Yasiyo Haki Yenye Kughadhabisha
Yesu Kristo anaelewa ukosefu wa haki na ana uwezo wa kutoa tiba.
Mnamo mwaka 1994, mauaji ya kimbari yalifanyika huko Afrika Mashariki katika nchi ya Rwanda ambayo kwa sehemu yalisababishwa na mgogoro wa kikabila wa muda mrefu. Makadirio ni kwamba zaidi ya watu nusu milioni waliuawa.1 La kusifika ni kwamba, watu wa Rwanda, kwa sehemu kubwa wamepatana,2 lakini matukio haya yanaendelea kufanya mwangwi tena na tena.
Muongo mmoja uliopita, wakati nikizuru Rwanda, mimi na mke wangu tulikuwa na mazungumzo na abiria mwingine katika uwanja wa ndege wa Kigali. Yeye alilalamikia kukosekana kwa haki ya mauaji yale ya kimbari na kwa uchungu aliuliza, “kama kungelikuwa na Mungu, asingelifanya kitu kuhusu jambo hilo?” Kwa mtu huyu—na kwa wengi wetu—mateso na ukatili yasiyo haki huonekana kutoakisi uhalisia wa wema, wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Lakini bado Yeye ni halisi, mwema, na anampenda kila mmoja wa watoto Wake kwa ukamilifu. Uelewa huu wa kukinzana kuhusu Mungu ni wa kale kama vile mwanadamu na hauwezi kuelezeka kwa njia rahisi ya sauti tu au kwenye stika ya bampa.
Ili kuanza kutengeneza maana yake, acha tuchunguze aina kadhaa za kukosekana kwa haki. Fikiria juu ya familia ambayo kila mtoto anapokea fedha ya matumizi ya kila wiki kwa kufanya kazi za kawaida za nyumbani. Mtoto mmoja wa kiume, John alinunua pipi; binti mmoja, Anna, aliweka akiba fedha yake. Hatimaye, Anna alinunua baiskeli. John aliona siyo haki kabisa kwamba Anna alipata baiskeli wakati yeye hakupata. Lakini ni uchaguzi wa John uliotengeneza ukosefu ule wa usawa, siyo matendo ya wazazi. Uamuzi wa Anna wa kushinda hamu ya muda ya kula pipi haukuweka ukosefu wowote wa usawa kwa John kwa sababu alipata fursa ile ile kama ya dada yake.
Maamuzi yetu vile vile yanaweza kutuletea heri au hasara ya muda mrefu. Kama Bwana alivyofunua, “Kama mtu anapata maarifa na akili katika maisha haya kwa njia ya juhudi yake na utii kuliko mwingine, yeye atakuwa na heri ya juu zaidi katika ulimwengu ujao.”3 Wakati wengine wanapata faida kwa sababu ya chaguzi zao za bidii, hatuwezi kwa haki kuhitimisha kuwa tumetendewa isivyo haki wakati tulikuwa na fursa sawa.
Mfano mwingine wa kukosekana kwa haki hutoka katika hali ya mke wangu, Ruth, aliyokabiliana nayo kama mtoto. Siku moja, Ruth aligundua kwamba mama yake alikuwa anampeleka dada yake mdogo, Merla, kununua viatu vipya. Ruth akanung’unika, “Mama, hiyo siyo haki! Merla akapata jozi mpya ya mwisho ya viatu.”
Mama yake Ruth akamuuliza, “Ruth, viatu vyako bado vinakutosha?”
Ruth akajibu, “Ndiyo, vinanitosha.”
Mama wa Ruth kisha akasema, “viatu vya Merla havimtoshi tena.”
Ruth alikubali kwamba kila mtoto katika familia anapaswa kuwa na viatu ambavyo vinamtosha. Ingawa Ruth angelipenda kuwa na viatu vipya, mtazamo wake wa kutendewa isivyo haki ulitoweka wakati alipoona hali ile kupitia macho ya mama yake.
