Miito ya Misheni
Sura ya 3: Somo la 2—Mpango wa Wokovu wa Baba wa Mbinguni


“Sura ya 3: Somo la 2—Mpango wa Wokovu wa Baba wa Mbinguni,” Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023)

“Sura ya 3: Somo la 2,” Hubiri Injili Yangu

Sura ya 3: Somo la 2

Mpango wa Wokovu wa Baba wa Mbinguni

Sanamu ya Christus

Watu Wanaweza Kujiuliza

  • Je! dhumuni la maisha ni lipi?

  • Nilitoka wapi?

  • Je, kuna Mungu ambaye anajali kuhusu mimi? Je, ni kwa jinsi gani ninaweza kuhisi kwamba Yeye anajali?

  • Je, ni kwa jinsi gani ninaweza kuamini katika Mungu wakati mambo mengi mabaya yanatokea?

  • Je, kwa nini maisha ni magumu sana wakati mwingine? Je, ni kwa jinsi gani ninaweza kupata nguvu katika nyakati hizi?

  • Je, ni kwa jinsi gani ninaweza kuwa mtu mwema?

  • Je, ni nini kitatokea baada ya mimi kufa?

Injili ya Yesu Kristo iliyorejeshwa hutusaidia tujibu maswali muhimu ya nafsi. Kupitia injili, tunajifunza kuhusu utambulisho wetu wa kiungu na uwezekeno wetu wa milele kama watoto wa Mungu. Injili inatupatia sisi tumaini na kutusaidia tupate amani, furaha, na maana. Kuishi injili hutusaidia tukue na tupate nguvu wakati tunapokabiliana na changamoto za maisha.

Mungu hutaka yaliyo mema kwa ajili ya watoto Wake na hutamani kutupatia baraka Zake kuu, ambazo ni kutokufa na uzima wa milele (ona Musa 1:39; Mafundisho na Maagano 14:7). Kwa sababu Yeye anatupenda, Yeye ametoa mpango kwa ajili yetu kupokea baraka hizi. Katika maandiko, mpango huu unaitwa mpango wa wokovu, mpango mkuu wa furaha, mpango wa ukombozi (ona Alma 42:5, 8, 11, 13, 16, 31).

Katika mpango wa Mungu, kila mmoja wetu hufanya safari kupitia maisha kabla ya kuja duniani, kuzaliwa, maisha ya duniani, na maisha baada ya kifo. Mungu ametoa kile tunachohitaji wakati wa safari hii ili kwamba baada ya sisi kufa, hatimaye tuweze kurudi katika uwepo Wake na kupokea utimilifu wa shangwe.

Yesu Kristo ni kiini cha mpango wa Mungu. Kupitia Upatanisho Wake na Ufufuko, Yesu alifanya iwezekane kwa kila mmoja wetu kupokea kutokufa na uzima wa milele.

Wakati wa maisha yetu hapa ulimwenguni, hatukumbuki maisha yetu kabla ya kuzaliwa. Wala hatuelewi kikamilifu maisha baada ya kifo. Hata hivyo, Mungu alifunua kweli nyingi kuhusu sehemu hizi za safari yetu ya milele. Kweli hizi zinatoa ufahamu wa kutosha kwa ajili yetu ili tuelewe dhumuni la maisha, tupate shangwe, na tuwe na tumaini la mambo mazuri yatakayokuja. Ufahamu huu ni hazina takatifu ya kutuongoza sisi wakati tukiwa hapa duniani.

Mapendekezo ya Kufundisha

Sehemu hii hutoa sampuli ya muhtasari wa kukusaidia ujiandae kufundisha. Pia inajumuisha mifano ya maswali na mialiko unayoweza kutumia.

Unapojiandaa kufundisha, kwa sala fikiria hali na mahitaji ya kiroho ya kila mtu. Amua kile kitakachokuwa chenye msaada zaidi ili ukifundishe. Jiandae kuelezea maneno ambayo watu wanaweza kuwa hawayaelewi. Panga kulingana na muda ulionao, ukikumbuka kufanya masomo yawe mafupi.

Chagua maandiko ya kutumia wakati unapofundisha. Kipengele cha somo cha “Msingi wa Mafundisho” hujumuisha maandiko mengi yenye msaada.

Fikiria ni maswali yapi ya kuuliza unapofundisha. Panga mialiko ya kutoa ambayo itamtia moyo kila mtu kutenda.

Sisitiza baraka za Mungu zilizoahidiwa, na shiriki ushuhuda wako wa kile unachofundisha.

wamisionari wakiifundisha familia

Ni kipi unachoweza Kuwafundisha Watu kwa Dakika 15–25

Chagua moja au zaidi ya kanuni zifuatazo kuhusu mpango wa wokovu ili kuzifundisha: Msingi wa mafundisho kwa kila kanuni umetolewa baada ya muhtasari huu.

Maisha kabla ya Kuzaliwa Duniani: Dhumuni na Mpango wa Mungu kwa ajili Yetu Sisi.

  • Sisi sote tu watoto wa kiroho wa Mungu. Yeye alituumba sisi kwa mfano Wake.

