“Maandalizi Mazuri kwa ajili ya Maisha,” Liahona, Julai 2024.
Maandalizi Mazuri kwa ajili ya Maisha
Kitu ambacho wavulana na wasichana wanajifuza kwenye misioni zao kitabariki maisha yao milele.
Tangu nilipokuwa mdogo, siku zote nilivutiwa na shauku ya wamisionari. Wakati mmoja wa mkutano wa sakramenti katika tawi langu dogo la Minas, huko Urugwai, mmisionari alitoa ushuhuda wake na kuelezea hisia zake kuhusu misioni. Maneno yake yalikaa akilini na moyoni mwangu.
“Siku moja,” nilijisemea mwenyewe, “Nitahudumu misioni.”
Wakati fulani baadaye, kama kuhani, nilipata fursa ya kuambatana na wamisionari kwenye somo. Ulikuwa ni uzoefu ambao sitausahau kuwa mmisionari katika umri wa miaka 16!
Nilipofikia umri wa miaka 18, vijana kadhaa kutoka katika tawi langu walirudi kutoka kwenye misioni zao, ikijumuisha Dada Ana, ambaye alikuwa amerudi kutoka kwenye misioni yake huko Ajentina. Uzoefu wao na shuhuda zao pia viligusa moyo wangu.
Kumbukizi ya miaka 19 ya kuzaliwa kwangu ilipokaribia, nilitaka kutoa jina langu kwenda na kutangaza injili ya Mwokozi na kuhudumu katika shamba lake la mizabibu (ona Mafundisho na Maagano 75:2). Niliandaa na kutuma maombi yangu ya kwenda misioni. Wito wangu ulipofika, niliifungua barua iliyosainiwa na Rais Spencer W. Kimball na nilisoma kwamba ningehudumu katika Misioni ya Urugwai/Paragwai. Nilikuwa ninaenda kuhudumu katika nchi yangu. Nilifurahi kupata nafasi ya kutangaza “habari njema za shangwe kuu, hata injili isiyo na mwisho” (Mafundisho na Maagano 79:1).
Niliwasili katika ofisi ya misheni baada ya kusafiri kwa saa mbili kwa basi hadi Montevideo, Urugwai. Rais wa misheni alinisimika kama mmisionari wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na kunipatia mwenzangu. Jioni ile, tulianza kubisha hodi milangoni.
Mwanzoni, kuna nyakati misioni haikuwa ya kusisimua kama nilivyofikiri ingekuwa. Kwa shukrani, nilikuwa na mwenzi mtiifu na mwenye bidii ambaye alinisaidia kugundua shangwe ya kujipoteza katika huduma ya Bwana. Mfano wake umenibariki kipindi chote cha misioni yangu.
Lakini maandalizi yangu ya kuwa mwakilishi wa Mwokozi Yesu Kristo yalianza kitambo sana kabla.
Yote Yalianza na Kibanio cha Tai
Mnamo Januari 1962, nilipokuwa na umri wa miaka sita, wamisionari walifika katika duka la vito la baba yangu wakitafuta kurudishia kibanio cha tai ambacho mmoja wao alikuwa amepoteza. Wakiwa hapo, walimsikia mtu akipiga gitaa. Walipouliza kuhusu hilo, baba yangu akawaalika kuingia ndani na kukutana na rafiki yake.
Wakati wa maongezi yao, baba yangu na rafiki yake waliwauliza wale wamisionari kama walipiga gitaa. Mzee mmoja alisema aliweza kidogo. Rafiki wa baba alimpa gitaa na akamwomba apige. Akaanza kupiga baadhi ya nyimbo wakati mwenzake akiimba.
Utafutaji wa wamisionari wa kibanio cha tai uliwaongoza kwa familia ya baba yangu kutambulishwa kwenye injili ya Yesu Kristo. Tukawa marafiki wazuri na wale wamisionari na kuanza kusikiliza masomo. Mbegu ya injili ikapandwa, na ikaanza kukua, kwanza kwa mama yangu, Elsa, na dada zangu, Ana na Stella, na kisha kwangu.
Kuanzia siku ile, mapenzi kwa kazi ya umisionari yamekua katika familia yangu. Nilihudumu misioni, wana wangu walihudumu misioni, na sasa wajukuu zetu wanaanza kujiandaa kwa ajili ya na kuhudumu misioni, wakitengeneza kizazi cha tatu cha wamisionari.
Siyo daima rahisi kuwa mmisionari. Inahitaji maandalizi kabla mvulana au msichana kuwa tayari kwenda katika eneo la misioni. Hapa ndio pale wazazi, familia na viongozi wa Kanisa wanaweza kuwa mifano mizuri na kufanya kazi kama timu kuwaandaa vijana kwenye umri mdogo.
Njia moja ya kuwasaidia wajiandae ni kushiriki nao ujuzi kwa vitendo. Ujuzi kama vile kuweka akiba ya fedha, kufua na kunyoosha nguo, kushona, kung’arisha viatu, kupika na kuzungumza na watu kutawasaidia katika misioni zao. Kushiriki katika seminari na chuo pia kunasaidia katika maandalizi hayo na kuongezea kwenye kile wanachojifunza nyumbani na katika akidi na madarasa.
