Liahona
Mwili Wako: Utunzaji wa Hiyo Zawadi Takatifu
Julai 2024


“Mwili Wako: Utunzaji wa Hiyo Zawadi Takatifu,” Liahona, Julai 2024.

Mwili Wako: Utunzaji wa Hiyo Zawadi Takatifu

Miili yetu ni zawadi kutoka kwa Mungu na ni mahekalu kwa ajili ya roho zetu, lakini inahitaji kujiongoza na nidhamu ili kuilisha na kuitunza ipasavyo.

Picha
mwanamume na mwanamke wakifanya mazoezi ya mwili ya kukimbia

Ni rahisi kuchukulia afya zetu nzuri kama kitu kisicho na maana—yaani, hadi soda 10 kwa siku, mtindo wa maisha ya kukaa tu, na ukosefu wa usingizi unatupata. Au pengine licha ya chaguzi zenye afya tunazozifanya, hitilafu ya kinasaba hutushughulikia bila ya kutarajia na changamoto za afya kutupiga.

Sisi sote tumepewa kiwango tofauti cha afya ya mwili ambacho hatuwezi kukidhibiti siku zote. Lakini kitu kimoja ni cha uhakika: Mpango wa Mungu unatuita tuboreshe kile ambacho tumepewa. Kufanya hivyo kunahitaji nidhamu na kujitolea sawa na vile tunavyohitaji ili kustawisha afya zetu za kiroho. Hiyo inamaanisha kudhibiti mazoea yetu ya asili ya kukaa badala ya kukimbia, kula pipi badala ya mboga, na kukesha badala ya kulala.

Tunapotafuta mwongozo wa kiungu ili kuboresha afya zetu za kimwili na tunapokuza nidhamu binafsi ya kudumisha hili, tutagundua uwezo mkubwa wa kumtumikia Mungu na kupata shangwe.

Mwili Wako ni Hekalu

Nafsi zinastawi wakati roho na mwili zinapotunzwa vizuri. “Roho na mwili ndiyo nafsi ya mwanadamu” (Mafundisho na Maagano 88:15). Akiunga mkono aya hii, Rais Russell M. Nelson alifundisha kwamba vyote viwili mwili na roho “vina umuhimu mkubwa. Mwilli wako ni uumbaji wa ajabu wa Mungu. Ni hekalu Lake na lako pia na ni lazima utendewe kwa heshima.”

Katika umri wa miaka 99 Rais Nelson anaendelea kutekeleza majukumu yake kama Rais wa Kanisa, wakati tukitambua kwamba wakati mwingine anatumia fimbo kwa ajili ya kupata uwiano na sasa anapendelea kutoa mahubiri ya mkutano mkuu akiwa amekaa. “Mara kwa mara, ninapata changamoto ndogo ya usawa wangu,” aliandika kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii mwezi Mei 2023. “Nadhani sipaswi kushangaa wakati vitu vidogo vinapoibuka kwani nakaribia kufikia karne. Kwa shukrani, moyo wangu ni mzuri, roho yangu ni imara kama ilivyo miguu yangu, na ubongo wangu bado unafanya kazi.”

Rais Nelson anafahamika kwa mazoezi yake makini ya kiafya na mtindo mzuri wa maisha. Siku zote amekuwa mtu mwembamba, amefanya bidii kubaki hivyo. Alifanya mazoezi mara kwa mara, akipendelea kuwa nje. Katika miaka yake ya 90, alikuwa akitoa theluji kwenye njia za nyumbani kwake mwenyewe na kwa majirani zake, akibiringisha mapipa ya uchafu kurudisha gerejini kwake na akifanya kazi ya kufeka uwanja. Hadi alipokuwa Rais wa Kanisa, alicheza mchezo wa kuteleza kwenye theluji mara kwa mara kadiri ratiba yake ilivyomruhusu.

Kukuza Nidhamu Binafsi

Tunajua mambo ya msingi ya afya nzuri ya kimwili:

  • Fanya mazoezi mara kwa mara.

  • Pata usingizi wa kutosha.

  • Kula mlo kamili.

  • Dumisha uzito wa kiafya.

  • Tawala msongo wa mawazo.

Ujanja hapa ni kuifanya miili yetu ifanye kile ambacho roho zetu zinajua kinapaswa kufanyika. Kulingana na Rais Nelson, moja ya mitihani ya duniani ni kutawala matamanio ya miili yetu kwa roho ambaye anakaa ndani yake.

