Waanzilishi katika Kila Nchi
Utafutaji wa Muda Mrefu wa Michael
Michael alijuiliza ni kanisa lipi lilikuwa la kweli.
Michael alitundika mkoba wake begani. Ilikuwa ni siku ya kwanza shuleni, na asingeweza kusubiri! Yeye na familia yake waliishi India. Watoto wengi katika mji wake hawakwenda shule. Michael alikuwa na shukrani alipata nafasi ya kujifunza.
Alipenda kujifunza—hasa hisabati. Pia alipenda kusoma magazeti. Alipekua kurasa zenye rangi. Alisoma kuhusu wanyama na sehemu tofauti kote ulimwenguni.
Siku moja Michael alisoma aina nyingine ya gazeti. Lilikuwa kutoka Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Michael alipenda kulisoma. Alitaka kujifunza zaidi.
Michael alikuwa ameenda katika makanisa mengine hapo awali. Alipenda kujifunza kuhusu Yesu. Lakini wakati mwingine alihisi kukanganyikiwa. Ni kanisa lipi lilikuwa la kweli.
Baadaye, alisoma kijitabu kuhusu nabii Joseph Smith. Alihisi kitu maalum alipokuwa akikisoma. Joseph Smith pia alikuwa ameenda katika makanisa tofauti tofauti kutafuta ukweli. Labda Mimi ni kama Joseph, Michael aliwaza.
Michael alitaka kwenda katika kanisa hili jipya kuona vile lilivyokuwa. Lakini hakukuwa na makanisa ya Watakatifu wa Siku za Mwisho nchini India. Michael alivunjika moyo. Aliendelea kujifunza yote aliyoweza. Alisoma Kitabu cha Mormoni na kusali. Alijua kwamba kilikuwa cha kweli! Alitaka kubatizwa. Lakini ingembidi kusubiri.
Miaka ilipita. Wakati Michael alipokuwa na umri wa miaka 21, wamisionari wanandoa walikuja India. Hatimaye, Michael alibatizwa! Punde aliweza kutumikia misheni yake katika Utah, Marekani.
Miaka zaidi ilipita. Siku moja rafiki alimpigia simu. Kanisa lilikuwa linatafuta watu wa kusaidia kutafsiri mkutano mkuu kwa ajili ya watu wa India. Michael alikuwa na woga mwanzoni. Lakini alikuwa na furaha kusaidia.
Alasiri moja ya Oktoba Michael alikuwa akitafsiri hotuba ya Rais Nelson kwenye mkutano mkuu. Alimsikia nabii akitangaza kwamba hekalu litajengwa nchini India! Michael alitaka kupiga kelele za furaha. Alilia machozi ya furaha.
Michael alikuwa na shukrani kwa yale yote aliyojifunza shuleni. Lakini zaidi ya yote, alikuwa na shukrani kwamba alikuwa amejifunza kuhusu Injili ya Yesu Kristo. Alikuwa na furaha kwamba watu wengi katika nchi yake wangeweza kujifunza kumhusu Yeye pia!