Shukrani Siku ya Sabato
Kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, siku ya Sabato ndiyo ya shukrani na upendo.
Kaka zangu na dada zangu wapendwa ambao mmetawanyika ulimwenguni kote katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Nina furaha kwamba Rais Thomas S. Monson ameniomba niongee katika mkutano huu mkuu kwenye siku hii ya Sabato. Ninaomba kwamba Roho Mtakatifu ayapeleka maneno yangu kwenye mioyo yenu.
Leo natamani kunena juu ya hisia za moyo. Jambo moja nitazingatia ni shukrani—hususani siku ya Sabato.
Tunashukuru kwa mambo mengi: wema toka kwa tusiyemfahamu, chakula wakati tuna njaa, paa lililopo juu yetu wakati wa kimbunga, kupona kwa mfupa uliovunjika, na kulia kwa dhati kwa mtoto mchanga anayezaliwa. Wengi wetu tutakumbuka kuhisi furaha katika vipindi kama hivyo.
Kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, Sabato ni muda, hasa ni siku ya shukrani na upendo. Bwana aliwaelekeza Watakatifu katika wilaya ya Jackson, Missouri, 1831 kwamba sala zao na shukrani ninapaswa kuelekezwa juu mbinguni. Watakatifu wa mwanzo walipewa ufunuo jinsi ya kuitakasa siku ya Sabato na jinsi ya kufunga na kuomba.1
Wao, na sisi, tuliambiwa na Bwana jinsi ya kuabudu na kutoa shukrani siku ya Sabato. Kama mnavyoweza kuona, kikubwa zaidi ni upendo tunaohisi kuhusu mtoa zawadi. Hapa kuna maneno ya Bwana ya jinsi ya kushukuru na jinsi ya kuonyesha upendo siku ya Sabato:
“Ninawapa amri, nikisema: Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa uwezo wako wote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote, na katika jina la Yesu Kristo utamtumikia yeye. …
“Nawe utamshukuru Bwana Mungu wako katika mambo yote.
“Nawe utamtolea dhabihu Bwana Mungu wako katika haki, hata ya ile ya moyo uliovunjika na roho iliyopondeka.”2
Na kisha, Bwana anaendelea kuonya juu ya kushindwa kuwapenda na kuwashukuru Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kama watoaji wa vipawa: “Na katika lolote mwanandamu hamkosei Mungu, au ghadhabu ya Mungu haiwaki kwa yeyote, isipokuwa wale tu wasiokiri mkono wake katika mambo yote, na wasiotii amri zake.”3
Wengi wenu mnaosikiliza tayari mnapata furaha katika Sabato kama siku ya kukumbuka na kutoa shukrani kwa Mungu kwa ajili ya baraka. Unaukumbuka wimbo unaojulikana:
Ukirushwarushwa na dunia hii,
Utakapo kufa moyo kwa kuudhika,
Hesabu baraka moja kwa moja,
Nawe utaona ni ajabu kuu
Hesabu baraka;
Moja kwa moja.
Hesabu baraka;
Ona yale Mungu ayafanyayo. …
Je, unalemewa na mzigo?
Msalaba wako ni mzito tu?
Hesabu baraka shaka ziishe,
Nawe utaimba siku zinaposonga mbele.4
Mimi hupokea barua na kutembelewa na Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaohisi kulemewa na mzigo. Baadhi wako karibu kuhisi kwamba, kwao, karibu vyote vimepotea. Ninatumaini na kuomba kwamba ninachosema kuhusu shukrani siku ya Sabato kitasaidia kufanya shaka zitokomee na kuanza kuimba katika mioyo yetu.
Baraka moja ambayo kwayo sisi tunashukuru ni kwamba tuko katika huo mkutano wa sakramenti, tukikusanyika na zaidi ya mmoja au wawili wa wanafunzi Wake katika jina Lake. Kuna wengine nyumbani wameshindwa kuamka kutoka vitandani mwao. Kuna wengine ambao wangependa kuwa pale tulipo lakini badala yake wanahudumu katika hospitali na kuangalia usalama wa umma au kukutetea wew kwa kuhatarisha maisha yao wenyewe katika jangwa au msitu fulani. Ukweli ni kwamba tunapoweza kukusanyika na hata Mtakatifu mmoja na kupokea sakramenti kutatusaidia kuanza kuhisi shukrani na upendo kwa ukarimu wa Mungu.
Kwa sababu ya Nabii Joseph Smith na injili iliyorejeshwa, baraka ya ingine tunayoweza kupata ni kwamba tuna nafasi ya kupokea sakramenti kila wiki—ikiandaliwa, kubarikiwa, na kupitishwa na watumishi wa Bwana wenye mamlaka. Tunaweza kushukuru Roho Mtakatifu athibitishapo kwetu kwamba maneno ya sala ya sakramenti, yanayotolewa na mwenye ukuhani walio mamlaka, yanaheshimiwa na Baba yetu wa Mbinguni.
