“Achilia, na Sikiliza,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Sept. 2023.
Achilia, na Sikiliza
Nilikuwa na mpango wa kufanikisha ndoto zangu. Lakini wakati nilipoachilia na kumruhusu Bwana kuongoza njia yangu, nilibarikiwa katika njia nzuri.
Wakati nilipokaribia miaka17, Nilihamia San Francisco, California, Marekani kwenda kwenye shule ya sanaa. Nilitamani kuja kuwa mtengenezai vielelezo wa Disney
Chuoni, nilijifunza mengi zaidi ya sanaa. Nilijifunza mimi nilikuwa nani kwa Baba yangu wa Mbinguni. Sikuwa nyumbani tena. Wazazi wangu hawakuwa wakiniamsha kunipeleka Kanisani kila Jumapili. Hakuna ambaye angejua kama nilikuwa naishi injili au la. Lakini nilijua nilimuhitaji Yeye. Nilitafuta Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho katika kitabu cha simu. Nilipoingia ndani ya jengo la Kanisa na kusikia “Najua Kristo Yu Hai” (Nyimbo za Dini, na. 68) ukiimbwa, nilihisi kama vile nyumbani. Nilianza kutambua kile injili ilichomaanisha kwangu na ni kipi kwa dhati nilikitaka.
Mfanye Bwana kuwa namba Moja Kwenye Maisha Yako
Katika wakati huo, nilitaka kumhusisha Baba yangu wa Mbinguni katika kila kitu nilichokifanya. Kwa mfano, nilianza kumwuliza Alifikiri nini kuhusu mipango yangu ya kazi na wapi napaswa kuwa. Nilipokuwa nikisali na kuuliza maswali haya, nilianza kuhisi kwamba nilihitaji kuwa sehemu nyingine tena.
Nilivunjika moyo kidogo. Nilikuwa nimeweka ndoto zangu zote na fokasi yangu kwenye mpango wangu. Nilifikiri nilijua kinagaubaga wapi ningekwenda na nini ningefanya. Lakini sasa, nilijua nilimtaka Bwana kuwa namba moja kwenye maisha yangu, na hili lilikuwa la maana zaidi kwangu kuliko chochote. Hata kama nilijua kwamba njia yangu inaweza kuwa tofauti kutoka kile nilichokuwa nimekipanga, nilikuwa nimehisi upendo Wake kwangu, na nilitumainia busara Yake.
Niliongozwa kwenda Chuo Kikuu cha Brigham Young–Idaho na Chuo Kikuu cha Brigham Young kilichopo Provo, Utah, kumaliza shahada zangu za vielelezo. Kabla tu ya kuhitimu, nilipata kazi kama mkufunzi katika studio ya michezo ya eneo lile. Takribani mwaka mmoja baadaye, baada ya kupewa ajira ya kudumu, bila kutarajia studio ilinunuliwa na Disney, jambo ambalo lilileta fursa mpya na ukuaji mpya.
Wakati unapokiacha kile unachodhani unahitaji kuwa nacho, Bwana atakubariki kwa wakati muafaka na kile ambacho kwa dhati kitakupa furaha. Huwezi kujua ni wapi Bwana atakupeleka. Achilia tu, na sikiliza.
Weka vitu vya kwanza kuwa vya kwanza.
Nikiwa shuleni, ilinibidi nishughulikie madarasa na kazi za shule za kufanyia nyumbani pamoja na majukumu ya Kanisani. Ilinibidi niamue vipaumbele vyangu vilikuwa ni vipi. Je, ninakwenda kuwatembelea watu ili niwahudumie, au ninasoma kwa ajili ya mtihani? Je, ninasoma maandiko yangu sasa hivi, au namalizia kazi ya shuleni?
Kila mara nilipomweka Bwana kwanza na kufanya kazi Aliyoniita kuifanya, vitu siku zote vilienda vizuri. Siku zote Anatimiza ahadi Zake. Tunapomweka Bwana kwanza, vitu vingine vyote huwa sawa sawa.
Nilipokwenda shule ya kuhitimu shahada, nilikutana na chaguzi zilezile. Nilikuwa rais wa wasichana wa kata kwa wakati huo. Siku moja ilibidi nichague kati ya kusoma kwa ajili ya mtihani na kuwasaidia wasichana kupanga shughuli. Nilikwenda na wasichana. Pamoja na muda mchache niliokuwa nao, nilisali na kusoma kwa kadiri nilivyoweza. Kwa namna fulani nilifaulu mtihani, kwa daraja zuri mno kuliko nilvyotegemea.
Mwache Akuongoze
Baba wa Mbinguni atakuongoza. Anakupenda na anajua ni kipi hasa unahitaji. Anajua hasa ni kipi kitakachokubariki zaidi na lini.
Katika maisha yangu, mambo yamebadilika na kusonga kidogo. Lakini Amekuwa ndani yake wakati wote. Nilipofuata mwongozo Wake kwa ajili yangu, mambo yamegeuka kuwa mazuri. Sivyo jinsi nilivyotegemea, lakini mazuri.
Anataka kuwa sehemu ya maisha yetu. Kama tunaweza kumruhusu kwenye maisha yetu, kuna maajabu ya kustaajabisha yanamsubiri kila mmoja wetu. Je, ni kipi kingine Alichonacho kwenye ghala kwa ajili yako ambacho huwezi hata kukiona?