Pale Haki, Upendo, na Rehema Hukutana
Yesu Kristo aliteseka, akafa, na kufufuka kutoka kwa wafu ili kwamba Yeye aweze kutuinua hata kwa uzima wa milele.
Bila ya kamba za usalama, lijamu au vifaa vya kukwea mlima vya aina yoyote, kaka wawili---Jimmy, mwenye umri wa miaka 14, na John, miaka 19 (hayo si majina yao halisi)---walijaribu kukwea ukuta wima wa korongo kuu katika eneo la bunga ya Snow Canyon State, katika eneo la kuzaliwa kwangu la Utah kusini. Wakiwa karibu na kilele cha juhudi zao za kukwea kwa shida, kwa mshangao waligundua kwamba kulikuwa mwamba uliochomoka iliowazuia kupanda hatua chache za mwisho. Hawakuweza kuvuuka, wala kurudi nyuma sasa.Walikuwa wamekwama. Baada ya kujitahidi kutumia werevu na uangalifu, John alipata nafasi ya kumsaidia kakake mdogo kufikia sehemu salama juu ya mwamba. Lakini hakupata njia ya kujiinua mwenyewe. Kadiri alivyojitahidi kupata wenzo kwa vidole na miguu, ndivyo misuli yake ilianza kukamaa. Wasiwasi ukamkumba, na akaanza kuhofia maisha yake.
Akishindwa kushikilia kwa muda zaidi, John aliamua kuwa njia ya pekee ilikuwa ni kujaribu kuruka juu katika jitihada za kuufikia ukingo wa mwamba. Kama angefaulu, angeweza, kwa kutumia nguvu kiasi za mkono wake, kujivuta hadi kwenye usalama.
Kwa maneno yake mwenyewe, alisema:
“Kabla ya kuruka kwangu nilimwambia Jimmy aende akatafute tawi la mti imara lenye uwezo wa kunifikia mimi kutoka juu, japokuwa nilijua hapakuwa na kitu kama hicho kwenye kilele cha miamba. Ilikuwa ni ujanja tu kumwondoa hapo. Kama ningeshindwa kuruka vizuri, basi angalau ningehakikisha kuwa hangeniona nikianguka hata kwenye kifo changu.
“Nikimpa nafasi ya kutosha kuwa mbali nami, nilitoa sala yangu ya mwisho---kwamba nilitaka familia yangu ijue niliwapenda na kwamba Jimmy angeweza kurudi nyumbani mwenyewe---kisha nikaruka. Nilikuwa na adrenalini za kutosha katika kuruka kwangu hivi kwamba kuruka kwangu kulinyosha mikono yangu juu ya ukuta karibu na viwiko vyangu. Lakini nilipobandika mikono yangu juu yake, sikuhisi chochote isipokuwa changarawe iliyotawanyika kwenye mwamba huo tambarare. Bado ninaweza kukumbuka hisia ya changarawe nikininginia pale bila ya chochote cha kushikilia---hakuna ukingo, wala mwamba, hakuna chochote cha kushikilia. Nikahisi vidole vyangu vinaanza kuteleza taratibu katika mchanga. Nilijua maisha yangu yamekwisha.
“Lakini ghafla, kama radi wakati wa kimbunga cha majira ya joto, mikono miwili ikachomoka kwa ghafla kutoka mahali fulani juu ya ukingo wa jabali, ikashika vifundo vya mikono yangu kwa nguvu na juhudi zilizoshinda ukubwa wake. Kaka yangu mdogo mwaminifu hakuwa ameenda kutafuta tawi la mti lisilokuwepo. Akikisia hasa nilichopanga kukifanya, hakusonga hata kidogo. Alisubiri---kimya, bila kupumua---akijua kabisa kuwa ningekuwa mjinga kujaribu kuruka. Niliporuka, alinishika kwa nguvu, alining’ang’ania, na akakataa kuniachilia nianguke. Mikono ya ukaka yenye nguvu iliokoa maisha yangu siku ile nikiwa naning’inia hewani bila msaada kwa kile ambacho kwa hakika kingekuwa kifo.”1
Ndugu na dada zangu wapendwa, leo ni Jumapili ya Pasaka. Ijapokuwa tunapaswa daima kukumbuka (tunaahidi katika sala ya sakramenti kila wiki kwamba tutamkubuka), hata hivyo hii ni siku takatifu zaidi ya mwaka kwa ajili ya ukumbusho maalumu wa mikono ya ukaka, viganja shupavu ambavyo vilifikia lindi kuu la kifo ili kutuokoa toka kwenye maanguko yetu na kushindwa kwetu, toka kwenye masikitiko na dhambi zetu. Kwenye muktadha ya hadithi hii iliyoripotiwa na familia ya John na Jimmy, ninatoa shukrani zangu kwa ajili ya Upatanisho na Ufufuko wa Bwana Yesu Kristo na ninakubali matukio katika mpango mkamilifu wa Mungu ambayo yalitokea na kutoa maana ya “upendo wa Kristo alioutoa [kwetu].”2
Katika jamii yetu inayozidi kuwa ya kilimwengu ni kawaida kama, isivyo mtindo ufaao kuzungumzia kuhusu Adamu na Hawa au Bustani la Edeni au “bahati ya kuanguka” kwao katika maisha ya mauti. Hata hivyo ukweli rahisi ni kwamba hatuwezi kuuelewa kwa ukamilifu Upatanisho na Ufufuko wa Kristo na hatutaweza kutambua vyema kusudi la kipekee ya kuzaliwa Kwake au kufa Kwake---kwa maneno mengine, hakuna njia ya kusherehekea kwa kweli Krismasi ama Pasaka---bila ya kuelewa kwamba kulikuwepo na Adamu na Hawa halisi ambao walianguka toka Edeni wakiwa na matokeo ya kule kuanguka kwao.
