2022
Chombo Mikononi mwa Bwana
Julai/Agosti 2022


“Chombo Mikononi mwa Bwana,” Liahona, Julai/Agosti. 2022.

Njoo, Unifuate

Esta

Chombo Mikononi mwa Bwana

Kama tutamfuata Roho na kuwa na moyo ulio tayari, Bwana atatuongoza kutenda kile Anachohitaji sisi tukitende.

Esta

Kielelezo na Dilleen Marsh

Kuwa chombo mikononi mwa Bwana ni jambo jepesi kweli. Tunahitaji tu kuwa tayari kumruhusu Roho atuongoze na kuwa na ujasiri wa kufuata misukumo Yake. Jambo kama hilo lilitokea pale wazazi wa mke wangu walipojiunga na Kanisa mnamo 1968. Mmisionari kijana aliyehitaji kuwa chombo mikononi mwa Bwana alisaidia kuileta familia yao Kanisani.

Wakwe zangu walikutana na wamisionari mara moja, lakini baada ya hapo, baba mkwe wangu hakutaka kuendelea. Kisha mmisionari mpya, Mzee Fetzer, alihamishiwa kwenye eneo hilo, na mmisionari huyu kijana na mwenzake walihisi kupokea msukumo wa kuitembelea na kuihudumia familia hiyo. Mzee Fetzer aliweza kuigusa mioyo ya wanafamilia katika njia ambayo wamisionari wengine hawakuweza.

Kwa miezi sita iliyofuatia wamisionari walihudumia mahitaji ya familia hiyo. Baada ya muda, wazazi wa mke wangu waliguswa na Roho na kujiunga na Kanisa. Walipokea baraka zitokanazo na kufanya na kutunza maagano. Kupitia wao, familia zaidi zimejiunga na Kanisa na kupokea baraka za injili.

Hili lilitokea kwa sababu mvulana kutokea Utah alikuwa tayari “kumruhusu Mungu ashinde” katika maisha yake. Alikuwa na ujasiri wa kuacha uzuri wa nyumbani, kujifunza lugha mpya na kumtumikia Bwana huko Brazili.

Uongofu Rahisi

Takribani mwaka mmoja uliopita mke wangu, Alessandra, alipokea ujumbe kwenye simu yake kutoka kwa dada wa kata yetu huko Brazili. Ilikuwa ni zaidi ya miaka mwili sasa tangu walipoonana mara ya mwisho. Dada huyu aliandika: “Katika mojawapo ya siku mbaya sana kwenye maisha yangu, sijui ni kwa jinsi gani nilijiunga na kanisa. Nilipojiunga, uliniona. Ulishika mkono wangu na kuniambia kukaa karibu nawe. Niliongea nawe. Ulinisikiliza na kunishauri.”

Haya yalionekana mazungumzo mepesi kwa muda huo. Lakini iligeuka kuwa fursa kwa mke wangu ya kuwa chombo mikononi mwa Bwana. Alimhudumia dada huyo mpendwa aliyekuwa anapitia wakati mgumu. Alessandra hakulifikiria suala hili. Yeye alihisi kusukumwa kusikiliza na kutoa faraja na alitendea kazi msukumo. Sasa, zaidi ya miaka miwili baadaye, alipokea ujumbe huu kutoka kwa dada yule, akitoa shukrani yake.

Kupitia matukio haya nimejifunza kwamba hatuhitaji wito ili kuwa chombo mikononi mwa Bwana. Tunahitaji tu kuwa na hamu. “Kwa hivyo, kama unayo tamaa ya kumtumikia Mungu wewe umeitwa kwenye kazi hiyo” (Mafundisho na Maagano 4:3).

“Kwa ajili ya wakati kama huo.”

Katika Agano la Kale tunajifunza kuhusu mtu mwingine ambaye alitumikia kama chombo mikononi mwa Mungu. Esta alikuwa ni msichana aliyewapoteza wazazi wake katika umri mdogo. Alilelewa na binamu yake Modekai.

Baada ya Mfalme Ahasuero kumpa talaka Malkia Vashti, alimchagua Esta kuwa malkia wake mpya. “Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake” (Esta 2:17). Esta alikuwa Myahudi, lakini mfalme hakujua hilo.