Baadhi ya kukosekana kwa usawa hakuwezi kuelezeka; kukosekana kwa usawa kusikofafanuliwa kunaghadhabisha. Kukosekana kwa usawa kunakuja kutokana na kuishi na miili ambayo si mikamilifu, iliyoumia au yenye magonjwa. Maisha ya duniani kwa asili hayana usawa. Baadhi ya watu wanazaliwa katika utajiri, wengine hapana. Baadhi wana wazazi wenye upendo, wengine hapana. Wengine wanaishi miaka mingi, wengine michache. Na kadhalika na kadhalika na kadhalika. Baadhi ya watu wanafanya makosa yenye kuumiza hata pale wanapojaribu kufanya mema. Baadhi wanachagua kutoachana na kukosekana kwa usawa wakati wangeweza kufanya hivyo. Cha kuhuzunisha, baadhi ya watu hutumia haki yao ya kujiamulia waliyopewa na Mungu kuwaumiza wengine wakati ambapo kamwe hawakupaswa.
Aina tofauti za ukosefu wa haki zinaweza kuungana, kutengeneza sunami ya ukosefu wa haki uliokithiri. Kwa mfano, janga la ulimwengu la COVID-19, pasipo uwiano linawaathiri zaidi wale ambao tayari wana matatizo tofauti ya kiafya, wanaonyemelewa na hali ngumu. Moyo wangu unauma kwa ajili ya hao wanaokabiliwa na ukosefu wa haki wa jinsi hiyo, lakini natamka kwa uchungu wa moyo wangu wote kwamba Yesu Kristo anaelewa vyote ukosefu wa haki na anao uwezo wa kutoa tiba. Hakuna chochote kinachoweza kulinganishwa na ukosefu wa haki aliovumilia. Haikuwa haki Kwake kupitia maumivu na mateso yote ya mwanadamu. Haikuwa haki kwa Yeye kuteseka kwa ajili ya dhambi na makosa yangu na ya kwako. Lakini Yeye alichagua kufanya hivyo kwa sababu ya upendo Wake kwetu sisi na kwa Baba wa Mbinguni. Kwa ukamilifu kabisa anaelewa tunayoyapitia.4
Maandiko yanaandika kwamba Waisraeli wa kale walinung’unika kwamba Mungu alikuwa akiwatendea visivyo haki. Katika kujibu, Yehova aliwauliza, “Kwani mwanamke anaweza kusahau mtoto wake ambaye anamnyonyesha, kwamba asiwe na huruma kwa mwana wa tumbo lake?” Kadiri isivyokuwa kawaida kwamba mama mwenye upendo aweza kumsahau mtoto wake mchanga, Yehova alitamka kwamba upendo wake ni imara zaidi. Anasisitiza: “ Ndio, wanaweza kusahau, lakini sitakusahau. … Tazama, nimekuchora viganjani mwa mikono yangu; kuta zako daima ziko mbele yangu.”5 Kwa sababu Yesu Kristo alivumilia dhabihu ya kulipia dhambi, isiyo na mwisho, Yeye ana huruma kamilifu.6 Yeye daima anatutambua sisi na hali zetu.
Hapa duniani, tunaweza “kusonga kwa ujasiri” kwa Mwokozi na kupokea huruma Yake, uponyaji, na msaada.7 Hata wakati tunapoteseka isivyoelezeka, Mungu anaweza kutubariki katika njia rahisi, ya kawaida, na ya kipekee. Tunapojifunza kuzitambua baraka hizi, tumaini letu kwa Mungu litaongezeka. Katika umilele, Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo watamaliza kukosekana kote kwa haki. Tunaelewa kuwa sisi tunataka kujua, kwa namna gani na lini. Ni kwa namna gani Wao watafanya hivyo? Lini Watafanya hivyo? Kwa ufahamu wangu, Wao bado hawajafunua namna au lini.8 Kile ninachojua ni kwamba Wao watafanya hivyo.
