“Kwa Mwongozo wa Bwana,” Liahona, Julai/Agosti. 2022.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Kwa Mwongozo wa Bwana
Katikati ya dhiki, nilijifunza kwamba ninaweza kufanya mambo magumu.
Kama nesi wa maswala ya ganzi katika Kikosi cha Jeshi la Akiba la Marekani wakati wa janga la UVIKO-19, nilipangwa katika hospitali ya dharura huko Jacob K. Javits Convention Center Jiji la New York, kutoa huduma za dharura wakati ongezeko kubwa la mlipuko wa UVIKO-19 kwenye jiji.
Nilipoanza majukumu yangu, mambo kadhaa yalijaza akili yangu. Nilikuwa na woga wa kuwahudumia wagonjwa na kukabiliana na kirusi hiki kilichokuwa kinadhohofisha afya.
Nilihisi kama Nefi “nikiongozwa na Roho, wala sikujua kimbele vitu ambavyo ningefanya” (1 Nefi 4:6). Wazo hili lilinisaidia kuamini kwa Baba wa Mbinguni na kusali mara kwa mara kwamba nitasikia sauti Yake, kufuata maelekezo Yake na kutoa huduma bora kwa wagonjwa wangu.
Wakati wa usiku wangu wa kwanza nikihudumia, mgonjwa aliletwa katika hali ya mahututi. Mimi pamoja na wenzangu tulipoanza kuchunguza hali yake, niligundua kwamba angeweza kuwasiliana kwa Kihispania tu. Nilikuwa mtu pekee niliyeongea Kihispania, nikiwa nimejifunza wakati wa misheni yangu ya Venezuela.
Nilipoanza kuongea na mgonjwa, aliuliza kama kila kitu kitakuwa SAWA. Nilimhakikishia, nikimwambia kwamba alikuwa anapokea huduma bora iwezekanayo. Nilihisi uaminifu na faraja katika macho yake Kwa usiku uliokuwa umebakia, nilitembelea kitanda chake mara kwa mara, nikifanya tathmini na kumpa taarifa mpya. Ndani ya siku chache, hali yake iliboreka sana na aliruhusiwa kwenye nyumbani.
Wakati wa kazi yangu, nilikutana na wagonjwa wengi ambao kimsingi waliwasiliana kwa Kihispania. Uwezo wangu wa kuongea nao ulileta ahueni na hakikisho wakati wa uponyaji wao.
Nilipokuwa natafakari uzoefu huu wa kutafuta mwongozo wa mbingu wa kuwapa wagonjwa huduma bora zaidi, ninakumbuka ushauri wa Mzee Brook P. Hales wa Sabini. Alisema Baba wa Mbinguni anahusika “katika vipengele vya maisha yetu” na kwamba “tuna haki ya mwongozo wa kiungu wa kila mara kwa kupitia ushawishi na msukumo wa Roho Mtakatifu.”1
Nilitambua kwamba uwezo wangu wa kuongea Kihispania ulikuwa wenye thamani sawa na elimu yangu ya utabibu. Nilipokuwa nikiwatunza wengine, nilipata pia mtazamo wa dhahiri kwamba katikati ya dhiki, na kwa mwongozo wa Bwana, ninaweza kufanya mambo magumu.