“Matumaini na Faraja katika Kristo,” Liahona, Sept. 2022.
Matumaini na Faraja katika Kristo
Na tushikilie ahadi kwamba Bwana anakumbuka na kuwazawadia Watakatifu Wake walio waaminifu.
Jens na Ane Cathrine Andersen walikuwa na ushuhuda wa kina na wa kudumu juu ya ukweli wa injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Licha ya mateso yaliyotokana na wakundi yaliyokasirika na wana jumuiya na wanaparokia, wao walijiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho mwaka 1861.
Ifikapo majira ya kuchipua mwaka uliofuata, walitii wito wa Sayuni, ikiashiria maili 5,000 (kilometa 8,000) hadi katika Bonde la Salt Lake. Kukusanywa kwa Israeli kulimaanisha kuacha nyuma maisha yao mazuri huko—ikijumuisha marafiki, wanafamilia, na shamba zuri ambalo kwa vizazi vingi limekuwa likirithishwa kutoka kwa baba kwenda kwa mwana wa kwanza. Likiwa katika kijiji cha Veddum, karibu na Aalborg, kwenye Peninsula ya Jutland yenye rutuba huko kaskazini mwa Denmark, shamba lilikuwa kubwa na lenye kuzalisha. Liliajiri dezeni kadhaa za wafanyakazi na lilileta heshima na fedha kwa familia ya Andersen.
Kushiriki mali hizo pamoja na waongofu wenzao, Jens na Ane Cathrine walilipa gharama za uhamiaji za waongofu wenzao takribani Watakatifu wengine 60 waliokuwa wakisafiri kwenda Sayuni. Mnamo Aprili 6, 1862, wakina Andersen, pamoja na mwana wao mwenye umri wa miaka 18, Andrew, waliungana na Watakatifu wengine 400 wa Kidanishi kwenye meli ndogo Albioni na wakasafiri kwenda Hamburg, Ujerumani. Wakafika huko Hamburg siku mbili baadaye, wakaungana na Watakatifu wengine zaidi kwenye meli kubwa ili kuanza safari yao ya kuvuka bahari ya Atlantiki.
Shangwe ya kukusanyika Sayuni, hata hivyo, punde iligeuka kuwa huzuni. Watoto kadhaa ambao walipanda kwenye Albioni walikuwa wamebeba virusi vya ugonjwa wa surua. Ugonjwa ulifagia wahamiaji wa rika mbali mbali, watoto 40 na wakubwa kadhaa walifariki dunia na walizikwa baharini. Miongoni mwao alikuwemo mwenye-miaka-49 Jens Andersen, ambaye ni babu wa babu wa baba yangu.
Ndoto ya Jens ya kufika na kujenga Sayuni pamoja na familia yake na Watakatifu wenzake wa Kidanishi iliisha siku 10 tu nje ya Hamburg. Mwanahistoria mmoja aliandika, “Mkombozi mmoja ambaye kama Musa katu hakuweka mguu wake juu ya nchi ya ahadi alikuwa Jens Andersen wa [Veddum], Aalborg, ambaye alikuwa amewasaidia wahamiaji wenzake wasiopungua sitini; alikutana na mauti kwenye Bahari ya Kaskazini mwaka 1842 muda mfupi baada ya kuondoka [Ujerumani].”1
Majaribu ya Duniani
Je, Dhabihu ya familia ya Andersen—ya kuacha shamba lao la faraja na kumpoteza mume na baba yao mpendwa—ilistahili? Ninao uhakika ulimwengu ungesema hapana. Lakini ulimwengu unakosa imani, kuona mbali, na ule “mtazamo wa milele”2 unaotolewa na injili ya urejesho ya Yesu Kristo.
Mtazamo huo unatusaidia kuelewa maisha yetu ya hapa duniani na majaribu yake mengi. Tunakabiliana na hofu, usaliti, majaribu, dhambi, upotevu, na upweke. Magonjwa, majanga, msongo wa mawazo, na mauti yanayozima ndoto zetu. Baada ya muda, mizigo yetu inaonekana kuwa mikubwa zaidi kuliko tunavyoweza kuibeba?
