2022
Siku Moja baada ya Nyingine
Septemba 2022


“Siku Moja baada ya Nyingine,” Liahona, Sept. 2022.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Siku Moja baada ya Nyingine

Tunayo shukrani kwa waumini wa ajabu wa kata yetu, ambao walitusaidia juu ya kijana wetu mwenye ugonjwa wa akili.

mvulana

Josh wakati wa safari ya hekaluni hivi karibuni.

Picha ya Joshua kwa Hisani ya mwandishi

Mwana wetu Joshua alipokuwa na umri wa miezi 18, tuligundua mambo mageni katika tabia yake. Josh angeliweza kukariri karibia kila neno katika kila wimbo kwenye maonyesho ya runinga alizokuwa ameangalia, lakini alikuwa amechelewa kuongea. Siku moja mama mkwe wangu alisema kwamba Josh alionyesha dalili za ugonjwa wa akili. Mtaalamu alituambia kitu hicho hicho.

Mke wangu Elizabeth, akajizamisha mwenyewe katika vitabu kuhusu ugonjwa wa akili. Pia akamwandikisha Josh katika programu ili kumsaidia. Alikuwa amedhamiria kwamba mtoto anapata mwanzo bora katika maisha ambayo tungeweza kumpatia.

Katika siku ambazo nilipata msongo wa mawazo kuhusu siku za baadae, Elizabeth angenituliza. Aliniambia kwamba tunahitajika kuchukulia mambo haya siku moja baada ya nyingine.

“Tunahitaji kuridhika na kila kitu kipya Josh anachojifunza badala ya kufokasi katika yote yasiyojulikana juu ya siku za baadae,” alisema.

Alipozidi kukua, Josh akawa hatiliziki kanisani. Ili kumfanya asivuruge darasa la Msingi au asiwadhuru watoto, nilimweka pajani pangu Alihangaika, alifurukuta, na kupiga mieleka na mimi kwa saa zote tatu za kanisa. Mara nyingi nilirudi nyumbani nikiwa nimechubuliwa na nimechoka.

“Kwa nini tusimwache tu nyumbani asiende kanisani na tufanye zamu ya kubaki naye?” Mimi nilishauri.

“Kama hatuendelei kumpeleka,” Elizabeti alijibu, “atajifunza kwamba kama atacharuka, anaondoka kanisani.” Nilijua alikuwa sahihi.

Siku moja mama wa familia nyingine yenye mtoto aliye na ugonjwa wa akili aliniambia, “Josh atakapofikia umri wa miaka minane na akampata Roho Mtakatifu, atakuwa vizuri tu!”

Nilitilia shaka maneno yake, lakini alipofikisha miaka minane, alimpokea Roho Mtakatifu na akawa vizuri—kidogo.

Josh alipokuwa na umri mkubwa zaidi, akapokea ukuhani. Akapitisha sakramenti, na akajifunza umuhimu wa huduma. Washiriki wa akidi yake ya ukuhani walijifunza dansi la muziki wa miaka ya 80 kwa video pamoja na Josh na wakaonyesha kwenye tafrija ya kata.

Kata yetu ilikuwa ya kupendeza kwa Josh. Waumini walitabasamu alipokuwa akipitisha sakramenti huku akifanya miondoko ya dansi ya miaka ya 80 huko.

Josh ana umri wa miaka 17 sasa. Ni mwanamziki mwenye kipaji ambaye anaandika nyimbo. Anapenda kuigiza na anaonekana mara kwa mara katika kumbi za maonyesho za shule na za mtaani.

Tunayo shukrani kuwa wazazi wa Josh na kushiriki katika safari yake. Hatuna uhakika siku za baadae kuna nini, lakini tumedhamiria kuishi kikamilifu kila siku pamoja naye.