2023
Masomo Matatu kutoka Miaka ya Ujana ya Joseph Smith
Septemba 2023


“Masomo matatu kutoka Miaka ya Ujana ya Joseph Smith,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Sept. 2023.

Masomo Matatu kutoka Miaka ya Ujana ya Joseph Smith

Tazama kile unachoweza kujifunza kutoka kwenye uzoefu wa Nabii Miaka 200 iliyopita.

mvulana

Je, umewahi kuhisi ugumu kuwa kwenye uzoefu wa watu walioshi zamani? Waliishi muda mrefu uliopita—Je, wanaweza kukufundisha chochote kuhusu maisha yako? Ndiyo! Joseph Smith ni mfano mkubwa. Wakati alipokuwa na umri wa miaka 18, alikuwa ameshajifunza mambo kadhaa kuhusu kupata majibu ya sala na uhusiano wake na Baba yake wa Mbinguni. Masomo hayo yanaweza kukusaidia leo.

Somo #1: Wakati mwingine inachukuwa muda kupata majibu.

Majibu ya sala si mara zote huja kwa haraka. Kungoja siyo rahisi—hususani wakati majibu ya haraka kwa takriban kila swali yanapopatikana kwenye intaneti.

Ikiwa unahisi kama inachukuwa muda mrefu kwa Mungu kukujibu, hauko peke yako. Joseph Smith alikuwa na umri wa miaka 12 wakati alipoanza kufikiri kuhusu “yote-muhimu yahusuyo ustawi wa nafsi [yake] ya milele.”1 Alikabiliana na maswali kuhusu ustahili wake binafsi na uovu wa ulimwengu kwa miaka miwili iliyofuatia. Ilichukuwa miaka miwili ya kutafakari, kujifunza maandiko, na kufanya kazi kupitia maswali hayo kabla ya Mungu na Yesu Kristo kumtokea katika Kijisitu Kitakatifu.

Vivyo hivyo na kwetu sisi. Tunapokuwa na maswali, inaweza kuchukuwa siku, miezi au hata miaka kabla hatujapata majibu. Lakini bado ni SAWA. Kazi tunayofanya wakati tukisuburi ni muhimu. Kumbuka kile Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alichofundisha: “Mbegu haina budi kurutubishwa na lazima tusubiri ikomae.”2

Joseph Smith akisoma waraka wa Yakobo

Somo #2: Mungu anatujua kwa jina.

Kabla hajafikisha miaka18 Joseph alikuwa ametembelewa na Mungu Baba, Yesu Kristo, na malaika Moroni. Hiyo ni ya kuvutia sana! Na viumbe hawa watakatifu wote walimjua Joseph kwa jina. Walimjua binafsi!

Mungu anakujua wewe pia binafsi. Wewe ni mtoto Wake na Analijua jina lako. Mungu alifundisha ukweli huu kuhusu uumbaji wake: “Vitu vyote vinahesabika kwangu, kwa kuwa ni vyangu nami navijua” (Musa 1:35).

Sehemu ya sababu ya Joseph kuwa na imani kufanya kile alicho takiwa kukifanya ilikuwa kwamba alielewa kwamba alikuwa mtoto wa Mungu, ambaye alimjua binafsi.

Joseph Smith katika Kijisitu Kitakatifu

Somo # 3: Tunapokuwa wenye kutubu, tunajiweka tayari kwa uzoefu wa kiroho.

Moja ya motisha kuu ya Joseph Smith kwenda kwenye Kijisitu Kitakatifu ilikuwa kutubu dhambi zake. Hiyo ni sababu ileile iliyofanya asali kwenye usiku ambapo malaika Moroni alimtokea: “kwa ajili ya msamaha wa dhambi [zake] zote na upuuzi wake wote” (Joseph Smith—Historia ya 1:29). Hii inatufundisha mambo mawili:

Kwanza, kama tumefanya makosa, hatupaswi kufikiri hatustahili kusali. Joseph alikuwa amefanya “dhambi na upuuzi,” bado hata hivyo alijua angeweza kusali na kupata msamaha.

Pili, tunapokuwa wenye kutubu, tunaweza kumhisi Roho kwa nguvu zaidi. Kama vile Mzee Jörg Klebingat wa Sabini alivyoeleza, “Kujiamini kiroho huongezeka wakati unapotubu dhambi kwa hiari na kwa shangwe.”3

Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba toba hutusaidia tuwe zaidi kama Mwokozi. Tunapotubu, tunafungua milango ya mbinguni. “Tunachagua kukua kiroho na kupokea shangwe—shangwe ya ukombozi katika Yeye.”4

Kwa hiyo kama unahitaji kutubu kuhusu kitu fulani, tubu! Si tu itakuletea amani na kukusaidia uwe zaidi kama Mwokozi, bali pia itakusaidia kumhisi Roho kwa nguvu zaidi na kupata majibu ya sala.

Joseph Smith yaweza kuwa aliishi muda mrefu uliopita, lakini masomo aliyojifunza kama kijana bado yanaweza kukusaidia leo. Ni sababu nyingine ya kuwa na shukrani kwa ajili ya Nabii Joseph Smith.