Usaidizi wetu unapaswa kuendelea wakati wakiwa katika misioni zao. Inapendeza kusikia uzoefu wa kupendeza ambao wamisionari wetu wanao karibia kila siku. Tunaweza pia kuwa sehemu ya uzoefu huo kwa kuwafikia wale wanaowafundisha. Kwa mfano, mama wa mmoja wa wamisionari ambaye aliifundisha familia yetu aliwasiliana na mama yangu na akamwandikia kwa miaka mingi, akimsaidia mama kubaki katika njia ya agano.
Tunapowasaidia wamisionari wa baadaye wajiandae, tunapaswa kukumbuka kwamba kazi ya umisionari ni zaidi ya utamaduni Kanisani—ni mwaliko na amri kutoka kwa Bwana (ona Mathayo 28:19). Hapo mwanzo, Adamu na Hawa walifundishwa injili. Wao kisha walifundisha injili kwa watoto wao (ona Musa 5:6–12). “Na hivyo Injili ikaanza kuhubiriwa, kutoka mwanzo, ikitangazwa na malaika watakatifu waliotumwa kutoka katika uwepo wa Mungu” (Musa 5:58).
Kuhubiri huku kunaendelea sasa na jeshi la zaidi ya wamisionari 71,000. Lakini tunawahitaji zaidi, wengi zaidi, kwenye mstari wa mbele—jeshi la wamisionari na waumini.
Kitu Tunachoweza Kujifunza kwenye Misioni Zetu
Wakati nikiwa misioni, nilikuja kuzoea kazi za umisionari na kuanza kufikiri kwa kina zaidi kuhusu ujumbe wetu. Siku zote nilikuwa nikihisi kwamba injili ilikuwa ya kweli, lakini nilikuwa na hamu kubwa ya kujua kwamba ilikuwa ya kweli. Nilisali, nilifunga, nilijifunza, nilifanya kazi na kisha nikasubiri jibu.
Wakati wa somo siku moja, nilishiriki hadithi ya Joseph Smith ya Ono la Kwanza:
“Niliona nguzo ya mwanga juu ya kichwa changu, ambao ulikuwa ni mng’aro uliozidi mwangaza wa jua, ambao ulishuka taratibu hadi ukatua juu yangu. …
“Wakati mwanga ulipotua juu yangu niliwaona Viumbe wawili, ambao mng’aro na utukufu wao unapita maelezo yote, wakiwa wamesimama juu yangu angani. Mmoja wao akaniambia, akiniita mimi kwa jina langu na kusema, huku akimwonyesha yule mwingine—Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!” (Joseph Smith—Historia ya 1:16–17).
Katika wakati ule, niliweza kumhisi Roho Mtakatifu akinithibitishia kwamba kile nilichokuwa nikikifundisha kilikuwa cha kweli. Nabii Joseph Smith hakika alimwona Baba na Mwana, na Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu na, pamoja na Biblia, vinashuhudia juu ya Mwokozi. Hii ilileta amani nafsini mwangu. Hata baada ya miongo kadhaa, bado inaleta msisimko moyoni mwangu.
Misheni yangu ilikuwa ni kama kupata shahada ya uzamivu ya kiroho. Kitu ambacho wavulana na wasichana wanajifuza kwenye misioni zao kitabariki maisha yao milele. Miongoni mwa mambo mengi wanajifunza:
-
Jinsi ya kujifunza, kusali, kufundisha na kutumia kanuni za injili kila siku.
-
Jinsi ya kuishi na mwenzake kwa saa 24 kila siku.
-
Jinsi ya kutunza afya zao.
-
Jinsi ya Kupanga.
-
Jinsi ya kuboresha ujuzi wa uongozi.
-
Jinsi ya kuhusiana kwa usahihi na watu wengine.
-
Jinsi ya kutafuta, kusikiliza na kuongozwa na Roho Mtakatifu.
Wavulana na wasichana wanaohudumu misioni wataimarishwa na kuandaliwa kukabiliana na changamoto za maisha kadiri wanavyoendelea kutumia kile walichojifunza wakati wakiwa misioni
Leo Ndiyo Siku
Nabii wetu mpendwa Rais Russell M. Nelson, amefundisha:
“Hakujawahi kuwepo na kipindi katika historia ya ulimwengu ambapo maarifa ya Mwokozi wetu ni ya msingi na muhimu sana binafsi kwa kila nafsi ya mwanadamu kama sasa. Fikiria jinsi mapigano ya uharibifu ulimwenguni kote—na yale katika maisha yetu binafsi—yatakavyotatuliwa kwa haraka kama sisi sote tukichagua kumfuata Yesu Kristo na kutii mafundisho Yake.”
Leo ndiyo siku ya sisi kuonyesha kwa vitendo na ujasiri na kushiriki injili ya Yesu Kristo. Leo ndiyo ile siku ya vijana wetu kujiandaa kuhudumu katika jeshi la Bwana kwenye misioni ya kufundisha au ya huduma. Ulimwengu unakuhitaji wewe! Kuna magoti ya kuimarisha, mikono ya kunyoosha na ukweli wa kuhubiriwa (ona Mafundisho na Maagano 81:5).
Na mwaliko unaofuata kutoka kwa Bwana utupeleke kwenye vitendo na kupandisha bendera ya ukweli kwa nguvu:
“Tazama, ninawaambia, ni mapenzi yangu kuwa ninyi muende …
“Mkipaza sauti zenu kama tarumbeta, mkitangaza ukweli kulingana na mafunuo na amri ambazo nimewapa.
“Na hivyo, endapo mtakuwa waaminifu … mtavikwa heshima, na utukufu, na kutokufa, na uzima wa milele” (Mafundisho na Maagano 75:3–5).