Waanzilishi katika Kila Nchi
Vicky Tadić
Mwongofu wa Mwanzoni nchini Boznia na Herzegovina
“Huyo alikuwa Roho Mtakatifu?” Vicky aliuliza.
“Njoo!” Kaka yake Vicky aliita. “Hebu twende tucheze na akina Rowe!”
Wakina Rowe walikuwa majirani wao wapya. Walikuwa wamehamia Boznia na Herzegovina kutoka Marekani. Walikuwa na watoto waliokuwa na umri sawa na Vicky na ndugu zake. Lakini hawakuwa wakizungumza Kiboznia. Vicky pekee ndiye alifahamu kuzungumza Kingereza katika familia yake. Alitafsiri ili waweze kucheza pamoja.
Vicky na Bi. Rowe waliketi kwenye veranda huku watoto wengine wakicheza.
“Familia yako inaonekana tofauti,” alisema Vicky. “Katika njia nzuri.”
Bi. Rowe alitabasamu. “Ungependa kuja kanisani pamoja na sisi? Huenda itakusaidia uelewe kwa nini sisi tuko tofauti. Kanisa letu halina jengo hapa Boznia, hivyo huwa tunakuwa na kanisa la familia yetu nyumbani.”
Vicky alikuwa na shauku alipowasili nyumbani kwa wakina Rowe siku ya Jumapili. Kwanza waliimba wimbo. Mmoja wa watoto akatoa sala. Kisha Bwana Rowe akaomba na akapitisha mkate na maji kwa kila mtu. Walisema kuwa inaitwa sakramenti. Baada ya hilo binti yao Jessie alizungumza.
“Baba wa Mbinguni anatupenda. Huzungumza nasi kupitia Roho Mtakatifu,” alisema Jessie. “Wakati mwingine Roho Mtakatifu hutupa hisia za amani. Au wakati mwingine hutupa wazo.”
Siku iliyofuata, Vicky alikwenda dukani kununua mkate. Alipokuwa akirudi nyumbani, alikuwa amekaribia kuyapita mapipa ya uchafu wakati sauti mawazoni mwake ilipomsimamisha. Kaambali, ilisema.
Vicky alisimama tuli. Ghafla, gari likaja likibiringika kwenye kona. PUUU! Likajibamiza kwenye mapipa hayo ya taka.
Vicky alivuta pumzi kwa nguvu. Alifurahi sana kuwa aliisikiliza ile sauti!
Baadaye, Vicky alimsimulia Bi Rowe yaliyotokea. “Huyo alikuwa Roho Mtakatifu?”
“Inasikika kama hivyo. Wakati mwingine Roho Mtakatifu hutuonya juu ya hatari.”
“God alinilinda,” alisema Vicky. “Daima nitamsikiliza Roho Mtakatifu.”
Vicky aliendelea kwenda kwa wakina Rowe kila Jumapili. Kisha Vicky alishiriki na mamake Kitabu cha Mormoni. Punde, familia yao yote ilikuwa ikijifunza injili kutoka kwa wakina Rowe. Vicky alitafsiri kwa ajili ya kila mtu.
Siku moja Bwana Rowe aliuliza familia ya Vicky swali. Vicky alilirudia swali hilo katika Kiboznia. “Je, mtafuata mfano wa Yesu Kristo kwa kubatizwa?”
Vicky alisubiri. Yeye alitaka kubatizwa. Lakini alikuwa na wasiwasi kuhusu familia yake ingesemaje.
Hatimaye, baba yake Vicky alizungumza. “Da.”
“Da,” familia yake ilisema.
Vicky alifurahi sana, alihisi kama moyo wake ungekuja kupasuka. “Ndiyo,” alimwambia Bwana Rowe. “Ndiyo, tutabatizwa.”
Wiki moja baadaye, Vicky pamoja na familia yake walisafiri kwa saa tano kuelekea kwenye jengo la Kanisa lililokuwa karibu zaidi. Vicky alikuwa mwenye furaha alipoingia majini ili kubatizwa. Alijisikia furahia zaidi wakati alipothibitishwa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Sasa Roho Mtakatifu atakuwa pamoja naye daima.