Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana
Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Ujumbe wa Mwokozi Kwako
Machi 2024


“Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Ujumbe wa Mwokozi Kwako,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Machi 2024.

Mwongozo kwenye Nguvu Zake

Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Ujumbe wa Mwokozi Kwako

Mwongozo huu unakusaidia uunganishe chaguzi zako kwa Yesu Kristo na mafundisho Yake.

Picha
Yesu Kristo

Ninasimama Mlangoni na Kubisha, na J. Kirk Richards

Fikiria unaishi katika Galilaya ya kale, miaka 2000 iliyopita. Wewe na rafiki zako mmealikwa kwenye ibada ya vijana katika sinagogi la eneo husika, kukiwa na mnenaji maalumu: Yesu wa Nazareti. Na wakati fulani katika ujumbe Wake, Yesu anawaalika vijana katika hadhira wamuulize Yeye maswali.

Ni maswali ya aina gani unadhani ungeweza kuyasikia?

Ninadhani baadhi ya maswali yangeakisi tamaduni na hali za wakati huo. Bali kwa kweli naamini mengi ya maswali yangesikika sana kama maswali tuliyonayo leo.

Kwa mfano, katika Agano Jipya, watu walimuuliza Mwokozi maswali kama haya:

  • Je, nifanye nini ili nipate uzima wa milele?1

  • Je, ninakubalika? Je, nimejumuishwa?2

  • Je, kama ndugu yangu amenikosea, ni mara ngapi ninapaswa kumsamehe?3

  • Ni kipi kitatokea kwenye ulimwengu huu siku zijazo? Je, nitakuwa salama?4

  • Je, Unaweza kumponya mpendwa wangu?5

  • Ukweli ni nini?6

  • Nitajua vipi kama ninaenenda katika njia sahihi?7

Je, sote hatujiulizi mambo haya kwa nyakati tofauti tofauti? Kwa karne nyingi, maswali haya hayajabadilika sana. Na wala huruma ya Mwokozi kwa wale ambao wanayauliza haijabadilika. Yeye anajua jinsi gani maisha yanavyoweza kuwa ya kuhangaisha na kukanganya. Yeye anajua jinsi ilivyo rahisi kupoteza njia yetu. Yeye anajua kwamba sisi tunahofia wakati mwingine kuhusu siku zijazo. Na Yeye anakuambia wewe pamoja na mimi, kama vile Yeye alivyowaambia wanafunzi Wake hapo kale:

  • “Msifadhaike mioyoni mwenu.”8

  • “Mimi ndimi njia, [na] kweli.”9

  • “Nifuateni mimi.”10

Wakati una chaguzi muhimu za kufanya, Yesu Kristo na injili Yake ya urejesho ndiyo uchaguzi bora zaidi. Unapokuwa na maswali, Yesu Kristo na injili Yake ya urejesho ndiyo jibu bora zaidi.

Hiyo ndiyo sababu ninaipenda Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana: Mwongozo wa Kufanya Chaguzi. Inatuelekeza sisi kwa Yesu Kristo ili tuweze kupokea nguvu Zake. Ninatunza nakala katika mfuko wangu wakati wote. Ninapokutana na watu kote ulimwenguni ambao wanataka kujua kwa nini sisi, kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo, tunafanya kile tunachofanya, mimi hushiriki nao mwongozo huu.

Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana inafundisha kweli za milele kuhusu Mwokozi na Njia Yake. Mwongozo huu hukualika wewe ufanye chaguzi kulingana na kweli hizo. Na unashiriki baraka zilizoahidiwa ambazo Yeye hutoa kwa wale ambao wanamfuata Yeye. Tafadhali soma, tafakari na shiriki mwongozo huu!

Mwalike Yeye Ndani

Yesu Kristo anataka kuwa sehemu ya maisha yako—daima, uwepo wa kila siku, katika nyakati mbaya na nzuri. Yeye hasimami tu mwisho wa njia, akikusubiri umfikie. Yeye atatembea pamoja nawe kila hatua ya njia hiyo. Yeye ndiye Njia!

