“Wakati Mpendwa Wako Anapokuwa na Changamoto za Afya ya Akili,” Kwa Ajili ya Nguvu Kwa Vijana, Sept. 2023.
Msaada wa Kimaisha
Wakati Mpendwa Wako Anapokuwa na Changamoto za Afya ya Akili
Haya ni mawazo matano ya kuweka akilini unapotaka kumsaidia mtu fulani ambaye anasumbuliwa na mfadhaiko, wasiwasi, au changamoto zingine za kihisia.
Inaweza kuumiza kumwona rafiki au mwanafamilia akipitia mfadhaiko, wasiwasi, au changamoto zingine za afya ya akili. Unaweza kutaka kufanya kitu fulani kusaidia lakini huna hakika ni kipi cha kufanya.
Haya ni mawazo matano ya kuweka akilini unapofikiria jinsi ya kumsaidia mtu fulani ambaye anasumbuliwa na mfadhaiko, wasiwasi au changamoto zingine za kihisia.
1 Wafikie.
Ikiwa unajiuliza kama ni vizuri zaidi kuwafikia au kuwa mbali, jibu ni: hakika wafikie. Mahusiano ya karibu hakika huwasaidia watu wanaosumbuka na afya ya akili. Wasiliana nao. Jumuika pamoja nao. Inaweza kuwa kitu fulani rahisi na cha kawaida, lakini wafikie.
2. Usitoe ushauri isipokuwa wameomba.
Kama mtu fulani hajaomba msaada wako, usianze kuwapa ushauri. Mpaka pale utakapoombwa ushauri, fokasi tu kwenye kuwa rafiki, kujali na kuwepo kwa ajili yao.
3. Kuwa mpole, mwenye nia chanya, na mwenye huruma.
Wakati mtu anapoomba msaada wako, fuata mfano wa Mwokozi. Sali kwa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya msukumo. Kuwa mwenye kuinua. Zungumza nao kwa upole. Sema vitu chanya. Onesha uelewa na huruma. Waruhusu wajue unawasaidia na upo pale kwa ajili yao. Kwa upole watie moyo watafute msaada wa kitaalamu.
4. Kuwa na subira na usikate tamaa
Watu wanaosumbuka wakati mwingine kwa nje wanaweza kutoonesha mwitikio au shukrani. . Lakini kuwa mwenye subira. Endelea kuwa nao. Upweke si kitu chenye afya kwao. Usijiondoe kabisa ikiwa hawaitikii katika njia ambayo ungependa.
5. Jilinde mwenyewe pia.
Hakikisha unapata furaha katika maisha yako. Endelea na sala yako binafsi na kujifunza maandiko. Hudhuria hekaluni. Fanya baadhi ya vitu vingine unavyovifurahia. Usiache msongo wa mawazo au wasiwasi wa wale uwapendao uwe mzigo kwenye maisha yako. Wafikie wengine kwa ajili ya msaada kama unauhitaji.