“Kumwacha Bwana Ayaongoze Maisha Yako,” Liahona, Sept. 2022.
Vijana Wakubwa
Kumwacha Bwana Aongoze Maisha Yako
Sikuwa daima naweza kuona jinsi ambavyo mambo yangekuwa, lakini nilipotenda kwa imani, Bwana alinibariki.
Dini haikuwa kitu maarufu nyumbani mwetu nilipokuwa ninakua—ingawa wazazi wangu walikuwa wapenda dini katika sehemu kubwa ya maisha yao yote, uchunguzi wa ugonjwa usiotibika wa baba yangu, miongoni mwa majaribu mengine, yaliwapeleka kuacha dini waliyolelewa. Nilikuwa na miaka minne wakati alipofariki kwa saratani na mimi nilikuwa ndio mdogo katika watoto 13, na mama yangu mjane hakuweza kuamini Mungu angeweza kuruhusu kitu kama hicho kitokee kwa famila yetu.
Lakini niilipokuwa na umri wa miaka 14, nilihisi kitu fulani kinakosekana katika maisha yangu. Nilijiuliza kama nilikuwa na kusudi kubwa zaidi ambalo sikuwa nalijua. Nilijisikia kama Joseph Smith, wakati “akili yangu ilipoitwa kwenye tafakuri nzito na mashaka makubwa” (Joseph Smith—Historia ya 1:8). Ingawa sikuwa nimewahi kusikia juu ya Joseph Smith kwa wakati huo, nilianza utafiti unaofanana sana na wake nilipokuwa nahudhuria makanisa mengi kwa matumaini kwamba ningeupata ukweli.
Na nilifanya hivyo, siku moja, nilipowaona vijana wawili waliovalia suti wakienda kwenye nyumba ya jirani yangu. Nilidadisi na kuwauliza kama ninaweza kuja kwenye miadi yao. Baada ya kupata ruhusa ya mama yangu, nilianza majadiliano ya kimisionari na mwishowe nikajiunga na Kanisa.
Kujiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kumenisaidia kupata kusudi langu, hususani miaka ya ujana wangu mkubwa ambapo nilipaswa kufanya maamuzi mengi ambayo watu wanaonizunguka walikuwa hawakubaliani nayo. Lakini ingawa nilikuwa na kusudi na mwelekeo, sio daima nilikuwa na uhakika wa jinsi mambo yatakavyo kuwa.
Hata hivyo, nilipokuwa nakabiliwa na yasiyojulikana na yasiyo na uhakika na mabadiliko mengi, mwongozo wa Baba wa Mbinguni ulikuwa naupata kila siku nilipokuwa namgeukia Yeye. Nilijifunza baadhi ya njia ya kumtegemea Yeye na katika imani yangu ambayo ilinisaidia kusonga mbele na kuendelea kutafuta kusudi langu.
Kusonga Mbele na Misheni
Kwenye umri ambao wengi wa rika yangu walikuwa wanajiandaa kwenda chuoni, nilikuwa nikiangalia jinsi ninavyoweza kwenda misheni. Huko Chile, kila mmoja lazima afanye mtihani kabla ya kwenda chuo kikuu. Na mtihani unatolewa mara moja tu kwa mwaka, hivyo basi, kama ningeenda misheni siyo tu ningechelewesha elimu yangu kwa miaka miwili lakini pia nitasubiri miaka ya nyongeza miwili ili niende shuleni baada ya hapo.
Familia yangu, hususani mama yangu, alipinga misheni. Ilikuwa muhimu sana kwake yeye kwamba nipokee elimu ya chuoni. Lakini niliamini kwamba Bwana angenisaidia mimi kufanya kile kilicho muhimu, hivyo kwa sala nilianza kujiandaa.
Askofu wangu alipofika nyumbani kwangu akiwa na nyaraka zangu za misheni zilizokamilika na kuomba sahihi ya mama yangu, alishangazwa; sikuwa nimemwambia kama naendelea na mchakato. Ilinibidi nichukue muda wa kumshawishi, lakini Bwana alilainisha moyo wake na alimsaidia kuelewa kwamba nilitaka kuhudumu.
Injili ilinipa uhakika kwamba nilikuwa nafanya kitu sahihi, lakini ni kwa kusonga mbele tu, hatua kwa hatua, kwa imani—hata pamoja na maswali na pasipo uhakika—kwamba niliendelea kwenda mbele.
Kufuatia Ufunuo baada ya Ufunuo
Kurudi nyumbani kutoka kwenye misheni yangu pia kulimaanisha kurudi kusiko na uhakika. Nilipokuwa natafuta mwongozo kutoka kwa Baba wa Mbinguni kupitia sala na kufunga, nilipokea ufunuo kwamba nilihitaji kuhamia Marekani na kuhudhuria Chuo Kikuu cha Brigham Young, ambako kulionekana kama kazi isiyo wezekana.
Nilifanya kadiri nilivyoweza na kuchukua hatua bora iliyofuata. Wakati mwingine nilijisikia kama siendi ko kote—nilifanya kazi kwa bidii kadiri nilivyoweza, lakini sikujua kwa hakika kwamba jitihada zangu zingenisaidia kufikia malengo yangu. Hata hivyo, lengo langu kuu lilikuwa ni kufuata kile ambacho Bwana anataka mimi nifanye, na lengo hilo lilikuwa la thamani kwangu.