  • Tuliishi pamoja na Mungu kabla hatujazaliwa duniani. Sisi ni washiriki wa familia Yake. Yeye anamjua na kumpenda kila mmoja wetu.

  • Mungu ametoa mpango kwa ajili ya furaha yetu na maendeleo yetu katika maisha haya na ya milele.

  • Katika maisha yetu kabla ya kuzaliwa duniani, tulichagua mpango wa Mungu. Hii ilimaanisha kuja duniani ili tuweze kupiga hatua inayofuata katika maendeleo yetu ya milele.

  • Yesu Kristo ni kiini cha mpango wa Mungu. Yeye hufanya iwezekane kwetu kupata kutokufa na uzima wa milele.

Uumbaji

  • Chini ya maelekezo ya Mungu, Yesu Kristo aliumba dunia.

Anguko la Adamu na Hawa

  • Adamu na Hawa walikuwa wa kwanza kati ya watoto wa kiroho wa Mungu kuja duniani. Mungu aliumba miili yao na kuwaweka katika Bustani la Edeni.

  • Adamu na hawa walifanya kosa, wakafukuzwa nje ya bustani, na walitengwa kutoka katika uwepo wa Mungu. Tukio hili linajulikana kama Anguko.

  • Baada ya Anguko, Adamu na Hawa wakawa wenye mwili wenye kufa. Kama wanaoweza kufa, waliweza kujifunza, kuendelea, na kuwa na watoto. Pia waliweza kupatwa na huzuni, dhambi na mauti.

  • Anguko lilikuwa hatua ya kusonga mbele kwa wanadamu. Anguko lilifanya iwezekane kwetu kuzaliwa duniani na kuendelea katika mpango wa Baba wa Mbinguni.

Maisha yetu Duniani

  • Katika mpango wa Mungu, tulihitaji kuja duniani ili tuweze kupokea miili, kujifunza na kukua.

  • Duniani, tunajifunza kutembea kwa imani. Hata hivyo, Baba wa Mbinguni hajatuacha peke yetu. Yeye ametoa vipawa vingi na miongozo ya kutusaidia turudi katika uwepo Wake.

Upatanisho wa Yesu Kristo

  • Kila mmoja wetu hutenda dhambi, na kila mmoja wetu atakufa. Kwa sababu Mungu anatupenda, Yeye alimtuma Mwanaye, Yesu Kristo, kuja duniani kutukomboa kutokana na dhambi na kifo.

  • Kwa sababu ya dhabihu ya Yesu ya kulipia dhambi, tunaweza kusamehewa na kusafishwa dhambi zetu. Mioyo yetu inaweza kubadilishwa kwa wema pale tunapotubu. Hii hufanya iwezekana kwetu kurudi katika uwepo wa Mungu na kupokea utimilifu wa shangwe.

  • Kwa sababu ya Ufufuko wa Yesu, sisi sote tutafufuka baada ya kufa. Hii inamaanisha kwamba roho na mwili wa kila mtu vitaunganika tena, na kila mmoja wetu ataishi milele katika mwili mkamilifu, uliofufuka.

  • Yesu Kristo hutoa faraja, tumaini, na uponyaji. Dhabihu Yake ya kulipia dhambi ni dhihirisho la msingi la upendo Wake. Yale yote yasiyo haki katika maisha yanaweza kufanywa kuwa sahihi kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

Ulimwengu wa Roho

  • Wakati miili yetu inapokufa, roho zetu huendelea kuishi katika ulimwengu wa roho. Hii ni hali ya muda ya kujifunza na kujiandaa kabla ya Ufufuo.

  • Injili ya Yesu Kristo inafundishwa katika ulimwengu wa roho, na tunaweza kuendelea kukua na kusonga mbele.

Ufufuo, Wokovu na Kuinuliwa

  • Baada ya muda wetu katika ulimwengu wa roho, Ufufuo ndiyo hatua inayofuata katika safari yetu ya milele.

  • Ufufuo ni kuunganika tena kwa roho zetu na mwili wetu. Kila mmoja wetu atafufuliwa na kuwa na mwili uliokamilika. Tutaishi milele. Hii inafanywa iwezekane kwa Upatanisho na Ufufuko wa Mwokozi.

Hukumu na Falme za Utukufu

  • Tutakapofufuka, Yesu Kristo atakuwa mwamuzi wetu. Pamoja na mambo ya kipekee machache sana, watoto wote wa Mungu watapokea nafasi katika ufalme wa utukufu.

  • Ingawa sisi sote tutafufuka, sisi sote hatutapokea utukufu sawa wa milele. Yesu atatuhukumu kulingana na imani yetu, kazi, na toba katika maisha ya duniani na katika ulimwengu wa roho. Tunaweza kurudi kuishi katika uwepo wa Mungu kama tu waaminifu.

Maswali ambayo Ungeweza Kuwauliza Watu

Maswali yafuatayo ni mifano ya kile ambacho ungeweza kuwauliza watu. Maswali haya yanaweza kukusaidia uwe na mazungumzo ya maana na uelewe mahitaji ya mtu na mtazamo wake.

  • Je! Wewe unadhani dhumuni la maisha ni lipi?