Lakini Yeye hatalazimisha njia Yake katika maisha yako. Wewe unamwalika Yeye aje, kupitia chaguzi zako. Hii ndiyo sababu mwongozo wa kufanya chaguzi, kama vile Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, ni wa thamani sana. Kila wakati unapofanya chaguzi za haki kulingana na kweli za milele za Mwokozi, unaonesha kwamba unamtaka Yeye katika maisha yako. Chaguzi hizo zinafungua milango ya mbinguni, na nguvu Zake huja zikitiririka katika maisha yako.11

Tengeneza Muunganiko Imara

Ungeweza kukumbuka kwamba Mwokozi aliwafananisha wale ambao husikia na kutenda maneno Yake na mtu mwenye hekima, ambaye “alijenga nyumba yake juu ya mwamba.” Yeye alieleza:

“Na mvua ilinyesha, na mafuriko yakaja, na pepo zikavuma, na zikapiga ile nyumba; na haikuanguka, kwani iliwekwa msingi wake kwenye mwamba.”12

Nyumba hainusuriki katika dhoruba kwa sababu nyumba ni imara. Pia hainusuriki tu kwa sababu mwamba ni imara. Nyumba hunusurika katika dhoruba kwa sababu imeunganishwa kwa uthabiti kwenye ule mwamba imara. Ni nguvu za muunganiko huu kwenye mwamba ambazo ni muhimu.

Vile vile, tunapojenga maisha yetu, ni muhimu kufanya chaguzi nzuri. Na ni muhimu kuelewa ukweli wa milele wa Mwokozi. Lakini nguvu tunazohitaji ili kustahimili dhoruba za maisha huja wakati sisi tunapounganisha chaguzi zetu kwa Yesu Kristo na mafundisho Yake. Hicho ndicho Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana hutusaidia sisi tufanye.

Kwa mfano, rafiki zako wangeweza kujua kwamba wewe unajaribu kutotumia lugha mbaya au yenye kuumiza. Wangeweza kukuona ukimfikia kijana yule shuleni ambaye karibu watu wote wanampuuza au hata kumuonea. Lakini je, wanajua kwamba wewe unafanya chaguzi hizo kwa sababu Yesu Kristo alifundisha kwamba “watu wote ni kaka na dada zako—ikijumuisha … watu ambao ni tofauti na wewe”?13

Rafiki zako wangeweza kujua kwamba unaenda kanisani kila Jumapili. Wangeweza kutambua wakati unapozima wimbo fulani au kukataa mwaliko wa kutazama sinema fulani. Lakini je, wanajua kwamba unafanya chaguzi hizo kwa sababu wewe una “uhusiano wa agano wa furaha na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo,” na kwamba kama sehemu ya ahadi ya kumfuata Mwokozi, una shukrani “kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenzi wako daima”?14

Watu wangeweza kujua kwamba hunywi pombe au huvuti sigara au hutumii dawa za kulevya. Lakini je, wanajua kwamba wewe unafanya chaguzi hizo kwa sababu Yesu Kristo alifundisha kwamba “mwili wako ni mtakatifu,” “zawadi nzuri kutoka kwa Baba yako wa Mbinguni,” ulioumbwa kwa mfano Wake?15

Rafiki wangeweza kujua kwamba wewe haudanganyi au kusema uongo na kwamba unachukulia elimu kwa uzito mkubwa. Lakini je, wao wanajua kwamba hii ni kwa sababu Yesu Kristo alifundisha kwamba “ukweli utakuweka huru”?16

Zaidi ya yote, je, rafiki zako wanajua kwamba wewe unafanya hizi chaguzi ambazo si maarufu ili ubakie mkweli kwa viwango vya Kristo kwa sababu unajua kwamba “Yesu Kristo ni nguvu yako”?17

Yeye Ni Nguvu Yako

Ninawapa ushahidi wangu wa hakika kuwa Yesu Kristo ndiye Njia hadi kwenye siku za usoni angavu na tukufu—siku zenu zijazo. Na Yeye pia ni Njia kwenye sasa iliyo angavu na tukufu. Tembea katika njia Yake, Naye atatembea pamoja nawe. Mnaweza kufanya hili!

Rafiki zangu wadogo wapendwa, Yesu Kristo ni nguvu yenu. Endeleeni kutembea pamoja na Yeye, na Yeye atawasaidia mpae ‘kwa mbawa kama tai”18 kuelekea shangwe ya milele ambayo Yeye ameiandaa kwa ajili yenu.

Chapisha