Kati ya baraka zote tunazoweza kuhesabu, kuu zaid kati yazo ni hisia za msamaha ambao huja tunapopokea sakramenti. Tutahisi upendo mwingi na shukrani kwa Mwokozi, ambaye dhabihu Yake isiyo na mwisho iliwezesha kutakaswa kwetu kutokana na dhambi. Tunapopokea mkate na maji, tunakumbuka kwamba Yeye aliteseka kwa ajili yetu. Na tunapohisi shukrani kwa kile Yeye ametufanyia, tunahisi upendo Wake kwetu na upendo wetu Kwake.
Baraka ya upendo tunayopokea itafanya iwe rahisi zaidi kwetu kushika amri ili “daima kumkumbuka yeye.”5 Unaweza kuhisi upendo na shukrani kwa Roho Mtakatifu, ambaye Baba wa Mbinguni aliahidi atakuwa nasi daima tunapobaki waminifu katika maagano tuliyoweka. Tunaweza kuhesabu hizo baraka zote kila Jumapili na kuhisi shukrani.
Sabato pia ni muda muafaka wa kukumbuka agano tuliloweka kwenye maji ya ubatizo kuwapenda na kuwatumikia watoto wa Mungu. Kutimiza ahadi hiyo siku ya Sabato itajumuisha kushiriki darasani au akidi kwa malengo kamili ya moyo kujenga imani na upendo miongoni mwa kaka na dada zetu ambao wako pamoja nasi. Ahadi hiyo itajumuisha kutimiza miito yetu kwa furaha.
Mimi nina shurkani kwa ajili ya Jumapili nyingi nilizowafundisha akidi ya mashemasi huko Bountiful, Utah, pia darasa la Shule ya Jumapili huko Idaho. Na mimi hata ninakumbuka wakati nilipohudumu kama msaidizi wa mke wangu kwenye darasa la chekechea, ambako wajibu wangu mkubwa ulikuwa ni kutoa na kuokota wanasesere
Ilikuwa miaka kabla sijagundua kupitia Roho kwamba huduma yangu ndogo kwa Bwana ilikuwa na maana katika maisha ya watoto wa Baba wa Mbinguni. Kwa mshangao wangu, baadhi yao wamekumbuka kunishukuru kwa juhudi zangu za kuwahudumia kwa ajili ya Bwana katika Sabato hizo.
Kama vile wakati mwingine tunashindwa kuona matokeo ya huduma zetu wenyewe tuzitoazo siku ya Sabato, huenda tusione matokeo ya watumishi wengine wa Bwana. Lakini Bwana anajenga ufalme Wake kimyakimya kupitia wachungaji Wake waaminifu na wanyenyekevu na kwa mbwembwe kidogo kuelekea utukufu wake wa milenia ya baadaye. Inahitaji Roho Mtakatifu kuuona utukufu ukikua.
Nilikua huku nikienda kwenye mikutano ya sakramenti katika tawi dogo sana la New Jersey lenye waumini wachache na familia moja, yangu mwenyewe. Miaka sabini na tano iliyopita, nilibatizwa Philadelphia kwenye Kanisa pekee lililojengwa huko Philadelphia au New Jersey. Hali kulikuwepo na tawi moja dogo huko Princeton, sasa kuna kata mbili kubwa. Na siku chache zilizopita, maelfu ya vijana walitumbuiza katika sherehe zilizotangulia wakati wa kuweka wakfu Hekalu la Philadelphia Pennsylvania.
Nikiwa kijana, niliitwa kama misionari wa wilaya katika kanisa dogo pekee huko Albuquerque, New Mexico. Leo kuna hekalu na vigingi vinne.
Niliondoka Albuquerque kwenda shule huko Cambridge, Massachusetts. Kulikuwa na kanisa dogo moja na kigingi kimoja ambacho kilitawanyika kati ya Massachusetts na Rhode Island. Niliendesha gari nikipita kwenye vilima vya nchi ile nzuri kwenda kwenye mikutano ya sakramenti kwenye matawi madogo, mengi yakiwa kwenye nyumba za kukodi au nyumba ndogo zilizofanyiwa ukarabati . Sasa kuna hekalu takatifu la Mungu huko Belmont, Massachusetts na vigingi ambavyo vimetapakaa nchi nzima.
