Liahona
Hadithi ya Mafanikio ya Mmisionari: Miaka 60 ya Maandalizi
Julai 2024


“Hadithi ya Mafanikio ya Mmisionari: Miaka 60 ya Maandalizi,” Liahona, Julai 2024.

Hadithi ya Mafanikio ya Mmisionari: Miaka: 60 ya Maandalizi

Ni tukio la shangwe kiasi gani lilitokea kwangu kusikia kwamba mbegu ya injili iliyopandwa miaka mingi iliyopita ilizaa matunda.

Picha
Mbegu zikiwa ardhini na mmea unaokua ukiwa na matunda

Kielelezo na Carolyn Vibbert

Daima nimependa Mafundisho na Maagano 18:10: “Thamani ya nafsi ni kuu machoni pa Bwana.” Na wakati mwingine inachukua wengi wetu kufanya kazi kwa pamoja katika kushiriki ushuhuda ili kuzileta nafsi kwa Mwokozi (ona 2 Wakorintho 13:1).

Nilikumbushwa juu ya wazo hili zuri la kazi jumuishi ya umisionari nilipopokea barua pepe siku moja. Kaka aliyesema alikuwa kijana wa rais wa misheni huko Wichita, Kansas, alijiuliza kama mimi nilikuwa mke wa Robert Monson. Kaka aliendelea kusema alikuwa akimtafuta Mzee Monson ambaye alihudumu katika Misioni ya Central State mwaka 1959. Huyo alikuwa mume wangu.

Alinieleza kuhusu wazee vijana wawili ambao walishawishika hivi karibuni kuingia kwenye nyumba ya makazi. Walipiga hodi kwenye mlango wa kwanza na kumkuta mwanamke kikongwe ambaye aliwaalika kurudi siku iliyofuata. Walipanga muda.

Waliporejea kwenye miadi yao, waligundua kwamba dada huyu kikongwe alikuwa na kitabu cha zamani sana chenye vitabu vitatu kwa pamoja (Kitabu cha Mormoni, Mafundisho na Maagano, na Lulu ya Thamani Kuu) alichopewa na wamisionari mwaka 1959. Alikuwa amekisoma mara nyingi sana na alijua mafundisho yaliyomo ndani yake ni ya kweli. Hakuwa amejiunga na Kanisa wakati huo kwa sababu mume wake hakutaka ahudhurie Kanisani au kubatizwa. Mume wake amefariki dunia hivi karibuni, na alisali kwamba awapate wamisionari tena. Katika kitabu chake hicho kulikuwa na majina ya wamisionari hao wawili kutoka mwaka 1959: Robert Monson na Granade Curran, mume wangu na mwenzake.

Kwa wiki kadhaa zilizofuata, mwanamke huyo alijifunza kuhusu mpango wa wokovu na baraka za hekalu. Mwanawe alikuwa amefariki katika umri wa miaka 22 na alisisimka kujua uwezekano wa kuungana tena pamoja naye. Wamisionari walipomwalika kubatizwa, kwa shangwe alikubali mwaliko wao.

Wote wawili mume wangu na mwenzake, Mzee Curran, wamefariki dunia, lakini ninaweza kuwafikiria wakihudhuria ubatizo huu mzuri kutoka upande wa pili wa pazia.

Wakati kijana wa rais wa misheni akinisimulia hadithi hii, nilikumbushwa kwamba Mwokozi hamsahau yeyote kati yetu. Yeye daima yuko pamoja nasi kama tunamruhusu katika maisha yetu. Agano Jipya linasimulia hadithi ya Zakayo, aliyepanda juu ya mti wa mkuyu ili amwone Mwokozi (ona Luka 19:1–10). Hata akiwa juu ya mti, Zakayo alionwa na Mwokozi, ambaye alimwambia atakula nyumbani mwake. Vivyo hivyo, dada kikongwe alisali na kusubiri wamisionari wabishe hodi mlangoni mwake, na walifanya hivyo. Mwokozi anatujua sisi sote. “Kwa kuwa Mwana wa Mtu alikuja kutafuta na kuokoa [kile] kilichopotea” (Luka 19:10).

Seti mbili za wamisionari—moja zaidi ya miaka 60 iliyopita na halafu moja hivi karibuni zaidi—walimleta dada huyu kwa Yesu Kristo na kama malipo waliimarisha shuhuda zao wenyewe na kupata shangwe katika Bwana. Nimenyenyekezwa kwa kuwa mtazamaji katika hadithi hii, nikijihisi mwenye shangwe kwa wote waliohusika katika kumleta dada huyu kwa Mwokozi (ona Mafundisho na Maagano 18:15).

Mwandishi anaishi Utah, Marekani.

Chapisha