  • Je, ni kitu gani kinakuletea furaha?

  • Je, ni changamoto zipi unazohitaji Mungu akusaidie kwenye hizo?

  • Je, umejifunza nini kutokana na changamoto ulizokabiliana nazo?

  • Je, unajua nini kuhusu Yesu Kristo? Je, ni kwa jinsi gani maisha na misheni Yake vimeathiri maisha yako?

Mialiko ambayo Ungeweza Kutoa

  • Je, utamwomba Mungu katika sala ili akusaidie ujue kwamba kile tulichofundisha ni cha kweli? (Ona “Umaizi wa Kufundisha: Sala” katika sehemu ya mwisho ya somo la 1.)

  • Je, utahudhuria kanisani pamoja nasi Jumapili hii ili ujifunze zaidi kuhusu kile tulichofundisha?

  • Je, utasoma Kitabu cha Mormoni na kusali ili kujua kwamba ni neno la Mungu? (Unaweza kupendekeza sura au mistari.)

  • Je, utafuata mfano wa Yesu na kubatizwa? (Ona “Mwaliko wa Kubatizwa na Kuthibitishwa,” ambao unakuja mara tu baada ya somo la 1.)

  • Je, tunaweza kupanga matembezi yetu yajayo?

mchoro wa mpango wa wokovu

Msingi wa Mafundisho

Sehemu hii inatoa mafundisho na maandiko kwa ajili ya kujifunza ili kuimarisha ufahamu na ushuhuda wako juu ya injili na kukusaidia ufundishe.

Makundi ya nyota

Maisha kabla ya Kuzaliwa Duniani: Dhumuni na Mpango wa Mungu kwa ajili Yetu Sisi.

Sisi ni Watoto wa Mungu, na Tuliishi Pamoja na Yeye kabla ya Kuzaliwa Kwetu duniani

Mungu ni Baba wa roho zetu. Sisi ni watoto halisi wa Mungu, tuliumbwa kwa mfano Wake. Kila mmoja wetu anayo asili takatifu kama mtoto wa Mungu. Ufahamu huu unaweza kutusaidia tupite nyakati ngumu na unaweza kutupatia msukumo wa kuwa bora kadiri tuwezavyo.

Tuliishi pamoja na Mungu kama watoto Wake wa kiroho kabla hatujazaliwa duniani. Sisi ni washiriki wa familia Yake.

Rais M. Russell Ballard

“Kuna utambulisho mmoja muhimu tunaoshiriki sasa na milele, utambulisho ambao kamwe hatutaupoteza, na utambulisho ambao tunapaswa kuwa na shukrani juu Yake. Hiyo ni kwamba wewe ni, na siku zote umekuwa mwana au binti wa Mungu ukiwa na mizizi ya kiroho katika milele yote.

“… Kuelewa ukweli huu—hasa kuuelewa na kuukumbatia—kunabadilisha maisha. Kunakupa utambulisho wa kupendeza ambao hakuna mtu anayeweza kuuchukua kutoka kwako. Lakini zaidi ya hayo, unapaswa kukupa hisia nyingi sana za thamani na maana ya thamani yako isiyo na mwisho. Hatimaye, unakupa dhumuni la kiungu, tukufu, na la thamani katika maisha” (“Children of Heavenly Father” [Brigham Young University devotional, Sept. 3, 2020], 2, speeches.byu.edu).

Tulichagua Kuja Duniani

Baba yetu wa Mbinguni anatupenda na anatamani kwamba sisi tuwe kama Yeye. Yeye ni kiumbe kilichoinuliwa kilicho na mwili mtukufu.

Katika maisha yetu kabla ya kuzaliwa, tulijifunza kwamba Mungu ana mpango kwa ajili yetu ili tuwe kama Yeye. Sehemu moja ya mpango Wake ilikuwa kwamba tungeondoka kutoka nyumbani kwetu mbinguni na kuja duniani ili kupokea miili. Pia tulihitajika kupata uzoefu na kukuza imani wakati tukiwa mbali na uwepo wa Mungu. Tusingeweza kukumbuka tulivyoishi na Mungu. Hata hivyo, Yeye angetoa kile tulichohitaji ili tuweze kurudi kuishi pamoja na Yeye.

Haki ya kujiamulia, au uhuru na uwezo wa kuchagua, ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu kwa ajili yetu. Katika maisha yetu kabla ya kuzaliwa duniani, kila mmoja wetu alichagua kufuata mpango wa Mungu na kuja duniani ili tuweze kupiga hatua inayofuata katika maendeleo yetu ya milele. Tulielewa kwamba wakati tuko hapa, tungeweza kuwa na fursa nyingi mpya za kukua na kuhisi furaha. Tulielewa pia kwamba tungekabiliwa na upinzani. Tungepata uzoefu wa majaribu, mateso, huzuni, na kifo.

Katika kuchagua kuja duniani, tulitumainia upendo na msaada wa Mungu. Tulitumainia mpango Wake kwa ajili ya wokovu wetu.

