mungu.
Je, kwa nini kitabu cha Mafundisho ya Maagano kiliandikwa?
Katika siku za mwanzo za Kanisa, kulikuwepo na nakala chache tu zilizoandikwa kwa mkono kuhusu ufunuo huu. Mnamo 1831, viongozi wa Kanisa waliamua kuchapisha ufunuo kwenye Kitabu ya Amri. Katika mkutano uliofanyika mnamo Novemba 1831 ili kujadili Kitabu cha Amri, Joseph alipokea ufunuo ambao sasa ni sehemu ya 1, utangulizi wa Mafundisho na Maagano.
Mafundisho
Mkusanyiko wa kwanza wa ufunuo ulijulikana kama Kitabu cha Amri. Mikusanyiko ya baadaye ilijulikana kama Mafundisho na Maagano kwa sababu ilijumuisha msururu wa mafunzo “kuhusu mafundisho ya kanisa,” yaliyojulikana kwa kifupi kama “mafundisho” (sasa yanajulikana kama Mafundisho ya Imani). Kuanzia toleo la 1921, Mafundisho ya Imani hayakujumuishwa tena, lakini jina Mafundisho na Maagano lilisalia.1
Maagano
Sehemu iliyosalia ya kitabu ilijumuisha ufunuo ambao Joseph Smith alipokea. Sehemu hii ilijulikana kama “maagano na amri za Bwana” au “maagano” kwa kifupi. Watakatifu wa mwanzo walitumia neno “maagano” au “amri” kurejelea ufunuo huu aliopokea Nabii ili kutofautisha na maandishi mengine ya Joseph Smith, kama vile mahubiri yenye uvuvio na tafsiri zake za Biblia.2
Je, kwa nini kitabu cha Mafundisho na Maagano ni muhimu leo?
Kitabu cha Mafundisho na Maagano kina ufunuo wa Yesu Kristo kwa watu Wake. Kinatufunza kuwa Mungu anatufahamu kwa majina, Anasikia maombi yetu na anajibu maswali yetu, na kuwa Mungu bado anazungumza hadi hii leo. Pia kinafundisha mafundisho muhimu kuhusu mpango wa wokovu na kinatupatia utambuzi wa ziada kwenye Upatanisho wa Yesu Kristo. Kinafariji kwa kutuonyesha jinsi Mungu anavyotupenda na bado anatuita twende Kwake hata tunapokosea.