Liahona
Ningewezaje Kumtumaini Baba wa Mbinguni Wakati Nilipohisi Nimesimama Peke Yangu?
Julai 2024


“Ningewezaje Kumtumaini Baba wa Mbinguni Wakati Nilipohisi Nimesimama Peke Yangu?,” Liahona, Julai 2024.

Vijana Wakubwa

Ningewezaje Kumtumaini Baba wa Mbinguni Wakati Nilipohisi Nimesimama Peke Yangu?

Nilikuwa najaribu kuwa na imani lakini niliendelea kukabiliana na changamoto nyingi. Je, ninawezaje kuendelea kumtumaini Bwana?

msichana mkubwa amekaa na anaonekana amezama katika mawazo

Vielelezo na Kathleen Peterson

Binamu zangu walinitambulisha kwa wamisionari nilipokuwa na umri wa miaka tisa. Nilijiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lakini nilikuwa muumini pekee katika familia. Tangu hapo, nimejifunza kupenda injili ya Yesu Kristo zaidi na zaidi. Hata hivyo, kwa wakati fulani, kutumaini katika Baba wa Mbinguni na ukweli Wake ilikuwa vigumu sana kwangu, na hakika nilipambana ili kusonga mbele kwa imani.

Kuishi tofauti na ulimwengu kama mwanafunzi wa Yesu Kristo inaweza kuwa vigumu mahali popote, lakini kukulia Hong Kong kama muumini wa Kanisa ilikuwa changamoto zaidi kuliko ambavyo wengine wangetarajia.

Sababu moja, ni kwamba watu wengi katika eneo hili hawalipendi Kanisa na wanafikiri linahusiana na mambo mabaya. Mwanzoni neno la Kichina lililotumika kwa ajili ya “Mormoni,” likirejelea Kanisa, lilijumuisha sauti ambayo ilihusisha sauti hiyo na neno la Kichina “ibilisi.” Kwa baadhi, hii ilitengeneza mtazamo hasi juu ya maadili ya Kanisa.

Pia, kwa sababu kuna dini zingine nyingi za kitamaduni tayari zimeenea na waumini wa Kanisa ni wachache katika Hong Kong, inaweza kuwa rahisi kuhisi upweke au kutengwa. Watu wengi wanajiuliza maswali kuhusu Kanisa, bila kuelewa kwa ukamilifu mafundisho yake na hawako tayari kusikiliza kile waumini wanachotaka kushiriki.

Nilihisi athari za vizuizi hivi zaidi nilipokuwa kijana, lakini kupitia uzoefu huo, nilijifunza mengi kuhusu kile inachomaanisha kumtumainia Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.

Je, Kuishi Injili Kulikuwa na Thamani?

Katika shule ya upili, wazazi wangu walikuwa marafiki na mmoja wa walimu wangu. Mwalimu huyu alikuwa Mkristo katika dhehebu jingine. Wakati huo nilikuwa muumini pekee wa Kanisa katika darasa langu, na wanadarasa wenzangu wengi na walimu tayari walikuwa wanakisia mambo kuhusu Kanisa la Yesu Kristo na waumini wake.

Mwalimu huyu alikuwa na maoni hasi ya nguvu sana kuhusu imani yangu, ambayo yalifanya mambo kuwa magumu sana kwa sababu alikuwa rafiki wa familia.

Moja, mara nyingi nilikuwa mtu mwenye usingizi katika darasa lake kwa sababu nilikuwa ninaamka mapema sana ili kwenda kwenye darasa la seminari alfajiri, kitu ambacho kilimfanya awe na mashaka kwamba nitarudi nyuma katika kazi zangu za shule. Pia yeye aliniweka kikaangoni na kunipa changamoto ya maswali magumu ya kimafundisho ambayo sikujua jinsi ya kuyajibu. Hata alinipa kazi za shule za kusoma maandishi ya wapinga–Kanisa! Alijaribu kwa bidii sana kunishawishi kukaa mbali na imani yangu.

Huu ulikuwa wakati wa changamoto kwenye imani yangu. Kwa nini, wakati nilipokuwa najaribu kukaa karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, kubaki mwaminifu kulisababisha changamoto na ugumu katika maisha yangu? Je, sikuwa napaswa kubarikiwa kwa kushika amri na kutoa dhabihu ya usingizi kwa kwenda seminari?

Badala yake, alama zangu za ufauli zilikuwa zinashuka, imani yangu ilikuwa inatindika, na uhusiano wangu na walimu wangu, familia yangu na Baba wa Mbinguni ulikuwa unaathirika

Kwa muda, nilianza kujiuliza kama kuishi injili kulikuwa na thamani. Nilianza kuacha kwenda seminari na punde nilihisi imani yangu inafifia. Ilionekana ni rahisi kukubali tu kile ambacho ulimwengu ulionizunguka ulinilazimisha nifanye.

Kuchagua Kutumaini

Niliendelea kusali kwa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya mwongozo na uelewa. Licha ya mkanganyiko wa kina na hasira ambayo nilihisi kuhusu hali yangu, kitu fulani katika moyo wangu kiliendelea kushikilia kwenye imani. Nilizungumza na marafiki waaminifu na niliwaambia siri hii vijana wa rika yangu kutoka Kanisani kuhusu kile nilichokuwa napitia na nilitiwa moyo kuzungumza na mwalimu wangu wa seminari kuhusu mapambano yangu.