Baba wa Mbinguni Alimchagua Yesu Kristo ili Atukomboe

Yesu Kristo ni kiini cha mpango wa Mungu. Kabla ya kuja duniani, tulijua kwamba hatungeweza kurudi kwenye uwepo wa Mungu sisi wenyewe. Baba wa Mbinguni alimchagua Yesu Kristo, Mwanaye Mzaliwa kwanza, ili afanye iwezekane kwetu kurudi Kwake na kuwa na uzima wa milele.

Yesu alikubali kwa hiari yake. Yeye alikubali kuja duniani na kutukomboa kupitia dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Upatanisho na Ufufuko Wake ungewezesha madhumuni ya Mungu kwa ajili yetu kutimia.

Kujifunza Maandiko

Watoto wa Mungu

Dhumuni la Mungu

Maisha Kabla ya Kuzaliwa Duniani

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

machweo baharini

Uumbaji

Mpango wa Baba wa Mbinguni uliwezesha uumbaji wa dunia, mahali ambapo watoto Wake wa Kiroho wangepokea miili na kupata uzoefu. Maisha yetu duniani ni muhimu kwa ajili yetu ili tuendelee na tuwe kama Mungu.

Chini ya maelekezo ya Baba wa Mbinguni, Yesu Kristo aliumba dunia na vitu vyote vyenye uhai. Baba wa Mbinguni kisha alimuumba mwanamume na mwanamke kwa mfano Wake. Uumbaji ni dhihirisho la upendo wa Mungu na hamu Yake kwa ajili yetu ili tuwe na fursa ya kukua.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko, “Umba, Uumbaji

  • Mada za Injili: “Uumbaji

Kuondoka katika Bustani ya Edeni, na Joseph Brickey

Anguko la Adamu na Hawa

Kabla ya Kuanguka

Adamu na Hawa walikuwa wa kwanza kati ya watoto wa kiroho wa Baba wa Mbinguni kuja duniani. Mungu aliumba miili yao katika mfano Wake na kuwaweka katika Bustani ya Edeni. Katika bustani walikuwa wasio na hatia, na Mungu alikidhi mahitaji yao.

Wakati Adamu na Hawa wakiwa katika bustani, Mungu aliwaamuru wasile tunda la mti wa ujuzi wa mema na maovu. Kama wangetii amri hii, wangeweza kubaki katika bustani. Hata hivyo, wasingeweza kuendelea kwa kujifunza kutokana na upinzani na changamoto za duniani. Hawangeweza kujua shangwe kwa sababu hawangeweza kupitia huzuni na uchungu.

Shetani aliwajaribu Adamu na Hawa wale tunda lililokatazwa, na walichagua kufanya hivyo. Kwa sababu ya uchaguzi huu, walitupwa nje ya bustani na wakatengwa mbali na uwepo wa Mungu. Tukio hili linajulikana kama Anguko.

Baada ya Anguko

Baada ya Anguko, Adamu na Hawa wakawa wenye kuweza kufa. Hawakuwa tena katika hali ya kutotenda dhambi, walielewa na kupata uzoefu wa mema na uovu. Wangeweza kutumia haki ya kujiamulia kuchagua kati ya hayo mawili. Kwa sababu Adamu na Hawa walikabiliwa na upinzani na changamoto, waliweza kujifunza na kuendelea mbele. Kwa sababu ya kupata huzuni, wangeweza pia kupata shangwe. (Ona 2 Nefi 2:22–25.)

Licha ya magumu yao, Adamu na Hawa walihisi kwamba kuwa na mwili wenye uwezekano wa kufa ilikuwa baraka kubwa. Baraka mojawapo ilikuwa ni kwamba wangeweza kupata watoto. Hii ilitoa njia ya watoto wengine wa kiroho wa Mungu kuja duniani na kupokea miili.

Kuhusu baraka za Anguko, wote Adamu na Hawa walifurahia. Hawa alisema, “Kama isingekuwa kwa uvunjifu wetu wa sheria kamwe tusingekuwa na [watoto], na kamwe tusingelijua mema na maovu, na shangwe ya ukombozi wetu, na uzima wa milele ambao Mungu huutoa kwa wote walio watiifu” (Musa 5:11; ona poa mstari wa 10).

Kujifunza Maandiko

Katika Bustani

Anguko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Maisha yetu Duniani

Watu wengi hujiuliza, “Kwa nini niko hapa duniani?” Maisha yetu duniani ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu kwa ajili ya maendeleo yetu ya milele. Dhumuni letu la msingi ni kujiandaa kurudi katika uwepo wa Mungu na kupokea utimilifu wa shangwe. Muhtasari hapa chini ni baadhi ya njia ambazo maisha ya duniani hutuandaa kwa ajili ya dhumuni hili.

mvulana akitabasamu

Kupokea Mwili

Dhumuni la kuja duniani ni kupokea mwili ambao roho zetu zinaweza kukaa ndani yake. Miili yetu ni mitakatifu, uumbaji wa kimiujiza wa Mungu. Kwa miili yetu, tunaweza kutenda, kujifunza, na kupata uzoefu wa mambo mengi ambayo roho zetu hazingeweza bila mwili. Tunaweza kuendelea katika njia nyingi ambazo hatungeweza kama roho.

