“Mchungaji Wako katika Mabonde ya Hofu,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Machi 2024.
Nguvu dhidi ya Wasiwasi na Hofu
Mchungaji Wako katika Mabonde ya Hofu
Katika nyakati za wasiwasi, tunaweza kusikiliza sauti ya Mchungaji wetu.
Mojawapo ya sura zinazojulikana sana za maandiko ni Zaburi 23. Watu waaminifu ulimwenguni kote kutoka katika dini nyingi wanaendelea kupata faraja katika mistari hii iliyoandikwa miaka mingi iliyopita.
Bwana ndiye mchungaji wangu; sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Hunihuisha nafsi yangu: huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; kwa maana wewe upo pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
Waandaa meza mbele yangu, machoni pa adui zangu; umenipaka mafuta kichwani pangu; kikombe changu kinafurika.
Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu, nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
Je, umeshawahi kuwa karibu na kondoo? Wanarukaruka kidogo na huanza kukimbia kwa sauti kubwa au mwendo. Hakika hawajulikani kwa kutokuwa na woga! Na pengine hilo ni jambo tunaloweza kujifunza kutoka kwa sitiari hii—Bwana anajua kwamba kila mmoja wetu atahisi hofu wakati fulani. Hakuna aibu katika hilo! Ni sehemu ya changamoto ya maisha ya duniani. Katika nyakati hizo za wasiwasi, tunaweza kusikiliza sauti ya Mchungaji wetu. Hatimaye anajaribu kutuongoza kwenye “malisho mabichi” ya amani na usalama. Hapa kuna baadhi ya njia anazotualika kwa upole kumfuata Yeye.
-
Jifunze maneno ya Mchungaji wetu—kama vile mafundisho Yake katika Agano Jipya, 3 Nefi au Mafundisho na Maagano. Tunapofanya hivyo, tunalishwa kiroho na kuwa na uwezo zaidi wa kutambua sauti Yake katika siku zijazo.
-
Omba kwa Baba wa Mbinguni katika jina la Yesu Kristo wakati wowote ili kuomba faraja na amani maishani mwako.
-
Kubali kwamba msaada wa Mwokozi unaweza kuja kwa njia nyingi, ikiwa ni pamoja na wazazi, viongozi wa Kanisa, marafiki, na hata madaktari na rasilimali nyingine za kitaaluma.
-
Kusanyika pamoja na wengine wanaompenda Mwokozi, kama vile kanisani au seminari. Hii inaweza kutuunganisha na jumuiya yenye upendo ya Watakatifu wanaofanya kazi pamoja kumfuata Mwokozi na kushinda matatizo ya kutisha kwa msaada Wake.
Nyakati nyingine kushinda woga ni safari, kama kusafiri katika bonde lenye giza, kama Zaburi 23 inavyotaja. Nicolas F., kutoka Brazil, anaweza kushuhudia kwamba ukiendelea kusonga mbele, uponyaji utakuja. Alipambana na hisia za kushindwa na hofu kwa muda mrefu.
“Nilisali sana, nikimwomba Mungu aondoe mawazo hayo mabaya akilini mwangu, nikimwomba aondoe hisia hizo mbaya,” anasema. Alipitia nyakati za kuchanganyikiwa na kutafakari makosa aliyofanya.
“Nilijaribu kupata nguvu za Mungu, lakini bado sikuhisi uponyaji Wake,” anasema Nicolas. Alichunguza maandiko kwa ajili ya mistari ihusuyo kushinda hofu na kupata nguvu katika maneno hayo. Alipata msaada kutoka kwa mama yake na wengine.
Hatimaye, alasiri moja, alihisi kuwa mzima na mwenye shukrani. Alitambua jinsi alivyotoka mbali.
“Awali, nilihisi kama niko gerezani,” anasema. “Lakini sasa ninahisi kama ninaweza kushinda vita. Ninapotafuta usaidizi wa Bwana, ninahisi tumaini.”
Iwe msimu huu wa maisha unaonekana kama kilima chenye jua au bonde lenye kivuli, una Mchungaji Mwema, Naye atatembea nawe. Yeye anakupenda! Yeye atakusaidia kupitia hili. Kaa karibu Naye, naye atakuongoza kwenye amani.