2022
Wamisionari Wahudumu: Kuujenga Ufalme kwa njia ya Huduma na Upendo
Julai/Agosti 2022


“Wamisionari Wahudumu: Kuujenga Ufalme kwa njia ya Huduma na Upendo,” Liahona, Julai/Agosti. 2022.

Vijana Wakubwa

Wamisionari Wahudumu: Kuujenga Ufalme kwa njia ya Huduma na Upendo

Nilidhani kutumikia misheni ya huduma ilimaanisha sikuwa “mzuri vya kutosha.”

Picha
wanawake wakichora

Wakati rais wangu wa kigingi aliponiuliza kwa mara ya kwanza kama ningekuwa radhi kutumikia misheni ya huduma, wazo langu la kwanza lilikuwa, “Ndio!”

Niliamini kwamba Bwana anayo kazi kwa ajili yangu kufanya, na niliamini kwamba chochote ambacho Yeye angenihitaji mimi kukifanya kingeniletea ukuaji na furaha kwa sababu Ananipenda na anataka kilicho chema kwa ajili yangu.

Wazo langu la pili lilikuwa, “misheni ya huduma ni nini?”

Rais wangu wa kigingi alifafanua misheni ya huduma ni nini wakati tulipokutana pamoja kwenye ofisi yake Jumapili hiyo, lakini sikuielewa au umuhimu wake mpaka hapo baadaye. Wakati mwingine nilijiuliza kama wito huu ulimaanisha nina tatizo, kwa sababu nilikuwa sijaona lengo kubwa nyuma ya misheni za huduma.

Je, Nilikuwa Nahitajika?

Nilipokea wito wangu wa kutumikia takribani mwezi mmoja kabla ya misheni yangu kuanza rasmi. Hii ilimaanisha kwamba nikutane na viongozi wangu wa misheni ya huduma, kuhudhuria mkutano wa misheni ya huduma katika eneo langu na niliombwa hata kuongoza masomo ya pamoja ya wadada wengine wawili katika eneo langu kabla sijatengwa kwenye wito.

Niliutumia mwezi kati ya kupokea wito wangu na kutoa hotuba yangu ya “kwaheri” (ingawa sikwenda kokote) kujifunza kuhusu misheni za huduma na wamisionari wahudumu walionizunguka.

Katika mkutano wa misheni ya huduma niliohudhuria, nilijifunza kwamba wengi wa wamisionari wahudumu, kwa mara ya kwanza wanapoitwa, hujihisi hawakuwa wazuri vya kutosha kutumikia misheni ya kuhubiri. Kwa aibu nilikumbuka mwitikio wangu wa awali kwenye wito wangu.

Hatimaye, nilitambua kwamba sikuitwa kwenye misheni ya huduma kwa sababu sikujitosheleza, lakini kwa sababu huu ulikuwa mwelekeo wa Baba wa Mbinguni kwa ajili yangu. Sikuwa “pungufu kuliko” wamisionari wahubiri; bali, Bwana alinihitaji nisaidie kujenga ufalme Wake kupitia njia zingine za huduma. Nilipokea ushuhuda wa nguvu kwamba misheni zote ni za muhimu kwa Baba wa Mbinguni na muhimu kwa kazi Yake, kwa sababu wamisionari wote wanatamani kumtumikia Yeye na kutumikia watoto Wake.

Baada ya kujifunza kuhusu wamisionari wahudumu wengine kwenye eneo langu, kukutana nao na kusikiliza simulizi zao, nilijua walikuwa wazuri, watumishi waaminifu wa Bwana. Nilitambua kwamba japo baadhi yetu hatukuhisi vizuri mwanzoni mwa misheni zetu, sote tulifikia hitimisho sawa: Bwana anawapenda wamisionari wahudumu na kwamba tuko sahihi pale Anapotuhitaji sisi tuwe, kujifunza na kukua wakati tukimtumikia Yeye kama mikono yake hapa duniani.

Ni Kwa Jinsi Gani Wamisionari Wahudumu Hujenga Sayuni

Wamisionari ni wa muhimu katika kila nyanja wanayohudumu. Tunahitaji wamisionari wanaoacha familia zao na nyumba zao kwa miaka miwili ili kufundisha na kuhubiri injili ulimwenguni kote. Lakini pia tunahitaji kujenga jamii za Sayuni zilizojaa upendo kwa wengine na hamu ya kutumikia na kuwainua walio wanyonge miongoni mwao. Hiki ndicho wamisionari wahudumu hufanya. Tunajenga Sayuni kwa kutengeneza utamaduni wa upendo na huduma. Hii hujenga jamii yenye makaribisho, ya haki na yenye kuinua kwa waumini wote wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho—waumini wa muda wote, waongofu wapya, kila mmoja.

Misheni yangu ya huduma kwenye magazeti ya Kanisa imenisaidia kuona ni kwa jinsi gani nimebarikiwa. Nimeweza kutumia kile nilichojifunza kuhusu majaribu ya maisha yangu kusaidia kuwanyanyua wengine waliokuwa na hali ngumu. Nimejaribu kushiriki uzoefu wangu na wengine na kwa kufanya hivyo nimewaimarisha wengine kushiriki simulizi zao. Watoto wote wa Mungu ni wa muhimu. Misheni yangu ya huduma imenisaidia kuwafanya wao kuwa wavumilivu zaidi na kuniruhusu kuwapenda kama walivyo kadiri tunavyojitahidi kusogea kwa pamoja kwa Kristo.