Kwa sababu miili yetu ni yenye kufa, tunapata uchungu, maradhi, na majaribu mengine. Uzoefu huu unaweza kutusaidia tujifunze subira, huruma, na sifa zingine za kiungu. Unaweza kuwa sehemu ya mapito yetu ya shangwe. Kuchagua kilicho sahihi wakati ni vigumu kufanya hivyo mara nyingi ndivyo jinsi imani, tumaini, na hisani vinavyokuwa sehemu ya hulka yetu.

Kujifunza Kutumia Haki ya Kujiamulia kwa Hekima

Dhumuni lingine la maisha ya duniani ni kujifunza kutumia haki ya kujiamulia kwa hekima—kuchagua kile kilicho sahihi. Kujifunza kutumia haki yetu ya kujiamulia kwa hekima ni muhimu katika kuwa kama Mungu.

Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanatufundisha kile kilicho sahihi na kutupatia amri za kutuongoza kwenye furaha. Shetani hutujaribu tufanye makosa, akitutaka tuwe wenye huzuni kama yeye. Tunakabiliana na upinzani kati ya wema na uovu, ambao ni muhimu katika kujifunza kutumia haki yetu ya kujiamulia (ona 2 Nefi 2:11).

Tunapomtii Mungu, tunakua na kupokea baraka ambazo Yeye aliahidi. Tunapokosa kutii, tunajitenga wenyewe mbali na Yeye na kupokea matokeo ya dhambi. Ingawaje mara nyingine inaonekana vinginevyo, dhambi hatimaye hutuelekeza kwenye huzuni. Mara nyingi baraka za utiifu—na athari za dhambi—hazionekani wazi mara moja au hazionekani kwa nje. Lakini ni hakika, kwani Mungu ni mwenye haki.

Hata wakati tunapofanya vyema tuwezavyo, sote tunatenda dhambi na “kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23). Kwa kujua hili, Baba wa Mbinguni alitoa njia kwa ajili yetu ya kutubu ili tuweze kurudi Kwake.

Toba huleta nguvu za Mkombozi wetu, Yesu Kristo, katika maisha yetu (ona Helamani 5:11). Tunapotubu, tunatakaswa kutokana na dhambi kupitia dhabihu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi, na kipawa cha Roho Mtakatifu (ona 3 Nefi 27:16–20). Kupitia toba, tunapata shangwe. Njia ya kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni imefunguliwa kwetu, kwani Yeye ni mwenye huruma. (Ona “Toba” katika somo la 3.)

Kujifunza Kutembea kwa Imani

Dhumuni lingine la maisha haya ni kupata uzoefu ambao unaweza kuja tu kupitia kutenganishwa na Baba wa Mbinguni. Kwa sababu hatumuoni Yeye, tunahitaji kujifunza kutembea kwa imani (ona 2 Wakorintho 5:6–7).

Mungu hajatuacha sisi peke yetu katika hii safari. Yeye amemtoa Roho Mtakatifu ili atuongoze, atuimarishe, na atutakase. Yeye pia ametoa maandiko, manabii, sala, na injili ya Yesu Kristo.

Kila sehemu ya uzoefu wetu wa duniani—shangwe na huzuni, mafanikio na vikwazo—vinaweza kutusaidia tukue wakati tunapojiandaa kurudi kwa Mungu.

Kujifunza Maandiko

Muda wa Kukua na Kuendelea

Uchaguzi

Mema na Maovu

Dhambi

Lazima Tuwe Wasafi ili Kuwa pamoja na Mungu

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Upatanisho wa Yesu Kristo

Kwa sababu ya Anguko la Adamu na Hawa, sisi sote tuko chini ya dhambi na kifo. Hatuwezi kushinda matokeo ya dhambi na kifo sisi wenyewe. Katika mpango wa wokovu wa Baba wa Mbinguni, Yeye alitoa njia ya kushinda athari za Anguko ili tuweze kurudi Kwake. Kabla ya ulimwengu kuumbwa, Yeye alimchagua Yesu Kristo kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu.

Yesu Kristo pekee ndiye angeweza kutukomboa kutokana na dhambi na mauti. Yeye ni Mwana halisi wa Mungu. Yeye aliishi maisha yasiyo na dhambi, mtiifu kikamilifu kwa Baba Yake. Yeye alikuwa amejitayarisha na alikuwa radhi kutenda mapenzi ya Baba Yake.

Upatanisho wa Mwokozi ulijumuisha kuteseka Kwake katika Gethsemane na kuteseka Kwake na kifo kwenye msalaba, na Ufufuko Wake. Yeye aliteseka zaidi ya vile tunavyoweza kudhani—zaidi sana kiasi kwamba alitokwa damu katika kila kinyweleo (ona Mafundisho na Maagano 19:18).

Upatanisho wa Yesu Kristo ndiyo tukio tukufu zaidi katika historia ya binadamu. Kupitia dhabihu Yake ya kulipia dhambi, Yesu alifanya mpango wa Baba ufanye kazi. Tungekuwa bila msaada bila kuwepo kwa Upatanisho wa Yesu Kristo kwa sababu hatungeweza kujiokoa wenyewe kutokana na dhambi na kifo (ona Alma 22:12–15).