Sijui utondoti wa kile kilichotokea katika sayari hii kabla ya hapo, lakini ninajua hawa wawili waliumbwa chini ya mikono mitakatifu ya Mungu, kwamba kwa muda waliishi peke yao katika hali ya kiparadiso ambako hapakuwa na kifo wala matarajio ya kuwa na familia, na kwamba kupitia mfululizo wa chaguzi walivunja amri ya Mungu ambapo wahitajika waondoke kutoka kwenye mazingira ya bustani yao lakini kuwawezesha wao kupata watoto kabla ya kukumbwa na mauti.3 Kwa kuongezea huzuni nachangamano katika hali yao, kuanguka kwao kulikuwa na madhara ya kiroho pia, kuwaondoa kabisa kutoka katika uwepo wa Mungu milele. Kwa sababu hiyo basi tunazaliwa katika dunia iliyoanguka na kwa sababu nasi pia tungevunja sheria za Mungu, nasi pia tulihukumiwa katika adhabu ambazo Adamu na Hawa walikuwa wanakabiliwa nazo.
Ni taabu ya jinsi gani! Wanadamu wote wakiwa katika kuanguka kusikozuilika---kila mwanaume, mwanamke, na mtoto wote wakiwa ndani ya mporomoko kwa vurumai kwenye kifo cha kudumu, kiroho wakitumbukia kwenye machungu ya milele. Je! Hivyo ndiyo maisha yalitakiwa kuwa? Je! Haya ndiyo matokeo ya mwisho ya uzoefu wa mwanadamu? Sisi sote tunaning’inia kwenye korongo baridi katika sehemu fulani ya ulimwengu usiojali, kila mmoja wetu akitafuta sehemu ya kushikilia, kila mmoja wetu akitafuta kitu chochote cha kushikilia---bila chochote isipokuwa hisia ya mchanga ukiteleza chini ya vidole vyetu, bila cha kutuokoa, bila cha kushikilia, na kwa hakika bila chochote cha kutushikilia sisi. Je, lengo letu katika maisha lilikuwa ni majaribio ya kuishi kwa utupu?---yaani kuruka juu kadiri tuwezavyo, na kuendelea kuvumilia kwa takribani miaka sabini, kisha kushindwa na kuanguka, na kuendelea kuanguka milele?
Jibu kwa maswali haya ni la, hasha, ya milele bila kusita! Pamoja na manabii wakale na wa sasa, ninashuhudia kwamba “mambo yote yamefanywa kwa hekima zake yule ajuaye mambo yote.”4 Hivyo, tangu pale wazazi wa kwanza walipotoka nje ya Bustani la Edeni, Mungu na Baba yetu sote, akitarajia maamuzi ya Adamu na Hawa, akawatuma malaika kutoka mbinguni kuwatangazia---kupitia wakati huo hadi sisi leo---kwamba msururu wote huu ulipangwa kwa ajili ya furaha yetu ya milele. Ilikuwa ni sehemu ya mpango Wake wa kiungu ambao Mwokozi alitolewa, Mwana wa Mungu Mwenyewe, ---“Adamu” mwingine---kama vile Mtume Paulo angemwita,5 ambaye angekuja wakati wa meridieni ili kulipia makosa ya Adamu wa kwanza. Upatanisho huo ungefanikisha ushindi kamili dhidi ya kifo cha mwili, na kutoa bila masharti uwezo wa kufufuka kwa kila mtu aliyezaliwa na yule atakayezaliwa katika ulimwengu huu. Kwa rehema pia hutatoa msamaha wa dhambi kwa watu wote kutoka kwa Adamu hata mwisho wa ulimwengu, kwa masharti ya kutubu na kutii amri za kiungu.
