2022
Maandiko: Neno la Mungu
Julai/Agosti 2022


“Maandiko: Neno la Mungu,” Liahona, Julai/Agosti. 2022.

Misingi ya Injili

Maandiko: Neno la Mungu

nabii wa Agano la Kale akiandika

Nabii wa Agano la Kale, na Judith A. Mehr

Maandiko ni vitabu vitakatifu ambavyo viliandikwa hasa na manabii. Maandiko hushuhudia juu ya Yesu Kristo na kufundisha injili Yake. Maandiko yaliyoidhinishwa ya Kanisa ni Biblia Takatifu (inayohusisha Agano la Kale na Agano Jipya), Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano na Lulu ya Thamani Kuu.

Agano la Kale

Agano la Kale ni kumbukumbu ya matendo ya Mungu na watu Wake wa agano katika nyakati za kale. Linahusisha mafundisho ya manabii kama vile Musa, Yoshua, Isaya, Yeremia na Danieli. Ingawa liliandikwa miaka kadhaa mingi kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, manabii wengi wa Agano la Kale waliandika kumhusu Yeye

Agano Jipya

Agano Jipya lina kumbukumbu ya kuzaliwa, maisha ya duniani, mafundisho na Upatanisho wa Yesu Kristo. Pia linahusisha mafundisho ya Mitume wa Kristo na wafuasi wengine. Agano jipya hutusaidia kuelewa jinsi ya kuishi injili ya Yesu Kristo leo.

Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo

Kitabu cha Mormoni ni kumbukumbu ya baadhi ya watu walioishi katika Amerika ya kale. Kinahusisha mafundisho kutoka kwa manabii na lengo lake kuu ni kuwashawishi watu wote kwamba Yesu ndiye Kristo. Nabii Joseph Smith alikitafsiri kutoka mabamba ya dhahabu kwa kipawa na nguvu ya Mungu.

Mafundisho na Maagano

Mafundisho na Maagano ina ufunuo uliotolewa kwa Joseph Smith na manabii wengine wa siku za mwisho. Ufunuo unafafanua jinsi Kanisa la Kristo linavyoundwa. Pia ina mafundisho ya msingi ya injili kuhusu ukuhani, ibada za injili na kile kinachotokea baada ya maisha haya.

Lulu ya Thamani Kuu

Lulu ya Thamani Kuu huhusisha vitabu vya Musa na Ibrahimu, ushuhuda wa Joseph Smith na Makala ya Imani ya Kanisa. Pia inahusisha Joseph Smith—Mathayo, sehemu ya tafsiri ya Joseph Smith ya Agano Jipya.

Kujifunza Maandiko

Manabii wametufundisha kujifunza maandiko kila siku. Kwa kufanya hivyo hutusaidia kuongeza imani yetu na kusogea karibu na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Tunapojifunza maandiko kwa sala, Roho Mtakatifu atatusaidia kupata majibu ya maswali yetu.

Manabii wa Kisasa

Wakati manabii a mitume wanapoongea leo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, maneno yao ni kama maandiko. Mfano mmoja wa hili ni mkutano mkuu. Tunaweza kusoma mafundisho kutoka kwenye mkutano kutoka toleo la mwezi Mei na Novemba la Liahona.