Dhabihu ya Mwokozi wetu ilikuwa dhihirisho kuu la upendo kwa ajili ya Baba Yake na kwa ajili yetu. “Upana, na urefu, na kimo, na kina” cha upendo wa Kristo kinashinda uelewa wetu (Waefeso 3:18; ona pia mstari wa 19).

Kusulubishwa, na Harry Anderson

Yesu Kristo Alishinda Kifo kwa ajili ya Wote

Wakati Yesu Kristo alipokufa msalabani, roho Yake ilitenganishwa kutoka kwenye mwili Wake. Katika siku ya tatu, roho Yake na mwili Wake viliunganika, kamwe visitengane tena. Yeye aliwatokea watu wengi, kuwaonesha kwamba alikuwa na mwili usiokufa wa nyama na mifupa. Kuungana huku tena kwa mwili na roho kunaitwa Ufufuko.

Kama watu wanaoweza kufa, kila mmoja wetu atakufa. Hata hivyo, kwa sababu Yesu alishinda kifo, kila mtu anayezaliwa duniani atafufuka. Ufufuo ni kipawa cha uungu kwa ajili ya wote, kilichotolewa kupitia rehema na neema ya Mwokozi. Roho na mwili wa kila mtu vitaunganika tena, na kila mmoja wetu ataishi milele katika mwili mkamilifu, uliofufuka. Kama siyo Yesu Kristo, kifo kingemaliza matumaini yote ya kuwa pamoja na Baba wa Mbinguni (ona 2 Nefi 9:8–12).

Yesu Anafanya Iwezekane kwa ajili Yetu Kutakaswa Dhambi Zetu

Ili kuelewa tumaini tunaloweza kupokea kupitia Kristo, tunahitaji kuelewa sheria ya haki. Hii ni sheria isiyobadilika ambayo huleta matokeo kwa ajili ya matendo yetu. Utiifu kwa Mungu huleta matokeo chanya, na kutotii huleta matokeo hasi. (Ona Alma 42:14–18.) Tunapotenda dhambi, tunakuwa wachafu kiroho, na hakuna kitu kichafu kinachoweza kuishi katika uwepo wa Mungu (ona 3 Nefi 27:19).

Kristo Akisali Gethsemane, na Harry Anderson

Wakati wa dhabihu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi, Yeye alisimama katika nafasi yetu, aliteseka, na kulipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu (ona 3 Nefi 27:16–20). Mpango wa Mungu unampa Yesu Kristo nguvu za kufanya maombezi kwa niaba yetu—kusimama kati yetu na haki (ona Mosia 15:9). Kwa sababu ya dhabihu ya Yesu ya kulipia dhambi, Yeye anaweza kudai haki Zake za rehema kwa niaba yetu kadiri tunavyofanyia kazi imani iongozayo kwenye toba (ona Moroni 7:27; Mafundisho na Maagano 45:3–5). “Basi rehema inaridhisha mahitaji ya haki, na kuwazingira kwa mikono ya usalama” (Alma 34:16).

Ni kupitia tu zawadi ya Upatanisho wa Mwokozi na toba yetu kwamba tunaweza kurudi ili kuishi na Mungu. Tunapotubu, tunasamehewa na kusafishwa kiroho. Tunaondolewa mzigo wa hatia kwa ajili ya dhambi zetu. Nafsi zetu zilizojeruhiwa zinaponywa. Tunajawa na shangwe (ona Alma 36:24).

Ingawa sisi si wakamilifu na tunaweza kupungukiwa tena, kuna neema zaidi, upendo, na rehema zaidi katika Yesu Kristo kuliko uwepo wa kushindwa, dosari, au dhambi, ndani yetu. Mungu daima yu tayari na ana hamu ya kutukumbatia pale tunapomgeukia Yeye na kutubu (ona Luka 15:11–32). Hakuna kitu na hakuna yeyote “atakayeweza kututenga na upendo wa Mungu, ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Warumi 8:39).

Yesu Kristo Alijichukulia juu Yake Uchungu Wetu, Mateso na Udhaifu Wetu.

Katika dhabihu Yake ya kulipia dhambi, Yesu Kristo alijichukulia juu Yake uchungu wetu, mateso na udhaifu wetu. Kwa sababu hii, Yeye anajua “kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao” (Alma 7:12; ona pia mstari wa 11). Yeye anatualika “Njooni kwangu,” na tunapofanya hivyo, Yeye anatupa pumziko, tumaini, nguvu, mtazamo, na uponyaji (Mathayo 11:28; ona pia mstari wa 29–30).

Tunapomtegemea Yesu Kristo na Upatanisho Wake, Yeye anaweza kutusaidia tuvumilie majaribu yetu, magonjwa, na uchungu wetu. Tunaweza kujazwa kwa shangwe, amani, na faraja. Yale yasiyo haki kuhusu maisha yanaweza kufanywa kuwa sahihi kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

Kujifunza Maandiko

Upatanisho wa Mwokozi

Ufufuo

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

familia ikitembelea kaburi

Ulimwengu wa Roho

Watu wengi wanajiuliza, “Ni nini hutokea baada ya mimi kufa? Mpango wa wokovu unatoa baadhi ya majibu muhimu kwa swali hili.