Katika hali zisizo haki, moja ya kazi zetu ni kuamini kwamba “yote yasiyo haki kuhusu maisha yanaweza kufanywa sawa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.”9 Yesu Kristo aliushinda ulimwengu na “kufyonza” yote yasiyo haki. Kwa sababu yake Yeye, sisi tunaweza kuwa na amani katika ulimwengu huu na kufurahia.10 Kama tutamwachia Yeye, Yesu Kristo atayaweka wakfu hayo yasiyo haki kwa faida yetu.11 Yeye siyo tu atatufariji na kurejesha kile kilichopotea;12 Atatumia yale yasiyo haki kwa faida yetu. Inapokuja kwenye kwa namna gani na lini, tunahitaji kutambua na kukubali, kama alivyofanya Alma, “haijalishi; kwani Mungu anajua vitu hivi vyote; na ninatosheka kujua kwamba hii ndiyo hali.”13
Tunaweza kujaribu kuzuia maswali yetu kuhusu ni kwa namna gani na lini kwa ajili ya baadae na kufokasi katika kukuza imani yetu katika Yesu Kristo, kwamba Yeye anazo nguvu kufanya kila kitu kiwe sawa na anatamani kufanya hivyo.14 Kwa sisi kung’ang’ania katika kujua kwa namna gani au lini hakuna manufaa na hata hivyo, ni kukosa kuona mbali.15
Tunapokuza imani katika Yesu Kristo, tunapaswa pia kujitahidi kuwa kama Yeye. Kisha tunawatendea wengine kwa huruma na kujaribu kuondoa kukosekana haki pale tunapouona;16 tunaweza kujaribu kutengeneza mambo kuwa sawa ndani ya uwezo wetu. Ndiyo, Mwokozi alielekeza kwamba sisi “tunapaswa kujishughulisha kwa shauku katika kazi njema, na kufanya mambo mengi kwa hiari [yetu] wenyewe, na kutekeleza haki nyingi.”17
Mtu ambaye amekuwa anajishughulisha kwa shauku katika kupambana na ukosefu wa haki ni wakili Bryan Stevenson. Utendaji wake wa kisheria hapa Marekani umejikita katika kuwatetea watu wanaotuhumiwa kimakosa, kupinga adhabu kali na kutetea haki za msingi za binadamu. Miaka kadhaa iliyopita, Bwana Stevenson alimtetea mwanaume ambaye alikuwa ametuhumiwa kimakosa kwa kesi ya mauaji na akahukumiwa kuuawa. Bwana Stevenson aliomba msaada kutoka katika kanisa la yule mtu katika eneo lile, ingawa mwanaume yule hakuwa mwenye kushiriki kikamilifu katika kanisa lake na hadhi yake kushuka katika jumuiya kutokana na kujulikana sana kwa masuala ya kimapenzi nje ya ndoa.
Ili kuifanya jumuiya izingatie juu ya jambo lililokuwa muhimu hapa, Bwana Stevenson aliwazungumzia kuhusu mwanamke aliyetuhumiwa kwa kosa la uzinzi na kuletwa kwa Yesu. Washitaki wake walitaka apigwe mawe hadi kufa, lakini Yesu alisema, “Yeye asiye na dhambi … , na awe wa kwanza kumtupia jiwe.”18 Washitaki wa mwanamke yule wakatoweka. Yesu hakumhukumu mwanamke yule bali alimtaka asitende dhambi tena.19
Baada ya kuelezea hadithi hii, Bwana Stevenson aligundua kwamba kujihesabia haki, woga, na hasira vimesababisha hata Wakristo kuwavurumishia mawe watu wanaojikwaa. Kisha akasema, “Hatuwezi kuangalia tu yakitokea,” na akawahimiza waumini kuwa “wadakaji wa mawe.”20 Akina kaka na dada, kutorusha mawe ni hatua ya kwanza katika kuwatendea wengine kwa huruma. Hatua ya pili ni kujaribu kudaka mawe yanayorushwa na wengine.
