“Pata Nguvu Zako Katika Yesu Kristo,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Machi 2024.
Tafuta Nguvu Zake
Pata Nguvu Zako katika Yesu Kristo
Yesu Kristo ndiye nguvu kwa vijana—kila kijana duniani—na hilo linakujumuisha wewe pia!
Ninayo furaha kutambulisha toleo hili maalumu la gazeti la Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, . Makala, shughuli na hadithi kutoka kwa vijana duniani kote zitasaidia kuimarisha ushuhuda wako juu ya ukweli muhimu na wa milele ulioonyeshwa na Urais wa Kwanza. Kuhusu Yesu Kristo wanatangaza kwa msisitizo, “Yeye ndiye ‘nguvu ya kijana.’”1 Hii ina maana Yesu Kristo ni nguvu yako. Ninaomba kwamba utakubali ukweli huu kwa furaha katika wakati huu muhimu katika maisha yako, sasa na hata milele.
Kila Mmoja Anahitaji Nguvu katika Kristo
Haupo hapa kwa bahati nasibu au makosa. Ulichagua kuja duniani kujifunza, kukua, kufanya mambo muhimu na kuwa zaidi kama Baba yako wa Mbinguni. Katika safari hii, utakumbana na nyakati za shida, majaribu binafsi, kuvunjika moyo na kukatishwa tamaa ambako unaweza kuhisi kulemewa. Labda unahisi umenaswa katika wakati kama huo hivi sasa.
Katika nyakati kama hizo, tafadhali kumbuka kwamba Baba yako wa Mbinguni anakupenda. Yeye mara zote amekupenda, na ataendelea kukupenda. Kwa sababu ya upendo Wake usio na mwisho na mkamilifu, alimtuma Mwanawe, Yesu Kristo, ili kukuimarisha na kukusaidia kusonga mbele. Na Yesu alikuja kwa sababu anakupenda sana pia.
Cha kusikitisha ni kwamba baadhi ya watu hawatambui hitaji lao la Mwokozi. Hawaelewi kwamba wao, kama watu wote, watafanya makosa wasiyoweza kurekebisha, watapata hasara wasiyoweza kurejesha, na wanakabiliwa na matatizo na misiba ambayo hawawezi kuvumilia wao wenyewe. Wala hawawezi kushinda dhambi na kifo peke yao. Hii ina maana kwamba wao—na watu wote—wanahitaji Upatanisho wa Yesu Kristo, kwa nguvu unayoweza kuleta.
“Hiyo ni nzuri, Mzee Holland,” unaweza kuwa unafikiri, “lakini ninawezaje kumfanya Yesu Kristo kuwa nguvu yangu?” Ili kusaidia kujibu swali hili, tafadhali niruhusu nishiriki njia chache tu kati ya nyingi ambazo Yesu Kristo hukutia nguvu kila siku.
Ana Uwezo wa Kukuimairisha Wewe
Katika usiku Wake wa mwisho katika maisha ya duniani, Yesu Kristo aliingia katika Bustani ya Gethsemane. Hapo, alipiga magoti miongoni mwa mizeituni na kuanza kujitwika dhambi za ulimwengu. Mateso haya makuu na yasiyopimika “yalisababisha [yeye], …aliye mkuu kuliko wote, kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutokwa damu kwenye kila kinyweleo” (Mafundisho na Maagano 19:18).
Kisha Yesu alichukuliwa hadi Kalvari na kusulubiwa. Hapo alikamilisha dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Yeye kwa hiari alitoa uhai Wake, na kisha akafufuka kwa ushindi kutoka kwa wafu. Msimu huu wa Pasaka, ninafurahi kutangaza kwamba Yesu Kristo yu hai! Pia ninatangaza kwamba Yeye sio tu kwamba anaondoa mzigo wa dhambi bali pia “[ali]teseka maumivu na mateso na majaribu ya kila namna” kwa kufanya hivyo (Alma 7:11; msisitizo umeongezwa).
Mwokozi alihisi kila maumivu ya moyo na huzuni na alivumilia, kwa njia ya binafsi, uchungu na mateso yote uliyopitia wewe, mimi na kila nafsi ambayo imewahi kuishi au itakayowahi kuishi. Kwa sababu ya yale aliyopitia kimwili, kiakili na kiroho kwa ajili yako, anajua jinsi ya kukutia nguvu.
Labda ni vigumu kwako kuamini kwamba Yesu angependa kukusaidia ukiwa mmoja tu kati ya mamilioni ya watu walio umri sawa. Kama umewahi kufikiria kama ana mambo bora zaidi ya kufanya kuliko kukutia nguvu katika nyakati zako za uhitaji, mfikirie katika bustani ile, mfikirie juu ya msalaba ule. “Aliteseka, alitokwa na damu na kufa”2 kwa ajili yako kwa sababu Alijua kwamba unastahili. Bado anajua hivyo. Yeye anapendezwa sana, yuko tayari, na anaweza kukusaidia wewe—sasa hivi na hata milele. Alitoa maisha Yake ili aweze kukuimarisha unapokubali mwaliko Wake wa kubadilisha maisha: Njooni kwangu”:(Mathayo 11:28).
Chagua Kutembea pamoja Naye
Ni chaguo lako kumfuata Yesu Kristo na kumfanya kuwa nguvu yako. “Ameweka alama kwenye njia na kuongoza njia”3 kurudi kwa Baba wa Mbinguni. Kwa hakika, Yeye ndiye “njia, kweli, na uzima” (Yohana 14:6).
Unapata njia kwa kukumbatia injili ya Yesu Kristo unapotumia imani Kwake na kutubu dhambi zako. Unakuza uhusiano wako Naye unapochagua kubatizwa katika jina Lake na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kisha unaendelea kwenye njia Yake ya injili kwa kushika amri, kupokea maagizo, kuheshimu maagano na kuishi kama mfuasi Wake.
Vitendo hivi hutengeneza muunganisho wenye nguvu—uunganisho wa agano—unaokufunga kwa usalama kwa Kristo—na Yeye kwako. Unapotembea pamoja Naye, Yeye na Baba wanakuwa vyanzo vyako vikuu vya mwelekeo na nguvu za kiroho. Kisha unaweza kusonga mbele kwa usalama na kwa furaha kila siku, kuwa kama Wao zaidi, na siku moja kurudi kuishi nao na kuwa na aina ya maisha Wanayoishi.
Songa Mbele katika Nguvu Zake
Kwa moyo wangu wote, ninashuhudia kwamba Yesu ndiye Kristo. Unapochukua hatua kuelekea Kwake, kumfikia Yeye, na umkaribishe kuwa nguvu zako, atakuja kwako na Utampata.4 Hakuna chaguo unaweza kufanya ambalo kwa namna fulani linakuweka nje ya ufikiaji Wake. Ninaamini kwa moyo wote kile nilichosema hapo awali: “Haiwezekani kwako [au mtu yeyote] kuzama chini kuliko nuru isiyo na kikomo ya Upatanisho wa Kristo ing’aavyo.”5
Iwapo utamjia Kristo, kwanza na daima ukishika amri Zake kwa “kusudi kamili la moyo” (3 Nefi 18:32), Yeye atatembea nawe katika safari ya maisha. Atachukua mkono wako na kuwa tumaini lako. Yeye atakuwa nguvu yako. Naye ataleta furaha ya kudumu, amani ya kweli na furaha kuu kwako.
Kama mmoja wa mashahidi Wake maalumu, ninashuhudia na kuahidi kwamba hii ni weli.