Kile ambacho sikuweza kukiona vizuri wakati ule ni kwamba Bwana alikuwa akitoa Roho Wake kwa watu katika mikutano hiyo midogo ya sakramenti. Niliweza kuhisi, lakini sikuweza kuona kiasi na majira ya nia ya Bwana ili kujenga na kuutukuza ufalme Wake Nabii, kwa ufunuo, aliona na kuandika kile ambacho sasa tunaweza kukiona wenyewe. Nefi alisema kwamba idadi yetu isingeweza kuwa kubwa, lakini mkusanyiko wa mwanga utaweza kuonekana:
“Na ikawa kwamba niliona kanisa la Mwanakondoo wa Mungu, na hesabu yake ilikuwa chache. …
“Na ikawa kwamba mimi, Nefi, niliona nguvu za Mwanakondoo wa Mungu, kwamba ziliwashukia watakatifu wa kanisa la Mwanakondoo, na kwa watu wa agano la Bwana, ambao walitawanyika kote usoni mwa dunia; na walikuwa wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu.”6
Katika nyakati hizi za maongozi haya ya Mungu, maelezo kama haya ya kinabii juu ya hali yetu na fursa iliyo mbele imeandikwa katika Mafundisho na Maagano:
“Nanyi bado hamjaelewa jinsi baraka kuu Baba alizo nazo katika mikono yake mwenyewe na amezitayarisha kwa ajili yenu;
“Na hamwezi kustahimili mambo yote kwa sasa; hata hivyo, changamkeni, kwa kuwa nitawaongoza. Ufalme ni wenu na baraka zake ni zenu na utajiri wa milele ni wenu.
“Na yule apokeaye vitu kwa shukrani atatukuzwa; na vitu vya dunia hii ataongezewa, hata mara mia, ndio, na zaidi.”7
Nimehisi kwamba mpito wa kukua kwa shukrani kwa ajili ya baraka na upendo wa Mungu unaongezeka kwa Kanisa zima. Unaonekana kusambaa miongoni mwa waumini wa Kanisa katika nyakati na sehemu ambazo kuna majaribu ya imani yao, ambako inawapasa wamwombe Mungu kwa ajili ya msaada.
Nyakati tutakazopitia zitakuwa na majaribu magumu kama ilivyokuwa kwa watu wa Alma chini ya katili Amuloni, ambaye aliweka mizigo migongoni mwao mizito kuibeba:
“Na ikawa kwamba sauti ya Bwana iliwafikia katika mateso yao ikisema: Inueni vichwa vyenu na msherehekee, kwani ninajua agano ambalo mlinifanyia; na nitaagana na watu wangu na kuwakomboa kutoka utumwani.
“Na pia nitawapunguzia mizigo ambayo imewekwa mabegani mwenu, hata kwamba hamtaisikia kamwe migongoni mwenu, hata mkiwa utumwani; na nitafanya haya ili muwe mashahidi wangu hapo baadaye, na kwamba mjue kwa hakika kwamba mimi, Bwana Mungu, huwatembelea watu wangu katika mateso yao.
“Na sasa ikawa kwamba mizigo ambayo ilikuwa wamewekewa Alma na ndugu zake ilipunguzwa; ndio, Bwana aliwapa nguvu kwamba wabebe mizigo yao kwa urahisi, na walinyenyekea kwa furaha na subira kwa mapenzi ya Bwana.”8
Wewe na mimi ni mashahidi kwamba pale tunaposhika maagao yetu na Mungu, hasa wakati ilipokuwa vigumu, Amesikia maombi yetu ya shukrani kwa kile ambacho tayari ameshakifanya kwetu na amejibu maombi yetu kwa nguvu ili kuvumilia kwa uaminifu. Zaidi ya mara moja ametufanya tuchangamke na pia kuwa na nguvu.
Unaweza ukawa unashangaa ungeweza kufanya nini ili kuishi na kuabudu katika siku ya Sabato ili kuonyesha shukrani na kujiimarisha mwenyewe na wengine kwa majaribu yaliyopo mbele.
Unaweza kuanza leo kwa maombi ya peke yako na ya familia ya kumshukuru Mungu kwa aliyokufanyia. Unaweza kuomba ili kujua ni nini ambacho Bwana anataka wewe ufanye ili umtumikie Yeye na wengine. Hasa, unaweza kuomba ili Roho Mtakatifu akuambie kuhusu mtu ambaye yuko peke yake au yule ambaye Bwana angetaka umwendee.
Ninaweza kukuahidi maombi yako yatajibiwa, na unapotenda kulingana na majibu utakayopokea, utapata furaha katika siku ya Sabato na moyo wako utafurika kwa shukrani.
Ninashuhudia kwamba Mungu Baba anakujua na anakupenda. Mwokozi, Bwana Yesu Kristo alifanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zako kutokana na upendo kwa ajili yako. Wao, Baba na Mwana walijua jina lako kama Walivyolijua jina la Nabii Joseph Smith wakati Walipomtokea. Ninashuhudia kwamba hili ni Kanisa la Yesu Kristo na kwamba Yeye atayaheshimu maagano uliyoweka na kuyafanya upya na Mungu. Asili yako yenyewe itabadilika na kuwa zaidi kama Mwokozi. Utaimrishwa dhidi ya majaribu na dhidi ya hisia za shaka kuhusu ukweli. Utapata furaha katika Sabato. Mimi nakuahidi hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.