“Shetani anajua nguvu ya matamanio yetu. Hivyo, anatujaribu tule vitu ambavyo hatupaswi kula, kunywa vitu ambavyo hatupaswi kunywa. …

“Hakika tunapojua asili yetu ya kiungu, tutataka kudhibiti aina hiyo ya matamanio. … Katika sala ya kila siku, kwa shukrani tutamtambua [Mungu] kama Muumba wetu na kumshukuru kwa uzuri wa hekalu letu la kimwili. Tutautunza na kuuthamini kama zawadi yetu binafsi kutoka kwa Mungu.”

Kukuza Shukrani na Kupata Shangwe katika Mwili ambao Mungu Alitupatia

Katika umri wa miaka 27 na kama mama wa watoto watatu, niligundulika nina ugonjwa wa baridi yabisi, mfumo wa kingamwili ambao unaharibu viungo vya mwili baada ya muda. Maisha yangu yalitoka nje ya udhibiti kimwili na kiakili. Nilimgeukia Mungu kwa usaidizi katika kupata ustahimilivu wa kiakili na afya bora ambayo mwanzo niliichukulia kama kitu ambacho si muhimu.

Nilitafuta usaidizi kutoka kwa wanasaikolojia kwa ajili ya wasiwasi wangu. Nilifanya kazi na mtaalamu wa viungo juu ya dawa gani za kunywa na tiba asilia vile vile. Sikukata tamaa. Baada ya miaka mingi na maumivu makali, afya yangu iliimarika kimwili na kiakili.

Ninakumbuka alasiri moja nikitembea umbali mrefu kwa burudani nikipita bahari ya maua pori kwenda ziwa la mlimani. Machozi yakitiririka usoni, nilimshukuru Mungu kwa baraka ya mwili wangu na uwezo wa kujiingiza katika shughuli niliyodhani kuwa nimeshaipoteza. Hakuna tiba kwa ajili ya hali yangu, na ugonjwa umechukua nafasi inayoonekana kwenye mwili wangu. Lakini matembezi ya mwendo mrefu kwa burudani na kufanya mazoezi vimekuwa ndiyo furaha yangu, na kamwe sichukulii afya yangu kwa urahisi.

Licha ya mapungufu ya mwili wangu, hivi karibuni nimehudumu misioni ya wakubwa pamoja na mume wangu huko Washington, Marekani (ambako ni kivutio cha utembeaji wa mwendo mrefu kwa ajili ya burudani!). Ninashukuru kwa kuweza kuhudumu katika maisha yangu yote karibia katika kila wito unaopatikana katika Kanisa.

Kama Rais Nelson alivyosema: “Na siku zote tushukuru kwa baraka ya ajabu ya mwili wa kupendeza, uumbaji mkubwa wa Baba yetu mpendwa wa Mbinguni. Kadiri mwili wetu ulivyo mzuri, wenyewe pekee siyo mwisho. Ni sehemu iliyo muhimu ya mpango mkuu wa Mungu wa furaha kwa ajili ya maendeleo yetu ya milele.”

Muhtasari

  1. Wakati wa kikao cha ukuhani cha mkutano mkuu, Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Wakati Yesu Kristo anapotutaka mimi na wewe ‘kutubu’ [ona Luka 13:3, 5], Anatualika kubadili akili zetu, ufahamu wetu, roho zetu—hata jinsi tunavyopumua. Anatuomba tubadili jinsi tunavyopenda, tunavyofikiri, tunavyotumikia, tunavyotumia muda wetu, tunavyowatendea wake zetu, tunavyowafunza watoto wetu na hata tunavyoitunza miili yetu” (“Tunaweza kufanya vyema na kuwa Bora zaidi,” Liahona, Mei 2019, 67; msisitizo umeongezwa).

  2. Russell M. Nelson, “Mwili Wako: Zawadi ya Kupendeza ya Kuthaminiwa,” Liahona, Aug. 2019, 52.

  3. Russell M. Nelson, Facebook, May 16, 2023, facebook.com/russell.m.nelson.

  4. Ona Sheri Dew, Insights from a Prophet’s Life: Russell M. Nelson (2019), 345–67.

  5. Russell M. Nelson, “Mwili Wako: Zawadi ya Kupendeza ya Kuthaminiwa,” 54.

  6. Russell M. Nelson, “Mwili Wako: Zawadi ya Kupendeza ya Kuthaminiwa,” 55.

Chapisha