Kifo ni sehemu ya “mpango wa rehema” wa Mungu kwa ajili yetu (2 Nefi 9:6). Badala ya kuwa mwisho wa kuwepo kwetu, kifo ni hatua inayofuata katika maendeleo yetu ya milele. Kuwa kama Mungu, lazima tupitie kifo na baadaye tupokee miili iliyo kamili, iliyofufuka.

Wakati miili yetu inapokufa, roho zetu huendelea kuishi katika ulimwengu wa roho. Hii ni hali ya muda ya kujifunza na kujiandaa kabla ya Ufufuo na Hukumu ya Mwisho. Ufahamu wetu kutoka kwenye maisha ya duniani hubakia pamoja nasi.

Katika ulimwengu wa roho, watu waliopokea na kuishi Injili ya Yesu Kristo “wanapokelewa katika hali ya furaha, ambayo inaitwa paradiso” (Alma 40:12). Watoto wadogo pia wanapokelewa katika paradiso pale wanapokufa.

Roho katika paradiso zitakuwa na amani kutokana na shida zao na huzuni. Wataendelea na ukuaji wa kiroho, wakifanya kazi ya Mungu na kuwatumikia wengine. Watafundisha injili kwa wale ambao hawakuipokea wakati wa maisha yao ya duniani (ona Mafundisho na Maagano 138: 32–37, 57–59)).

Katika ulimwengu wa roho, watu ambao hawakuweza kuipokea injili duniani, au wale waliochagua kutofuata amri, watapata ukomo fulani (ona Mafundisho na Maagano 138:6–37; Alma 40:6–14). Hata hivyo, kwa sababu Mungu ni mwenye haki na rehema, watapata nafasi ya kufundishwa injili ya Yesu Kristo. Kama wakiipokea na kutubu, watakombolewa kutokana na dhambi zao (ona Mafundisho na Maagano 138:58; ona pia 138:31–35; 128:22). Watakaribishwa katika amani ya paradiso. Hatimaye watapokea sehemu katika ufalme wa utukufu kulingana na chaguzi walizozifanya duniani na katika ulimwengu wa roho.

Tunabakia katika ulimwengu wa roho hadi tutakapofufuka.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Ufufuo, Wokovu na Kuinuliwa

Ufufuo

Mpango wa Mungu hufanya iwezekane kwetu kukua na kupokea uzima wa milele. Baada ya muda wetu katika ulimwengu wa roho, Ufufuo ndiyo hatua inayofuata katika ukuaji huo.

Ufufuo ni kuunganika tena kwa roho zetu na miili yetu. Kila mmoja wetu atafufuka. Hii inafanywa iwezekane kwa Upatanisho na Ufufuko wa Mwokozi. (Ona Alma 11:42–44.)

Sisi sote tutakapofufuka, kila mmoja wetu atakuwa na mwili mkamilifu, huru kutokana na uchungu na magonjwa. Tutakuwa wasiokufa, tukiishi milele.

Wokovu

Kwa sababu sisi sote tutafufuka, sisi sote tutaokolewa—au tutapata wokovu—kutokana na kifo cha kimwili. Kipawa hiki kinatolewa kwetu kupitia neema ya Yesu Kristo.

Sisi pia tunaweza kuokolewa—au kupata wokovu—kutokana na matokeo ambayo sheria ya haki inadai kwa ajili ya dhambi zetu. Zawadi hii pia inawezeshwa kupitia fadhili na rehema ya Yesu Kristo pale tunapotubu. (Ona Alma 42:13–15, 21–25.)

Kuinuliwa

Kuinuliwa, au uzima wa milele, ni hali ya juu sana ya furaha na utukufu katika ufalme wa selestia. Kuinuliwa ni zawadi yenye masharti. Rais Russell M. Nelson alifundisha, “Hayo masharti ya kufuzu yanajumuisha imani katika Bwana, toba, ubatizo, kupokea Roho Mtakatifu, na kubakia mwaminifu kwenye ibada na maagano ya hekaluni” (“Wokovu na Kuinuliwa,” Liahona, Mei 2008, 9).

Kuinuliwa humaanisha kuishi na Mungu milele katika familia za milele. Ni kumjua Mungu na Yesu Kristo na kuwa kama Wao, na kupata uzoefu wa maisha yale ambayo Wao wanayafurahia.

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

  • Mwongozo wa Maandiko: “Ufufuo

  • Mada za Injili: “Ufufuo,” “Wokovu

miale ya jua ikiangaza mawinguni

Hukumu na Falme za Utukufu

Zingatia: Unapofundisha kuhusu falme za utukufu kwa mara ya kwanza, fundisha katika kiwango cha msingi kulingana na mahitaji na uelewa wa mtu.

Tutakapofufuka, Yesu Kristo atakuwa mwamuzi wetu mwenye haki na rehema. Isipokuwa wachache tu, kila mmoja wetu atapokea nafasi katika ufalme wa utukufu. Ingawa sisi sote tutafufuka, siyo wote watakaopokea utukufu wa milele ulio sawa (ona Mafundisho na Maagano 88:22–24, 29–34; 130:20–21; 132:5).

