Bwana Yesu Kristo Anatufundisha Kusali
Wakati unaposali, unasali kwa kweli au unasema tu sala?
Mwaka wa 1977, nilikuwa nikihudumu kama mmisionari kule Cusco, Peru. Mwenzi wangu nami tulipata idhini ya kuwapeleka wamisionari wote wa eneo la Cusco kwenye magofu ya ajabu ya Machu Picchu.
Kuelekea mwisho wa ziara yetu katika magofu, baadhi ya wamisionari walitaka kwenda kwenye Daraja la Inca, lililokuwa katika sehemu ya njia ya mlimani. Mara moja, nilihisi moyoni Roho akinizuia tusiende mahala pale. Njia ilikuwa kwenye upande wa mlima uliokuwa na mteremko wa futi 2000 (610 m). Katika sehemu kadhaa, njia ilikuwa pana tu kiasi cha kuruhusu mtu mmoja kupita kwa wakati mmoja. Mwenzi wangu nami tuliwaambia kwamba wasiende kwenye Daraja la Inca.
Hata hivyo, wamisionari walisisitiza kwamba twende. Utetezi wao ulizidi mno, na kinyume na kile Roho alikuwa ameniashiria, nilikubali ushawishi wa kundi na kuwaambia kwamba tungeenda kwenye daraja, lakini tu ikiwa tungekuwa waangalifu.
Tuliingia kwenye njia iliyoelekea hadi kwenye Daraja la Inca nikiwa nyuma ya kikundi, na mwanzoni, kila mtu alitembea polepole tulivyokuwa tumekubaliana. Kisha wamisionari wakaanza kutembea haraka na hata kukimbia. Walipuuza malalamiko yangu ya kuwataka wapunguze mwendo. Nilihisi wajibu wa kuwafikia, niwaeleze kwamba tulihitajika kurudi. Nilikuwa nyuma yao kabisa, na ilinibidi nikimbie haraka ili niweze kuwafikia.
Nilipokaribia kona, kwenye kijia ambapo palikuwa pembamba kwa watu wawili kutembea, nilimpata mmisionari akiwa amesimama tuli na mgongo dhidi ya miamba. Nilimwuliza ni kwa nini alikuwa amesimama pale. Aliniambia alikuwa amepokea wazo asalie mahali pale kwa muda na kwamba mimi niendelee.
Nilihisi umuhimu wa kuwafikia wale waliokuwa mbele yetu, kwa hivyo alinisaidia nikampita, na niliweza kufika mbele kidogo kwenye njia. Niliona ardhi ilikuwa imejaa mimea. Nilikanyaga na mguu wangu wa kulia kwenye ardhi, nikitambua, huku nikianguka, kwamba hapakuwepo na ardhi chini ya mimea. Nilifanya kila juhudi kushikilia baadhi ya matawi yaliyokuwa chini ya njia. Kwa muda niliweza kuona chini, takriban futi 2,000 chini yangu, Mto wa Urubamba unaovuka Bonde Takatifu la Incas. Nilihisi kama kwamba nguvu zangu zilikuwa zimeniishia, na ilikuwa tu muda mfupi kabla ya kushindwa kushikilia tena. Katika wakati huo, nilisali kwa dhati. Ilikuwa sala fupi sana. Nilifungua kinywa changu na kusema, “Baba, nisaidie!”
Matawi hayakuwa yenye nguvu kiasi cha kustahimili uzito wa mwili wangu. Nilijua mwisho ulikuwa karibu. Katika ule wakati ambapo nilikuwa karibu kuanguka, nilihisi mkono imara ukinishika mkononi na kunivuta juu. Kwa usaidizi huo, niliweza kuendelea kupambana na kurudi kwenye njia. Yule mmisionari aliyebaki nyuma ndiye aliyeniokoa.
Lakini kihalisia Baba yetu wa Mbinguni aliniokoa. Alisikiliza sauti yangu. Nilikuwa nimesikia sauti ya Roho mara tatu mwanzoni, akiniambia nisiende kwenye Daraja la Inca, lakini sikuwa nimetii sauti hiyo. Nilikuwa nimeshtuka, nikakwajuka, na sikujua la kusema. Kisha nikakumbuka kwamba wale wamisionari wengine walikuwa mbele yetu, kwa hivyo tulienda kuwatafuta hadi tukawapata na kuwaelezea yaliyokuwa yamenikumba.
