Sakramenti Yaweza Kutusaidia Kuwa Watakatifu
Zingatia njia tano ambazo zinaweza kuboresha matokeo na uwezo wetu wa kushiriki kila siku katika ibada takatifu ya sakramenti.
Mojawapo kati ya kumbukumbu zangu za awali kabisa ni za mikutano ya sakramenti iliyofanyika nyumbani kwetu kule Warrnambool, Australia. Kati ya watu 10 na 15 walihudhuria tawi letu, na baba yangu, mmoja kati ya watatu wenye ukuhani, kawaida alipata nafasi ya kubariki sakramenti. Ninakumbuka hisia nilizokuwa nazo wakati aliposoma kwa unyenyekevu na kwa makini maneno ya sala za sakramenti. Mara nyingi sauti yake ilitetemeka alipohisi Roho. Mara nyingine ilimbidi atue kwa muda ili kudhibiti hisia zake kabla ya kukamilisha sala.
Kama mtoto mwenye umri wa miaka mitano, sikuelewa maana kamili ya kile kilichosemwa au kilichotendeka; hata hivyo, nilijua jambo maalum lilikuwa likitendeka. Niliweza kuhisi ushawishi mtulivu na wa kuondoa shaka wa Roho Mtakatifu wakati baba yangu alitafakari upendo wa Mwokozi kwetu.
Mwokozi alifundisha: “Daima mtafanya hivi kwa wale wanaotubu na kubatizwa katika jina langu; na mtafanya hivi kwa ukumbusho wa damu yangu, ambayo nilimwaga kwa ajili yenu, ili mshuhudie kwa Baba kwamba daima mnanikumbuka. Na ikiwa mnanikumbuka daima Roho yangu itukuwa na nyinyi” (3 Nefi 18:11).
Ninawaalikeni nyinyi nyote mzingatie njia tano ambazo zinaweza kuboresha matokeo na uwezo wetu wa kushiriki kila siku katika agizo takatifu la sakramenti, agizo ambalo linaweza kutusaidia kuwa watakatifu.
1. Jiandaeni Mapema
Tunaweza kuanza maandalizi ya sakramenti mapema kabla ya mkutano wa sakramenti kuanza. Jumamosi yaweza kuwa wakati mwafaka wa kutafakari kuhusu maendeleo yetu ya kiroho na maandalizi.
Maisha ya duniani ni kipaji muhimu katika safari yetu ya kuwa kama Baba wa Mbinguni. Kwa vyovyote, inajumuisha majaribu, na changamoto ambazo zinatoa nafasi kwetu sisi kubadilika na kukua. Mfalme Benjamin alifundisha kwamba “mwanadamu wa kawaida ni adui kwa Mungu, … na atakuwa, milele na milele, hasipokubali ushawishi wa Roho Mtakatifu, na kumvua mtu wa kawaida na kuwa mtakatifu kupitia upatanisho wa Kristo aliye Bwana” (Mosia 3:19). Kushiriki katika agizo la sakramenti kunatoa nafasi ya kusalimisha kikamilifu mioyo yetu na nafsi zetu kwa Mungu.
Katika maandalizi yetu, mioyo yetu hupondeka wakati tunapotoa shukrani kwa Upatanisho wa Kristo, kutubu makosa yetu na upungufu, na kuuliza msaada kutoka kwa Baba katika safari yetu tunapoendelea ya kuwa kama alivyo Yeye. Kisha tunaweza kutegemea nafasi ambayo sakramenti inatupa kukumbuka dhabihu Yake na kufanya upya sharti letu kwa maagano yote ambayo tumefanya.
2. Fika Mapema
Wakati wetu wa sakramenti unaweza kuimarishwa wakati tunapowasili mapema kabla ya mkutano na kutafakari muziki unaotangulia unapochezwa.
Mzee Boyd K. Packer alifundisha: “Muziki unaotangulia, unapochezwa kwa staha, ni chakula cha roho. Hualika maongozi.”1 ‘Huu si muda,” Russell M. Nelson alieleza, “wa mazungumzo au kupeana ujumbe lakini ni wakati wa kutafakari kwa maombi huku viongozi na waumini wakijiandaa kiroho kwa sakramenti.”2
3. Imba na Ujifunze kutoka kwa Maneno ya Wimbo wa Sakramenti
Wimbo wa sakramenti ni sehemu muhimu hasa ya wakati wetu wa sakramenti. Muziki huinua mawazo yetu na hisia. Wimbo wa sakramenti una ushawishi mkubwa zaidi wakati tunapozingatia kwa makini maneno na mafundisho yenye nguvu yanayofundishwa. Tunajifunza mengi kutoka kwa maneno kama “Alijeruhiwa, kuvunjwa kwa ajili yetu,”3 “Na tukumbuke na kuwa na hakika kuwa mioyo yetu na mikono ni misafi,”4 na “Pale Haki, upendo na rehema hukutana kwa uwiano wa kiungu!”5
Wakati tunapoimba wimbo wa injili katika maandalizi ya kupokea sakramenti, maneno hayo yanaweza kuwa sehemu ya sharti letu la agizo. Zingatia, kwa mfano,: “Twakupenda ewe, Bwana; mioyo yetu imejaa. Tutatembea katika njia yako teule.”6
4. Shiriki Kiroho katika Sala za Sakramenti (Ona Moroni 4–5)
Badala ya kupuuza maneno ya kawaida ya sala za sakramenti, tunaweza kujifunza mengi na kuhisi zaidi tunaposhiriki kiroho kwa kuzingatia ahadi na baraka zinazohusishwa zikijumuishwa katika sala hizi.
