“Kutetea Imani Yangu,” Kwa ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Januari 2021, 27.
Misingi Imara
Kutetea Imani Yangu
Usiku mmoja nilikuwa pamoja na kundi la marafiki. Tulikuwa tukizungumza kisha wakaanza kupiga umbeya kuhusu marafiki zangu wengine ambao hawakuwepo. Sikufurahishwa na mambo waliyokuwa wakiyazungumza. Kisha nilipata ushawishi kutoka kwa Roho kuwa ninapaswa kutetea msimamo wangu wa imani.
Bila kusubiri zaidi, niliwaeleza kuwa sikufurahishwa na mambo waliyokuwa wakizungumza na nikawasihi wasifanye umbeya nikiwepo. Walisema hiyo ni sehemu ya maisha na hakukuwa na shida. Bila kuudhika na jambo hilo, nilisikiliza mtazamo wao halafu nikafafanua msimamo wangu wa imani. Kisha nikasimama na kuondoka.
Tukio la usiku huo lilinifanya nifikirie kuhusu mambo aliyopitia Joseph Smith. Wakati Joseph Smith alipopata mabamba ya dhahabu, alipitia mateso mengi. Bila kujali mateso aliyopitia, Joseph Smith bado alishikilia msimamo wake na hakutikisika. Mungu alikuwa pamoja na Joseph Smith na alimsaidia, nami pia nilijua kuwa Mungu alikuwa na mimi nilipotetea yaliyo mema.
Nilipoteza marafiki kadhaa usiku ule kwa kutetea imani yangu, na nilihuzunika. Lakini nilihisi amani na utulivu kwa kufanya yaliyo mema. Baadaye kidogo, rafiki yangu mmoja alinishukuru kwa kile nilichokifanya. Kwa sababu hiyo, nilipata tena urafiki na tukawa karibu zaidi kuliko awali.
Andrew F., Utah, Marekani