Kama mmoja wa mashahidi wake waliosimikwa, ninatangaza katika asubuhi hii ya Pasaka kwamba Yesu wa Nazareti ndiye yule Mwokozi wa ulimwengu, ndiye “Adamu wa mwisho,”6 Mwanzilishi na Mtimizaji wa imani yetu, Alfa na Omega wa uzima wa milele. “Kama vile watu wote wanakufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo,”7 Paulo alitangaza. Vivyo hivyo kutoka kwa nabii---baba mkuu Lehi: “Adamu alianguka ili wanadamu wawe. … na Masiya anakuja katika wakati mtimilifu, ili awakomboe watoto wa watu kutokana na mwanguko.”8 Zaidi ya yote, nabii Yakobo wa Kitabu cha Mormoni alifundisha kama sehemu ya mahubiri yake ya siku mbili juu ya Upatanisho wa Yesu Kristo “ufufuko lazima … umfikie … kwa njia ya mwanguko.”9
Kwa hivyo leo tunasherehekea zawadi ya ushindi dhidi ya kila mwanguko ambao tumeweza kukumbana nao, kila huzuni ambao tumekuwa nao, kukata tamaa tulikoweza kupata, kila hofu tuliokumbana nayo---bila kusahau ufufuko wetu toka kifo na msamaha wa dhambi zetu. Ushindi huo unapatikana kwetu kwa sababu ya matukio yaliyotokea kwenye wikendi kama hii zaidi ya milenia mbili zilizopita kule Yerusalemu.
Kuanzia kwenye machungu ya kiroho ya Bustani la Gethsemane, kuelekea kwenye Usulubisho msalabani pale Kalvari, kumalizikia Jumapili njema ndani ya kaburi alilopewa bure, mtu asiye na dhambi, msafi, na mtakatifu, Mwana wa Mungu Mwenyewe, alifanya ambacho hakuna kati ya mtu aliyekufa ameweza kukifanya. Chini ya uwezo Wake mwenyewe, Alifufuka, kamwe mwili wake hauwezi kutengana na nafsi Yake tena. Kwa hiari yake mwenyewe, alivua sanda ambayo alivalishwa, kwa umakini akaifungua sanda ambayo alivalishwa usoni “akaiweka kando,”10 maandiko yanasema.
Mfuatano huu wa siku tatu za Upatanisho na Ufufuko na yale yote Yesu Alikumbana nayo katika mchakato yanajumuisha matukio muhimu, dhabihu ya kipekee, na ni maonyesho yenye matokeo ya upendo wa kiungu ambao haujawahi kuonyeshwa katika historia ya ulimwengu. Yesu Kristo aliteseka, alikufa, na alifufuka ili kwamba Aweze, kama radi wakati wa kimbunga cha majira ya joto, anyooshe mikono miwili ya usaidizi, mikono miwili ya ukaka ili kutushika, kutuinua na kupitia kwa uaminifu wetu Kwake atatuinua katika uzima wa milele.
Pasaka hii ninamshukuru Yeye na Baba, ambaye Aliyemtoa Yeye kwetu, kwamba Yesu bado amesimama kwa ushindi dhidi ya kifo, ijapokuwa Yeye anasimama na miguu iliyojeruhiwa. Pasaka hii ninamshukuru Yeye na Baba, ambaye alimtoa kwetu, kwamba Yesu bado anatupa neema isiyo na mwisho, ijapokuwa ananyoosha viganja na vifundo vilivyojeruhiwa. Pasaka hii ninamshukuru Yeye na Baba ambaye alimtoa kwetu, ili tuweze kuimba mbele ya bustani iliyochafuka kwa jasho, misumari kwenye msalaba, na kaburi tukufu lililo tupu:
Je! Ni mtukufu jinsi gani, ni kamili jinsi gani,
Usanifu mkuu wa ukombozi,
Pale haki, upendo, rehema hukutana
Kwenye uwiano wa kiungu!11
Katika jina takatifu la Yesu Kristo mfufuka, amina.