Watu ambao hawakupata nafasi ya kuelewa kikamilifu na kuzitii sheria za Mungu wakati wa maisha yao duniani watapewa nafasi hiyo katika ulimwengu wa roho. Yesu atamhukumu kila mmoja kulingana na imani yake, kazi, matamanio, na toba yake hapa duniani na katika ulimwengu wa roho (ona Mafundisho na Maagano 138:32–34, 57–59.

Maandiko yanafundisha juu ya falme za utukufu za selestia, terestria, na telestia. Kila mojawapo ni dhihirisho la upendo wa Mungu, haki, na rehema.

Wale wanaoonesha imani katika Kristo, kutubu dhambi zao, kupokea ibada za injili, kushika maagano yao, kupokea Roho Mtakatifu, na kuvumilia hadi mwisho wataokolewa katika ufalme wa selestia. Ufalme huu pia utajumuisha watu ambao hawakupata nafasi ya kupokea injili wakati wa maisha yao duniani lakini “wangeipokea kwa mioyo yao yote” na walifanya hivyo katika ulimwengu wa roho (Mafundisho na Maagano 137:8; ona pia mstari wa 7). Watoto waliofariki kabla ya kufikia umri wa kuwajibika (miaka minane) pia wataokolewa katika ufame wa selestia (ona Mafundisho na Maagano 137:10).

Katika maandiko, ufalme wa selestia unalinganishwa na utukufu au uangavu wa jua. (Ona Mafundisho na Maagano 76:50, 70).

Watu walioishi maisha ya heshima “ambao hawakupokea ushuhuda wa Yesu katika mwili, lakini baadaye waliupokea” watapokea sehemu katika ufalme wa terestria (Mafundisho na Maagano 76:74). Hiyo pia ni kweli kwa wale ambao hawakuwa hodari katika ushuhuda wao juu ya Yesu. Ufalme huu unalinganishwa na utukufu wa mwezi. (Ona Mafundisho na Maagano 76:71–80.)

Wale ambao waliendelea katika dhambi zao na hawakutubu katika maisha haya au kupokea injili ya Yesu Kristo katika ulimwengu wa roho watapokea zawadi yao katika ufalme wa telestia. Ufalme huu unalinganishwa na utukufu wa nyota. (Ona Mafundisho na Maagano 76:81–86.)

Kujifunza Maandiko

Jifunze Zaidi kuhusu Kanuni Hii

Muhtasari Mfupi hadi wa Wastani wa Somo

Muhtasari ufuatao ni sampuli ya kile ambacho ungemfundisha mtu fulani kama una muda mfupi. Unapotumia muhtasari huu, chagua kanuni moja au zaidi za kufundisha. Msingi wa mafundisho kwa kila kanuni ulitolewa mapema katika somo hili.

Unapofundisha, uliza maswali na usikilize. Toa mwaliko ambao utawasaidia watu wajifunze jinsi ya kusonga karibu na Mungu. Mwaliko mmoja muhimu ni kwa ajili mtu kukutana nanyi tena. Urefu wa somo utategemea maswali unayouliza na usikilizaji unaoufanya.

Kile unachoweza Kuwafundisha Watu kwa Dakika 3–10

  • Sisi sote tu watoto wa kiroho wa Mungu. Sisi ni washiriki wa familia Yake. Yeye anamjua na kumpenda kila mmoja wetu.

  • Mungu ametoa mpango kwa ajili ya furaha yetu na maendeleo yetu katika maisha haya na ya milele.

  • Katika mpango wa Mungu, tulihitajika kuja duniani ili tuweze kupokea miili, kujifunza na kukua.

  • Yesu Kristo ni kiini cha mpango wa Mungu. Yeye hutuwezesha tuwe na uzima wa milele.

  • Chini ya maelekezo ya Mungu, Yesu aliumba dunia.

  • Uzoefu wetu hapa duniani ulidhamiriwa utusaidie tujiandae kurudi kwenye uwepo wa Mungu.

  • Kila mmoja wetu hutenda dhambi, na kila mmoja wetu atakufa. Kwa sababu Mungu anatupenda, Yeye alimtuma Mwanaye, Yesu Kristo, kuja duniani kutukomboa kutokana na dhambi na kifo.

  • Yale yasiyo haki kuhusu maisha yanaweza kufanywa sahihi kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.

  • Wakati mwili wetu unapokufa, roho yetu inaendelea kuishi. Hatimaye sisi sote tutafufuliwa. Hii inamaanisha kwamba roho na mwili wa kila mtu vitaunganika tena, na kila mmoja wetu ataishi milele katika mwili mkamilifu, uliofufuka.

  • Tutakapofufuka, Yesu Kristo atakuwa mwamuzi wetu. Pamoja na mambo ya kipekee machache sana, watoto wote wa Mungu watapokea nafasi katika ufalme wa utukufu. Tunaweza kurudi kuishi katika uwepo wa Mungu kama tu waaminifu.