“Njia 4 za Kuimarisha Familia Yako,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Okt 2023.
Njia 4 za Kuimarisha Familia Yako
Unaweza kuimarisha familia yako kuwa bora zaidi kwa kuishi injili ya Yesu Kristo.
Bila kujali familia yako ni imara kiasi gani, inaweza kutumia nguvu kidogo ya ziada kila wakati. Siku hizi, inaonekana kama mapigo kwa familia yanaendelea tu kuja. Hii ni kwa sababu Shetani anajua kwamba familia ni muhimu kwenye mpango wa Baba wa Mbinguni. Ikiwa kuna kitu chochote ambacho adui anaweza kufanya ili kuvuruga maisha ya familia, hakika atakijaribu.
Ingawa hakuna familia iliyo kamilifu, yako ina jambo moja ambalo hakuna familia nyingine inalo: wewe! Na wewe unayo injili ya Yesu Kristo upande wako. Manabii na mitume wamefundisha, “Furaha katika maisha ya familia ina uwezekano mkubwa wa kupatikana inapojengwa juu ya mafundisho ya Bwana Yesu Kristo.”1
Hapa kuna baadhi ya njia injili ya Bwana inaweza kuimarisha na kuleta furaha kwenye familia yako:
-
Familia zinaweza kuunganishwa kwa milele yote.
-
Familia zinaweza kufurahia kutumia wakati pamoja, kutoa huduma kwa kila mmoja na mwingine, na kupata uzoefu wa kuwa sehemu ya familia na hisia ya utambulisho wa kiungu.
-
Familia zinaweza kutegemea uwezo wa Yesu Kristo kutatua kutoelewana, mabishano, na changamoto kupitia toba, msamaha na imani.
Hizi ni njia nne wewe unaweza kuimarisha familia yako kwa kuishi injili:
1 Himiza Sala
Familia zinakuwa imara pale wanaposali pamoja. Sala yaweza kubariki familia yako kwa amani, upendo na maelewano. Ikiwa sala si mazoea katika familia yako, omba ili kujua jinsi unavyoweza kuisaidia familia yako kusali pamoja. Kuwa tayari kufanyia kazi majibu utakayopokea.
2 Nendeni Kanisani Pamoja
Kanisani tunajifunza kuhusu injili ya Yesu Kristo. Pia tunashiriki sakramenti na kuweka agano na Mungu kwamba tuko tayari kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo na kumkumbuka daima.(ona Mosia 18:8–10; Mafundisho na Maagano 20:77, 79).
Kuhudhuria kanisani kama familia husaidia kumleta kila mtu karibu na Mungu na kwa kila mmoja. Inahitaji msimamo kwenda kila juma, lakini Mungu atabariki jitihada zako. Ikiwa familia yako itachagua kutohudhuria kanisani pamoja nawe, tafadhali fahamu kwamba kuhudhuria kwako kutakuimarisha na kukusaidia kupata njia zingine za kuimarisha familia yako.
3 Penda na Tumikia
Mwokozi alifundisha “Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi” (Yohana 15:12). Iambie familia yako jinsi unavyowapenda—hata kama una uhakika kwamba tayari wanafahamu. Kuonesha upendo wako kwa familia yako kupitia maneno na matendo humwalika Roho nyumbani kwako.
Kuwatumikia wanafamilia ni njia muhimu ya kuonesha upendo wako. Na kuwatumikia wengine pamoja pia huileta familia yako karibu na kila mmoja na kwa Baba wa Mbinguni. Sio lazima kuandaa mradi mkubwa wa huduma. Huduma inaweza kuwa rahisi, kama vile kuandaa chakula pendwa kwa ajili ya jirani. Kutumikia kama familia huleta furaha kwa sababu, kama tusomavyo katika maandiko, “Mnapowatumikia wanadamu wenzenu mnamtumikia tu Mungu wenu.” (Mosia 2:17).
4 Ishi Injili
Familia nyingi zina washiriki ambao si waumini wa Kanisa au ambao wamechagua kuacha kwenda kanisani. Bila msaada wa familia, inaweza kuwa vigumu kushiriki kanisani. Ikiwa familia yako iko katika hali kama hiyo, kumbuka kwamba bado wewe unaweza kuwa nguvu ya wema kwa kuishi injili.
Acha familia yako ikuone ukiishi kile unachokiamini. Huwezi kujua wakati wanapotazama kile unachosema na kufanya. Hii italeta nuru ya injili kwa familia yako. Haijalishi hali ya familia yako, juhudi zako thabiti za kuishi injili zinaweza kufungua mlango kwa Roho kuongoza, kushawishi, na kuinua familia yako na kuwasaidia waje karibu na Mwokozi, Yesu Kristo.