Nilipokuwa nikifanya jitihada hizo, siku moja nilihisi kupata mwongozo wa kiungu wa kumfikia rafiki yangu mwema ambaye alikuwa anatokea Marekani na alikuwa akiishi katika mji wangu wa nyumbani. Sikujua jinsi mambo yatakavyokuja kuwa kwa wakati huo—nilimwomba kwa sababu tu Roho alikuwa amenielekeza kufanya hivyo—lakini rafiki yangu na baba yake waliishia kuwa vyombo katika kunisaidia kujua kitu cha kufanya ili kuomba na kupata visa niliyohitaji ili kusoma huko BYU. Kwa msaada wao na kwa dhabihu kubwa iliyofanywa na mama yangu kulipia usafiri wangu, nilifika huko. Ilikuwa ni muujiza.
Maisha yangu yaliendelea kwenda mbele katika njia hiyo hiyo. Ningefanya kadiri ya uwezo wangu na kisha nipate mwongozo wa kiungu, kitu kimoja kimoja, kwa kile ninachopaswa kukifanya baadae. Katika namna hiyo, nilipata kazi kwenye kituo cha mafunzo ya umisionari, nilipata njia ya kulipa ada ya masomo, nilifanya uamuzi wa taaluma, hatimaye nilihitimu, na nikaoa.
Majibu niliyopokea hayakuwa daima mara moja, na kamwe sikupata mpango ulio kamilika wenye maelezo ya kina, lakini nilipokea uhakikisho kwamba Bwana alipendezwa na mwelekeo niliokuwa nikiendea.
Ufunuo Unapokuwa Hauleti Maana
Miaka michache baadae, nilijifunza jinsi dhabihu ilivyo muhimu katika kuishi injili. Kama tunataka Bwana atupe kusudi na mwelekeo lazima tuwe tayari kuchukua mwongozo huo.
Baada ya shule, mambo hayakwenda kulingana na mpango na kampuni niliyokuwa nikifanya kazi, hivyo mke wangu na mimi tulikuwa na chaguzi mbili tu: kubaki Marekani au turudi Chile. Sote kwa uwazi kabisa tulihisi kwamba tunahitajika kurudi Chile. Inawezekana ikaonekana ni kawaida kutaka kurudi nyumbani, lakini hili lilikuwa kwenye wakati mgumu sana. Hapakuwa na kazi nyingi huko Chile. Nilikuwa napata taabu kuuza nyumba yetu. Kifedha na kimpangilio, halikuwa jambo rahisi kulifanya; hata familia zetu walifikiri tunakuwa watu wasio na busara.
Je, unafanya nini wakati ufunuo unapoingia kwenye mgogoro na akili ya kawaida? Ingawa ilikuwa vigumu, mke wangu na mimi tulijua kitu cha kufanya. Tulijikumbusha kwamba injili ndiyo imetufikisha sisi pale tulipo. Bila Bwana, nisingeweza kupata mwongozo wa kiungu ambao ulinisaidia kutumikia misheni, kupokea elimu yangu, na kukutana na mke wangu. Tunapaswa kuamini tu kwamba kwa sababu iwayo yo yote ile, tunahitajika Chile.
Tuliiacha nyumba yetu mikononi mwa askofu ili ipangishwe hadi pale atakapoweza kuiuza, nasi tukahama zetu. Ilikuwa vigumu, lakini tulipitia baraka na miujiza mingi tulipoitikia wito wa Bwana. Bwana anajua pale tunapohitajika na mahali tunapoweza kuhudumia vyema zaidi makusudi Yake, na Yeye anatubariki kwa ajili ya utiifu wetu.
Kutafuta Suluhisho pamoja na Bwana
Ninatumaini kwamba vijana wakubwa leo watafuata mfano wa kaka wa Yaredi. Ingawa Wayaredi walijua kwamba walihitajika kusafiri kwenda nchi ya ahadi, hawakuwa na uhakika sahihi wa jinsi ya kwenda safari hiyo. Wakati kaka wa Yaredi “alipolilingana jina na Bwana” (Etheri 2:15), Yeye alimpa masuluhisho machache. Bwana alimwambia ajenge mashua na akampa mwongozo juu ya namna kuingiza hewa kwa ajili wale watakao kuwemo ndani ya mashua hizo.
Bwana alimuuliza kaka ya Yaredi swali hili, “ Ungetaka nifanye nini ili muwe na mwangaza kwenye vyombo vyenu?” (Etheri 2:23). Badala ya kumwambia kaka wa Yaredi hasa kitu cha kufanya , Bwana alimwambia aende na kutafuta suluhisho yeye mwenyewe.
Hivyo ndivyo ilivyofanyika katika maisha yangu. Wakati mwingine Bwana ananipa maelekezo ya wazi kabisa. Wakati mwingine ananisubiri nimwendee nikiwa na mawazo yangu mimi mwenyewe. Katika njia yo yote, hata hivyo, ni muhimu kwamba nimshirikishe Yeye katika mchakato huo. Kufunga, kuomba, na kushauriana na Bwana ni hatua muhimu kwa mtu ye yote anayejaribu kufanya maamuzi kuhusu maisha yao.
Kwa kijana mkubwa ye yote anayetafuta kusudi lililoongezeka, ninampa ushauri huu: Mgeukia Bwana kwa ajili ya ufunuo. Rejelea mara kwa mara kwenye baraka yako ya Kipatriaki Na uwe tayari kutoa dhabihu ya mambo yasiyo na umuhimu katika maisha yako kama Bwana anakuambia kwamba analo kusudi lililo kubwa kwa ajili yako.
Mimi nampenda Bwana. Injili ndio kila kitu kwangu mimi. Ninajua kwamba Bwana anaona uwezekano wako wa kuwa na anataka kukusaidia upate kusudi lako la kiungu.