Hamani, mmoja wa washauri wa mfalme, alipandishwa cheo na kuwa juu ya wana wote wa mfalme waliokuwa pamoja naye (ona Esta 3:1). Na alipanga “kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee” (Esta 3:13).

Esta alipojua mpango wa Hamani, Modekai alimshauri Esta kuongea na mfalme. Kwa kufanya hivyo kuliweka hatari kwake, lakini alikuwa jasiri kutokana na maneno ya Modekai. Alisema “walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?” (Esta 4:14).

“Nami nikiangamia, na niangamie,” Esta alisema (Esta 4:16) na aliingia kwa mfalme bila wito. Hili lilikuwa kosa la hukumu ya kifo. Kwa sababu ya ujasiri wake, Esta aliweza kumshawishi mfalme. Hatimaye, alitoa amri ya kutowaangamiza Wayahudi. Kuhusu hili, mfalme “aliwaruhusu Wayahudi wakusanyike katika kila mji na kuzisimamia maisha zao” (Esta 8:11).

Kila Jukumu Ni Muhimu

Esta alikuwa tayari kuwa chombo katika mikono ya Bwana. Maisha yake ya utiifu na ucha Mungu yalimuandaa. Ninapomfikiria akiingia chumba cha ndani cha mfalme bila wito, nashangaa ujasiri wake. Inaikumbusha kuhusu mwaliko wa Rais Russell M. Nelson kwetu sisi sote wa kumruhusu Mungu ashinde katika maisha yetu.1 Esta alikuwa radhi kumruhusu Mungu ashinde.

Binamu wa Esta Modekai pia alikuwa chombo mikononi mwa Bwana. Alimlea Esta vyema. Alimpa msaada, ujasiri na kumtia moyo. Sote tunalo jukumu la kutenda na kila jukumu lina umuhimu na uzito sawa.

Bwana alimuweka Esta katika nyumba ya mfalme kwa kusudi—kuwaokoa Wayahudi. Kama alivyofanya kwa Esta, Bwana hutuweka mahali tunapoweza kusaidia kutimiza malengo Yake. Kwa sababu hii, tunapaswa kuwa tayari na wenye kustahili tunapokumbana na fursa Alizoziandaa.

Fursa Kila Mahali

Fursa za kuwa vyombo mikononi mwa Bwana zimetuzunguka. Jukumu letu ni kujiandaa kutenda. Mara nyingi hatujui ni lini au kwa jinsi gani fursa hizo zitajitokeza. Tunapaswa kuwa wenye kustahili wenza wa Roho Mtakatifu na kuwa na moyo ulio tayari. Kisha Bwana atatuongoza kutenda kile Anachotaka tutende.

Katika Mafundisho na Maagano 35:3, Bwana anamwambia Sidney Rigdon, “nimekuangalia wewe na kazi zako. Nimezisikia sala zako, na nimekutayarisha kwa kazi iliyo kuu.”

Bwana anatujua na ana kazi kwa ajili kwa kila mmoja wetu kufanya. Wakati mwingine ni kazi ambayo ni sisi tu tunaweza kuifanya. Kazi hii inaweza kuwa nyumbani kama wazazi wakimsaidia mwana au binti anayepitia ugumu fulani. Au inaweza kuwa ndani ya majukumu yetu ya Kanisa. Kwa kweli, inaweza kuwa ya muda wowote, popote na kwa yeyote.

Rais Dieter F.Uchtdorf, akiwa Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza, alisema: “Bwana alikupa majukumu yako kwa sababu maalum. Kunaweza kuwa na watu na mioyo ambayo wewe pekee unaweza kuifikia na kuigusa. Huenda hakuna mwingine yeyote angeweza kufanya katika njia sawa na yako.”2

Rais Uchtdorf pia alisema, “Tunapofuata mfano mkamilifu wa [Mwokozi], mikono yetu inaweza kuwa mikono Yake; macho yetu, macho Yake; moyo wetu, moyo Wake.”3

Kama vile Esta, Modekai, Mzee Fetzer, mke wangu na wengine wengi, sote tunaweza kuwa vyombo katika mikono ya Bwana.