Jinsi tunavyoshughulikia mazuri na mabaya ni sehemu ya mtihani wa maisha. Tutahukumiwa siyo sana kwa yale tunayosema lakini kwa namna gani tunawatendea wanyonge na wenye hali ngumu.21 Kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunatafuta kufuata mfano wa Mwokozi wa kuendelea kutenda mema.22 Tunaonyesha upendo wetu kwa jirani zetu kwa kupambana ili kuhakikisha utu kwa watoto wote wa Baba wa Mbinguni.
Tukiwa na mazuri na magumu yetu wenyewe akilini, kutafakari ni jambo la afya. Kwa John kuelewa kwa nini Anna alipata baiskeli ilikuwa ni swala la kufunuliwa. Kwa Ruth kuona hitaji la Merla la viatu kupitia macho ya mama yake ilikuwa ni kuangaziwa. Kujaribu kuona mambo kwa mtazamo wa milele kunaweza kufafanua mambo. Kadiri tunavyokuwa zaidi kama Mwokozi, tunakuza uwezo wa kuhisi wahisivyo wengine, uelewa, na hisani.
Ninarudi kwenye swali lililoulizwa na abiria mwenzetu huko Kigali ambaye alililia ukosefu wa haki wa mauaji ya kimbari ya Rwanda na kuuliza, “Kama kungelikuwepo na Mungu, asingelifanya chochote juu ya hilo?”
Pasipo kupunguza mateso yaliyosababishwa na mauaji haya ya kimbari, na baada ya kutambua uwezo wetu wa kutoelewa mateso ya jinsi hiyo, tulijibu kwamba Yesu Kristo amefanya kitu juu ya majanga yasiyo haki.23 Tulielezea kanuni nyingi za injili kuhusiana na Yesu Kristo na Urejesho wa Kanisa Lake.24
Baadaye, rafiki yetu aliuliza, akiwa na machozi machoni mwake, “Mnamaanisha kuna kitu ninachoweza kufanya kwa ajili ya marehemu wazazi wangu na mjomba wangu?”
Tukasema, “Ee, ndiyo!” Kisha tukashuhudia kwamba yote yasiyo haki kuhusu maisha yanaweza kuwekwa sawa kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo na kwamba kwa mamlaka Yake familia zinaweza kuunganishwa pamoja milele.
Tunapokabiliwa na yasiyo haki, tunaweza kujiweka wenyewe mbali na Mungu au tunaweza kusogea Kwake kwa ajili ya msaada na tegemeo. Kwa mfano, vita vya muda mrefu kati ya Wanefi na Walamani viliwaathiri watu kwa namna tofauti. Mormoni alisema kwamba “wengi wamefanywa kuwa na roho ngumu” hali wengine “walilainishwa kwa sababu ya mateso yao, mpaka kwamba walijinyenyekeza mbele ya Mungu.”25
Usiache ukosefu wa haki ukushupaze, au kuharibu imani yako kwa Mungu. Badala yake, mwombe Mungu msaada. Ongeza shukrani yako kwa ajili ya na utegemezi wako kwa Mwokozi. Badala ya kuwa na machungu, muache Yeye akusaidie kuwa bora.26 Mruhusu Yeye akusaidie kuvumilia, ili mateso yako “yamezwe katika furaha ya Kristo.”27 Ungana naye katika misheni Yake “kuponya waliovunjika moyo,”28 jitahidi kupambana na yasiyo haki, na uwe mdaka mawe.29
Ninashuhudia kwamba Mwokozi anaishi. Anaelewa yasiyo haki. Alama katika viganja vya mikono Yake daima humkumbusha juu yako wewe na hali zako. Anakuhudumia katika magumu yako yote. Kwa wale wanaomjia Yeye, taji la uzuri litakaa badala ya majivu ya kuomboleza; shangwe na furaha zitachukua nafasi ya huzuni na uchungu; shukrani na sherehe zitachukua nafasi ya kuvunjika moyo na kukata tamaa.30 Imani yako kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo zitalipwa kuliko unavyoweza kufikiria. Yote yasiyo haki—hususani ukosefu wa haki unaoghadhabisha—utawekwa wakfu kwa faida yako. Ninashuhudia hivyo katika jina la Yesu Kristo, amina.