“Ingawaje maelezo ya kina yatatofautiana, mikasa, mitihani na majaribu yasiyotarajiwa, yote ya kimwili na ya kiroho, huja kwa kila mmoja wetu kwa sababu haya ni maisha ya duniani,” alisema Mzee Neil L. Andersen wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Yeye aliongeza: “Tunatafuta furaha. Tunatamani amani. Tunatumainia upendo. Na Bwana anatunyunyizia baraka tele za ajabu. Lakini zikiwa zimechanganyika pamoja na ile shangwe na furaha, kitu kimoja ni hakika: kutakuwa na nyakati, saa, siku, wakati mwingine miaka ambapo nafsi yako itajeruhiwa.”3
Tunaukabili bila woga uchungu ili tupate kuonja utamu (ona Mafundisho na Maagano 29:39). Katika maneno ya nabii Isaya, sisi sote tunasafishwa—na kuchaguliwa—“katika tanuru la mateso” (Isaya 48:10).
Ahadi ya Upatanisho
Huzuni ni sehemu ya “mpango mkuu wa furaha” wa Baba (Alma 42:8; ona pia 2 Nefi 2:11). Lakini kitovu cha mpango huo ni faraja na matumaini ambayo huja kutokana na “ule Upatanisho mkuu na mtukufu.”4 Kupitia Upatanisho Wake, Yesu Kristo alikuja kutuokoa. (Ona Alma 36:3.)
Mwokozi “alishuka chini ya vitu vyote” (Mafundisho na Maagano 88:6) ili kwamba aweze kujichukulia juu yake Mwenyewe magumu na makosa yetu. Yeye anajua jinsi ya kutuhudumia sisi kwa ufahamu kamili wa wapi na kwa nini inauma.
“Kwa vile Mwokozi ameteseka kila kitu na vitu vyote ambavyo sisi tungeweza kuhisi au kupitia, Yeye anaweza kumsaidia aliye dhaifu kuwa imara,” alisema Rais James E. Faust (1920–2007), Mshauri wa Pili katika Urais wa Kwanza. “Yeye binafsi amepitia yote haya. Anaelewa maumivu yetu na atatembea nasi hata katika saa yetu ya kiza zaidi.”5
Hiyo ndiyo sababu sisi tunaweza kutia nanga ya matumaini yetu ya mwisho katika Yeye na Upatanisho Wake.
“Wetu sisi ni ulimwengu wa kutazamia misiba na beuzi—ambao, kwa sehemu kubwa, hauna matumaini katika Yesu Kristo au katika mpango wa Mungu wa furaha kwa wanadamu,” alisema Rais Russell M. Nelson. “Kwa nini ugomvi na huzuni ya jinsi hii ulimwenguni? Sababu ni wazi kabisa. Kama hakuna matumaini katika Kristo, hakuna utambuzi wa mpango mtakatifu kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu. Pasipo elimu hiyo, watu kimakosa kabisa wanaamini kwamba kuwepo kwao leo kunafuatiwa na kufa kwao kesho—kwamba furaha na ushirikiano wa kifamilia ni wa kupita tu.”6
Ninapata matumaini na uponyaji katika Yesu Kristo ninapohudhuria hekaluni na kusikiliza maneno ya manabii walio hai. Ninapata faraja ninapojifunza maandiko ambayo yanashuhudia juu ya Yake na Upatanisho Wake. Wakati maisha ya duniani yanapotishia “kuangamiza amani yako,”7 geukia kile ninachokiita “maandiko ya ulinzi.” Hapa ni baadhi ya mapendeleo yangu:
Agano la Kale
-
“Amemeza mauti hata milele; na Bwana Mungu atafuta machozi katika nyuso zote” (Isaya 25:8).
-
“Kwa hakika amejichukulia unyonge wetu, na kubeba huzuni zetu. … “Lakini alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu: adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake; na kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:4–5).
Agano Jipya
-
Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28).
-
Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu” (Yohana 16:33).
Kitabu cha Mormoni
-
“Na atajichukulia kifo, ili afungue kamba za kifo ambazo zinafunga watu wake; na atajichukulia unyonge wao, ili moyo wake ujae rehema, kulingana na mwili, ili ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao” (Alma 7:12).
-
“Na ni kitu gani mtakachotumainia? Tazama nawaambia kwamba mtakuwa na tumaini kupitia upatanisho wa Kristo na uwezo wa kufufuka kwake, kuinuliwa kwa maisha ya milele, na hii kwa sababu ya imani yenu kwake kulingana na ile ahadi” (Moroni 7:41).