Mkate na maji hubarikiwa na kutakaswa kwa ajili ya nafsi zetu. Inatukumbusha kuhusu dhabihu ya Mwokozi na kwamba Yeye anaweza kutusaidia kuwa watakatifu.
Sala zinaeleza kwamba tunakula mkate kwa ukumbusho wa mwili wa Mwana, ambao aliutoa kama fidia kuwawezesha wote kufufuka, na tunakunywa maji kwa ukumbusho wa damu ya Mwana, ambayo alimwaga kwa ukarimu ili tuweze kukombolewa kwa sharti la toba.
Sala zinawasilisha maagizo kwa kishazi “kwamba wako radhi”(Moroni 4:). Kishazi hiki rahisi kina uwezo mkubwa sana kwetu sisi. Tuko radhi kuhudumu na kuchangia? Tuko radhi kubadilika? Tuko radhi kushughulikia udhaifu wetu? Tuko radhi kunyosha mkono wa usaidizi na kuwabariki wengine? Tuko radhi kumwamini Mwokozi?
Wakati ahadi zinapotajwa na tunaposhiriki, tunathibitisha katika mioyo yetu kwamba tuko radhi:
-
Kulichukua juu yetu jina la Yesu Kristo.
-
Kujitahidi kushika amri Zake zote.
-
Kumkumbuka daima.
Sala inahitimisha na mwaliko mtukufu na ahadi: “Ili daima Roho wake apate kuwa pamoja nao” (Moroni 4:3).
Paulo aliandika, “Tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, [na] upole kiasi” (Wagalatia 5:22–23). Baraka na zawadi nzuri zinapatikana ikiwa tutashika maagizo yetu.
5. Tafakari na Umkumbuke wakati Nembo za Sakramenti Zinapitishwa
Nyakati za staha wakati wenye ukuhani wanapopitisha sakramenti zinaweza kuwa takatifu kwetu.
Huku mkate unapopitishwa, tunaweza kutafakari kwamba katika tendo la hali ya juu zaidi la upendo Mwokozi “atajichukulia kifo, ili afungue kamba za kifo ambazo zinafunga watu wake” (Alma 7:12).
Twaweza kukumbuka baraka tukufu ya Ufufuo ambayo “itakuwa kwa wote, … wote wafungwa na huru, waume na wake, wote waovu na wenye haki; na hakuna hata unywele wa vichwa vyao utakaopotea; lakini kila kitu kitarejeshwa mahali pake kamili” (Alma 11:44).
Maji yanapopitishwa, twaweza kumbuka ombi la Mwokozi:
“Tazama, Mimi, Mungu nimeteseka mambo haya kwa ajili ya watu wote, ili kwamba wasiteseke kama watatubu; …
“Mateso ambayo yaliyosababisha Mimi mwenyewe, hata Mungu, mkuu kuliko yote, kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutoka damu kwenye kila kinyweleo, na kuteseka mwili na roho—na kutamani nisinywe kikombe kichungu, na kusita” (M&M 19:16, 18).
Tunakumbuka kwamba “atajichukulia unyonge [wetu], ili moyo wake ujae rehema, kulingana na mwili, ili ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge [wetu]” (Alma 7:12).
Tunapozingatia uzoefu wetu wa sakramenti, twaweza kujiuliza:
-
Ni kipi nitakachoweza kufanya wiki hii ili niweze kujiandaa vyema kwa sakramenti?
-
Ninaweza kuchangia zaidi kwa staha na ufunuo ambao huambatana na mwanzo wa mkutano wa sakramenti?
-
Ni fundisho gani lilifunzwa katika wimbo wa sakramenti?
-
Nilisikia nini na kuhisi nini nilipokuwa nikisikiliza sala za sakramenti?
-
Nilifikiria kuhusu nini wakati sakramenti ilipokuwa ikipitishwa?
Mzee David A. Bednar alifundisha: “Ibada ya sakramenti ni mwaliko mtakatifu na unaorudiwa kwa ajili ya kutubu kwa dhati na kufanywa upya kiroho. Tendo la kushiriki sakramenti, pekee yake tu, haliondoi dhambi. Lakini tunapojiandaa kwa dhamira na kushiriki katika ibada hii takatifu kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka, basi ahadi ni kwamba tunaweza daima kuwa na Roho wa Bwana pamoja nasi. Na kwa nguvu za kutakasa za Roho Mtakatifu kama mwenzi wetu wa kila wakati, twaweza daima kudumisha msamaha wa dhambi zetu.”7
Ninashuhudia kuhusu baraka chungu nzima tunazoweza kupata tunapozidi kujiandaa na kushiriki kiroho katika ibada ya sakramenti. Zaidi ninashuhudia kwamba baraka hizi zinapatikana kwetu sisi kwa sababu ya upendo wa Baba yetu wa Mbinguni na dhabihu isiyo na kikomo ya upatanisho ya Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo. Katika jina lake takatifu, hata Yesu Kristo, amina.