Tulirudi Machu Picchu, kwa uangalifu zaidi, na kimya. Katika safari ya kurudi, nilisalia kimya, na dhana ikanijia akilini kwamba alikuwa amesikiliza sauti yangu lakini mimi sikuisikiliza Yake. Kulikuwa na uchungu mkubwa moyoni mwangu kwa kutotii sauti Yake na wakati huo huo pia hisia ya shukrani kubwa sana kwa hekima yake. Hakutumia haki Yake kwangu, lakini kwa hekima yake kuu, aliokoa maisha yangu (ona Alma 26:20).
Jioni, wakati wa sala yangu ya kibinafsi, nilisali kutoka moyoni “Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;” (2 Wakorintho 1:3). Nilisali “na moyo wa kweli, na kusudi halisi, nikiwa na imani katika Kristo” (Moroni 10:4).
Mapema asubuhi ya siku hiyo, nilisali kwa mdomo, na wakati nilipokuwa karibu kuangamia, nilisali Kwake kutoka moyoni. Nilitafakari maisha yangu kufikia hapo. Niligundua kwamba katika hali nyingi, Baba yetu wa Mbinguni alikuwa amenionyesha rehema. Alinifundisha mambo mengi siku hiyo kule Machu Picchu na kule Cusco, Peru. Mojawapo ya jambo muhimu nililojifunza ilikuwa ni kwamba sikuzote nisali na moyo wa kweli, na kusudi halisi, [mkifanya] imani katika Kristo.
Wakati fulani Bwana Yesu Kristo “ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba,” na “alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali” (Luka 11:1). Kisha aliwafundisha wanafunzi wake kusali. Na anatufundisha wewe na mimi kusali tumwonapo akilini mwetu akisali kule Gethsemane na akisema “walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke” (Luka 22:42). Wakati unaposali, ni kweli, kweli kabisa, unataka hivyo “si mapenzi yangu, bali yako yatendeke”?
Paulo anaeleza jinsi Yesu alisali “siku hizo za mwili wake,” hasa kule Gethsemane: “Alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; ” (Waebrania 5:7). Wakati unaposali, unasali kwa kweli au unasema tu sala? Wewe u makini katika sala zako?
Yesu alisali kwa dhati na alisema na Baba Yake. “Ikawa, kwamba Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; ” (Luka 3:21). Wakati unaposali, unahisi kama mbingu zimefunguka? Ni wakati gani wa mwisho ulihisi umeunganishwa na mbingu?
Yesu alijitayarisha kufanya uamuzi mkuu kwa kusali kwa Baba Yake.
“Aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu.
“Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao” (Luka 6:12–13).
Je, wewe hujitayarisha kufanya uamuzi muhimu kupitia maombi kwa Baba yako wa Mbinguni? Je, wewe hujiandaa kwa wakati wa maombi?
Wakati Yesu alipokuja katika bara la Amerika, aliwafundisha watu kusali. “Na Yesu akasema kwao: Endeleeni kuomba; walakini, hawakukoma kuomba” (3 Nefi 19:26).
Yesu anatualika “Omba daima” (M&M 10:5). Yesu anajua kwamba Baba yetu wa Mbinguni anasikia na anatupa kile kinachotufaa sisi. Kwa nini mara nyingine hatutaki kupokea? Kwa Nini?
Wakati ule ule tunaposema, “Baba aliye Mbinguni,” Yeye husikia maombi yetu na ni msikivu kwetu na mahitaji yetu. Na kwa hivyo macho yake na masikio yake sasa yameunganishwa nawe. Yeye anaona akili zetu, na anahisi mioyo yetu. Hauwezi ukamficha chochote. Sasa, jambo la ajabu ni kwamba atakuangalia kwa macho yenye upendo na rehema—upendo na rehema ambao hatuwezi kuelewa kikamilifu. Lakini upendo na rehema ipo naye wakati tu utasema, “Baba wa Mbinguni.”
Kwa hivyo wakati wa sala, ni wakati mtakatifu sana kabisa. Yeye si mwanadamu aseme, “La, sitakusikiliza hivi sasa, kwa sababu wewe hunijia tu wakati una shida.” Ni wanadamu tu hufanya hivyo. Yeye si mtu wa kusema, “Ee, huwezi ukatafakari jinsi nilivyo na shughuli nyingi mno hivi sasa.” Ni wanadamu ndiyo husema hivyo.
Kwamba sisi sote tuweze kusali jinsi Yesu alivyotufundisha ni matumaini yangu na maombi yangu katika jina la Bwana Yesu Kristo, amina.