Mafundisho na Maagano
-
“Kwa hiyo, changamkeni, na msiogope kwani mimi Bwana nipo pamoja nanyi, na nitasimama karibu yenu; nanyi mtanishuhudia, hata Yesu kristo, kuwa mimi ndimi Mwana wa Mungu aliye hai, kwamba nilikuwepo, kwamba nipo, na kwamba nitakuja” (Mafundisho na Maagano 68:6).
-
“Kwa hiyo, msiogope hata kwa mauti; kwani katika ulimwengu huu shangwe yenu siyo kamilifu, bali ndani yangu shangwe yenu ni kamilifu” (Mafundisho na Maagano 101: 36).
Hizi na lundo la mistari mingine inashuhudia, katika maneno ya Rais Boyd K. Packer (1924–2015), Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, juu ya “ahadi ya upatanisho wa Yesu Kristo.”8
Maombi ya Nabii
Tunapoelewa umuhimu wa nafasi ya Mwokozi anayocheza katika furaha yetu sasa na katika ulimwengu ujao, tunaelewa kwa nini Rais Nelson anatuomba sisi kumfanya Yeye kuwa msingi wa maisha yetu:
“Ninakuombeni kutenga muda kwa ajili ya Bwana! Fanya msingi wako mwenyewe wa kiroho kuwa imara na unaoweza kuhimili majaribu ya kila wakati kwa kufanya mambo yale ambayo yanamruhusu Roho Mtakatifu kuwa pamoja nawe daima.” Kutenga muda kwa ajili ya Bwana, Rais Nelson aliongeza, kunajumuisha kutenga “muda kwa ajili ya Bwana katika nyumba Yake takatifu” kwa njia ya huduma na kuabudu hekaluni.9
“Kwa kila mmoja wenu ninyi ambao mmefanya maagano ya hekaluni, ninawasihi mtafute—kwa sala na kwa mwendelezo—kuelewa maagano na ibada za hekaluni. …
“… Wakati mabadiliko ya aina yoyote yanapotokea katika maisha yako, mahali salama zaidi pa kuwa kiroho ni kuishi ndani ya maagano yako ya hekaluni!
“Tafadhali mniamini ninaposema kwamba wakati msingi wako wa kiroho unapojengwa kwa uimara juu ya Yesu Kristo, hauhitaji kuogopa.”10
Umechongwa juu ya Viganja vya Mikono Yake
Je, Ni nini kilikuja kutokana na Ane Catherine na mwanawe, Andrew? Je, walikata tamaa na kurudi Denmark kufuatia safari yao ya huzuni ya wiki sita njiani kwenda Jijini New York? Hapana. Wakitegemea shuhuda zao juu ya Mwokozi na mpango wa wokovu, na kutumaini katika Mungu, kwa ujasiri walisonga mbele kwa treni, boti liendeshwalo kwa mvuke, na treni ya mizigo. Walifika Bonde la Salt Lake mnamo September 3, 1862, na kujiunga katika kujenga Sayuni.
Walikaa huko Ephraim, Utah, mahali ambapo Andrew alioa na kuanzisha familia. Baadaye, Andrew alihamisha familia yake, iliyojumuisha mama yake kwenda, Lehi, Utah, mahali ambapo alikuja kuwa mkulima mwenye mafanikio, mtunza fedha, na meya. Alihudumu misheni ya miaka mitatu kwenye nchi yake ya asili, zaidi ya miongo miwili katika uaskofu, na zaidi ya miongo mitatu katika halmashauri kuu au katika akidi ya makuhani wakuu. Watatu miongoni mwa watoto wake walihudumu misheni huko Denmark na Norway.
Kwa macho ya kibinadamu, hatuwezi kuona mwisho wenye utukufu unaoanza na mwanzo wenye macho yenye machozi. Lakini kwa imani katika Kristo, tunaweza kutazama siku za usoni kwa matumaini. Na tunaweza kushikilia ahadi kwamba Bwana anakumbuka na kuwazawadia Watakatifu Wake, wakiwemo Jens, Ane Catherine, na Andrew. Bwana anawakumbuka, na anatukumbuka sisi. Yeye ameahidi:
“Bado sitakusahau wewe.
“Tazama, nimekuchora viganjani mwa mikono yangu” (Isaya 49:15–16).