Liahona
Tunaweza Kusali Juu ya Nini?
Julai 2024


“Tunaweza Kusali Juu ya Nini?,” Liahona, Julai 2024.

Njoo, Unifuate

Alma 33-34

Tunaweza Kusali Juu ya Nini?

Katika Alma 33 na 34, tunafundishwa kwamba tunaweza kusali popote, wakati wowote, na juu ya chochote. Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya watu mbalimbali wakisali katika hali tofauti.

Unaposoma matukio haya, fikiria baadhi ya njia ambazo kwazo wewe umesali “juu ya mifugo katika shamba lenu” na katika vijumba vyenu, na mahali penu pa siri, na kwenye nyika zenu” (Alma 34:25, 26).

Picha
mtu amesimama katika mavazi ya wanariadha

Mtakatifu wa Siku za Mwisho Alma Richards alishinda katika michezo ya Olimpiki ya mwaka1912.

Kusali kwenye michezo ya Olimpiki

Mrukaji wa juu, Alma Richards alikuwa sehemu ya timu ya michezo ya mbio za Olimpiki ya mwaka 1912 iliyomalizika huko Stockholm, Sweden. Wakati wa mashindano, wengine waliondolewa mmoja mmoja hadi Alma na mwingine mmoja wakabakia.

“Alma alipojiandaa kuruka, akili yake ilikwenda kasi. Alikuwepo pale, akiiwakilisha nchi yake kwenye mashindano makubwa ya riadha ulimwenguni. Lakini bado alijihisi mnyonge, kana kwamba ulimwengu wote ulikuwa umelala mabegani mwake. Alifikiria juu ya Utah, familia yake na mji wake wa nyumbani. Alifikiria juu ya BYU na Watakatifu. Akiinamisha kichwa chake, kimya kimya alimwomba Mungu ampe nguvu. ‘Kama ni sahihi kwamba ninapaswa kushinda,’ alisali, ‘nitafanya niwezalo kuweka mfano mwema siku zote za maisha yangu.’”

Akichota nguvu kutoka kwa Bwana, Alma aliruka na kufikia kiwango cha juu zaidi. Mshindani wake aliyebaki aliposhindwa, Alma alishinda medali ya dhahabu.

Picha
mwanamume akiruka juu ya ufito katika tukio la riadha.

Baadaye, rafiki “alimtania kuhusu kusali kabla ya kushinda kwenye kuruka. ‘Natamani usingecheka,’ Alma kimya kimya alijibu. ‘Nilisali kwa Bwana anipe nguvu ya kuruka juu ya kile kiwango, na nilivuka.’”

Kusali kwenye Kona ya Mtaa

Mnamo mwaka 1898, Inez Knight na Jennie Brimhall walikuwa wanawake waseja wawili wa kwanza kuitwa kuwa wamisionari kwa ajili ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Muda mfupi baada ya kuwasili kwenye misioni zao huko Uingereza, wanawake hawa wawili walienda kuhubiri huko Oldham, mji mdogo wa viwanda karibu na Liverpool.

Picha
akina dada wawili wamisionari

Inez Knight na Jennie Brimhall walisali kwa ajili ya msaada katika huduma yao ya kimisionari huko Uingereza.

Kulia: picha kwa hisani ya Jennifer Whatcott Hooton

Akina dada wawili, rais wao wa misheni, na wamisionari wengine walikusanyika pamoja jioni moja. “Walitengeneza mduara kwenye kona ya mtaa wenye shughuli nyingi, wakatoa sala, na wakaimba nyimbo hadi umati mkubwa ulipojitengeneza kuwazunguka.” Juhudi zao zilikuwa na mafaniko kiasi kwamba rais wa misheni “alitangaza kwamba mkutano maalumu ungefanyika siku iliyofuata, na akamwalika kila mtu kuja na kusikia mahubiri mubashara kutoka kwa ‘wanawake halisi wa Kimormoni.’”

Kusali kwa ajili ya Usafiri

Sahr kutoka Bo, Sierra Leone, alisafiri kwa pikipiki kwenda eneo la vijijini kupeleka dawa iliyohitajika sana kwa wazazi wake wazee. Alikawia kurudi mjini kuliko alivyopanga ili kuwasaidia wazazi wake kukarabati paa lao, ambalo lilikuwa limeharibiwa na kimbunga. Wakati lilipokuwa limerekebishwa, jioni ikawa imeingia.

Kwa sababu ya saa za jioni, ilikuwa dhahiri teksi haingeweza kuja. Sahr akawa mwenye wasiwasi. Bila teksi, alikabiliwa na safari ya kutembea ambayo siyo tu ingekuwa ndefu bali pia uwezekano wa kuwa yenye hatari. Kubaki nyumbani kwa wazazi wake halikuwa chaguo sahihi kwa sababu alikuwa na zamu ya kuwa kazini mapema asubuhi iliyofuata. Kwa nyongeza, hakutaka kuiacha familia yake changa peke yao usiku.

Kusali kwa ajili ya pikipiki kulionekana kama kitu cha ajabu, lakini Sahr alisali kwa Mungu amsaidie kufika nyumbani. Dakika kadhaa baadaye, pikipiki ilikuja, baada tu ya kumshusha mtu katika eneo lile ambalo kwa kawaida ni eneo la ukimya. Sahr kwa shukrani alipanda, akihisi kubarikiwa kwamba angeweza kufika nyumbani mapema ili kutimiza ahadi yake ya kuwahi kazini na kuilinda familia yake.

Kusali kwa ajili ya Mabadiliko ya Ratiba

Kaka Miguel Troncoso kutoka Santa Cruz, Argentina, alikuwa akitazamia kumsikiliza Mzee Carlos H. Amado wa Sabini akizungumza katika kigingi chake. Lakini Mzee Amado alikuwa amepangiwa kuzungumza Jumanne jioni, na Kaka Troncoso, mwalimu wa shule ya upili, alipaswa kufundisha darasa usiku ule. Akiwa ameazimia kuhudhuria mkutano ule, yeye na familia yake walisali kwa ajili ya msaada.

Kaka Troncoso alisema hivi kuhusu uzoefu wake:

“Siku moja kabla ya mkutano, nilihisi kushawishika kuzungumza na mwalimu mkuu kuhusu kuondoka dakika 20 kabla. … Kabla sijasema neno, aliniuliza kama ningeweza kubadili ratiba ya darasa langu siku ya Jumanne kwa kuanza masaa mawili kabla ya muda wa kawaida. …

“Ilikuwa baraka iliyoje kwetu. Tulifika kwenye mkutano mapema sana na tulimhisi Roho katika uwepo wa mmoja wa wanafunzi wa Bwana. … Kwa nyongeza, tulipata ushuhuda kama familia kwamba Baba wa Mbinguni anajua matamanio yetu na anasikiliza sala zetu.”

Muhtasari

  1. Ona Saints: The Story of the Church of Jesus Christ in the Latter Days, vol. 3, Boldly, Nobly, and Independent, 1893–1955 (2022), 156–59. Maelezo zaidi kuhusu uzoefu wake yanaweza kupatikana katika “Alma Richards: 1912 Olympian” (makala ya kidijitali), Liahona, Jan. 2022, Maktaba ya Injili.

  2. Ona Saints, 3:63–64.

  3. Miguel Troncoso, “We Turned to Prayer,” Liahona, Machi. 2011, 69.

Chapisha