Wamisionari wahudumu hutumia muda na nguvu zao wakijenga Sayuni katika njia nyingi tofauti lakini zenye manufaa. Baadhi husaidia kwa huduma za kutumia nguvu katika sehemu kama vile Mahali pa Ustawi au maghala ya chakula ya mahala husika. Kuna wamisionari wahudumu ambao hurembesha uwa wa hekalu na wale wanaohudumu kama wafanyakazi wahusikao na ibada hekaluni. Baadhi husaidia katika kusambaza chakula kwa watoto ambao hawana chochote shule zinapofungwa na kuwatumikia kwa kuwajenga. Wengine husaidia kusambaza injili na kuwaimarisha waumini ambao tayari wamepokea injili. Kuna hata wamisionari ambao husaidia kufanyia matengenezo magari mbalimbali ya wafanyakazi wa Kanisa.

Picha
mwanaume akirekebisha gari

Wamisionari wahudumu pia hutumikia katika njia nyingine kama kutengeneza alama kwa ajili ya maaskofu ndani ya majengo ya Kanisa, kufanya kazi kwenye studio ya Kanisa ya picha za taratibu na kusafisha vitu vingi ili kumuweka kila mtu salama katikati ya UVIKO-19. Kwa vyovyote vile majukumu yetu yanavyotofautiana, tunasaidia kujenga Sayuni kwa kuweka mazingira ya upendo na hudumu isiyo ya kibinafsi.

Sisi wamisionari wote tunashiriki katika mafunzo ya injili, kufundisha masomo, kuhudhuria kwenye masomo na mabaraza ya wilaya, na kuimarishana na kunyanyuana sisi kwa sisi na kila mmoja anayetuzunguka, iwe au isiwe sehemu ya majukumu yetu tuliyopangiwa.

Mojawapo ya mambo ya msingi ninayoyafanya huhusiana kidogo na majukumu yangu niliyopangiwa ya maudhui ya timu ya vijana wadogo kwa ajili ya magazeti ya Kanisa na zaidi huhusiana na kuwatumikia wamisionari wengine katika kundi langu eneo la Temple Square. Ninatumikia kwa kuhakikisha kwamba wanaonekana na kusikilizwa na kwamba wanajua kwamba nawajali na kwamba wao ni sehemu ya.

Je, hilo sio wanalolifanya wamisionari wote? Je, si wamisionari wote wanamhakikishia kila mmoja ulimwenguni kwamba hapa, katika ufalme wa Mungu, kuna sehemu ya muhimu na ya kila mtu kwa ajili ya watoto Wake? Wamisionari wanaohubiri husaidia kuufundisha ulimwengu kwamba ufalme wa Mungu uko duniani, na wamisionari wahudumu huwasaidia wengine kuona ufalme huo unapaswa uonekane vipi kwa kadiri tunavyojiandaa kwa Ujio wa Pili wa Mwokozi—sehemu ambayo mioyo yetu huwageukia wengine, sehemu tunayohudumu pasipo mipaka na sehemu tunayowasaidia wengine kujua kwamba wao ni sehemu ya.

Kutumikia kama ambavyo Mwokozi Angetumikia—kwa Kumfikia Mmoja

Hata hivyo tunatumikia na popote tunapotumikia, kuna jambo moja ambalo wamisionari wote hulifanya—kutumikia kama ambavyo Yesu Kristo alitumikia, kwa kumhudumia yule mmoja.

Zaidi ya kutimiza majukumu yetu binafsi, “lengo letu ni kuwasaidia wengine kuja kwa Kristo kwa kuwatumikia kama ambavyo Kristo angewatumikia. Tunatumikia kwa kujitolea katika mashirika ya hisani, shughuli za Kanisa na katika jamii. Tutahudumu katika jina Lake kwa yule mmoja, kama Yeye alivyofanya, akionyesha wema Wake wa upendo.”1

Sisi wamisionari wahudumu tunathamini maneno katika lengo letu kwa sababu tunajua Mwokozi hutuhudumia sisi binafsi na tumehisi wema Wake wa upendo. Nimehisi wema wa upendo wa Mwokozi kwenye misheni yangu kwa kumjua Yeye vizuri zaidi, kwa matatizo yangu kufanywa kuwa mepesi, kwa ushuhuda wangu kuimarishwa na kwa wamisionari wanaonizunguka kunipenda na kuniinua.

Wamisionari wahudumu wanatafuta kushiriki wema wa upendo wa Mwokozi na kila mmoja, na tunaweka wakfu maisha yetu kufanya hilo tu kwa kipindi cha misheni yetu—na kwa kipindi cha maisha yetu yote.

Muhtasari

  1. Missionary Standards for Disciples of Jesus Christ—Service Missions (2021), ndani ya jalada la mbele, ChurchofJesusChrist.org.

Chapisha