Alinijibu kwa huruma na kunitia moyo wa kuendelea kuhudhuria seminari kwa moyo wenye matumaini. Aliniahidi kwamba nitaona baraka zikifunguka kama nitaendelea kushikilia kwenye imani na kumtumainia kwamba Bwana ana baraka nyingi alizoweka kwa ajili yangu na ataziweka wakfu changamoto zangu (ona 2 Nefi 2:1–2).

Hivyo, licha ya changamoto hizo nilizokabiliana nazo, nilichagua kutumaini.

msichana mkubwa akitabasamu

Baada ya muda, nilianza kuhisi mtazamo wangu ukibadilika. Badala ya kufokasi juu ya magumu niliyokuwa nakabiliana nayo, nilifokasi juu ya shukrani niliyoiona kwa ajili ya injili. Nilianza kufokasi juu ya baraka za familia yangu, utambulisho wangu wa kiungu na ukweli wa milele juu ya injili. Na mwishowe, nilifikia kujua kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanajua hali zangu na siku zote walisimama pamoja nami katika nyakati hizo nilizohisi kana kwamba nimesimama peke yangu.

Hii ilibadilisha kila kitu.

Nilipoendelea kuweka matumaini yangu Kwao, kushika amri, kutubu kila siku na kufanya yale mambo madogo madogo kila siku ya kuunganika Nao, nilihisi msingi wangu wa imani ukiota mizizi na kuimarika.

Rais Russell M. Nelson hivi karibuni alisema: “Simamia ushuhuda wako wewe mwenyewe juu ya Yesu Kristo na injili Yake. Utafute. Utunze ili ukue. Ulishe ukweli. Usiuchafue kwa falsafa za uongo za wanaume na wanawake wasioamini. Unapofanya uimarishaji endelevu wa ushuhuda wako juu ya Yesu Kristo kuwa kipaumbele chako cha juu zaidi, tazamia miujiza kutokea katika maisha yako.

Na nilipofanya hivyo, muujiza ulitokea.

Kile Inachomaanisha Kumtumaini Bwana

Baada ya kuepuka kila mazungumzo kuhusu imani na mwalimu wangu kwa muda, siku moja aliponikaribia akiwa na maswali, nilihisi kuwa tayari kuyajibu nikiwa na imani iliyofanywa upya. Kwa ukarimu nilimwuliza kama amewahi kuhudhuria moja ya mikutano ya kanisa letu au kusoma Kitabu cha Mormoni. Aliposema hapana, nilihisi kushawishika kutoa ushuhuda wangu juu ya kweli rahisi.

Nilimwambia kwamba kamwe huwezi kujua kama kitu fulani ni cha kweli pasipo kupata uzoefu wake au kufanya uchunguzi kwa ajili ya majibu wewe mwenyewe. Nilimweleza kwamba mimi najua injili ni ya kweli kwa sababu nimefanya kazi kupata majibu na kuhisi katika moyo wangu kwamba ilikuwa ya kweli. Nilimwalika afanye vivyo hivyo, na kuanzia hapo na kuendelea, uhusiano wetu ukawa wa amani zaidi.

Changamoto hii ya imani niliyokuwa nayo kama kijana hakika iliniandaa kwa ajili ya maisha ya usoni kama mfuasi wa Kristo. Nimeona baraka nyingi sana na ahadi zikija kuzaa matunda kadiri nilivyoendelea kumtumainia Bwana zaidi ya maoni ya mtu mwingine yeyote. Kama vile Nefi alivyoeleza, “Ewe Bwana, nimekuamini, na nitakuamini milele. Sitaweka matumaini yangu kwenye mkono wa mwanadamu” (2 Nefi 4:34).

Mambo yanapokuwa hayaendi kama yalivyopangwa au tunapokabiliana na magumu tusiyoyatarajia, inaweza kuwa rahisi kuhisi kama Baba wa Mbinguni ametuongoza vibaya, ametuacha au hajali.

Lakini hiyo si kweli.

Ukweli ni kwamba, siku zote ni katika nyakati hizo za changamoto za kukanganya na kuvunja moyo kwamba ninakumbushwa kile inachomaanisha kuweka kikamilifu tumaini langu katika Bwana. Lazima niruhusu ufuasi wangu na imani yangu kuwa na maana na vyenye kubadili maisha badala ya kuwa ya kiroboti na kimazoea. Rais Nelson pia alifundisha, “Imani yako yenye kustawi itakusaidia ugeuze changamoto kuwa ukuaji na fursa zisizo kifani.”

Ninaweza kuona jinsi gani kuchagua imani katika Yesu Kristo kumenibariki katika njia nyingi zaidi kuliko nilivyofikiria inawezekana. Hii haimaanishi kwamba siku zote nitaepuka huzuni, magumu au mkanganyiko, lakini inamaanisha kwamba ninajua wapi pa kugeukia kwa ajili ya amani na utulivu.

Rais Nelson kwa upendo anatukumbusha, “Tafadhali jua hili: kama kila kitu na kila mtu mwingine katika ulimwengu ambaye unamwamini atashindwa, Yesu Kristo na Kanisa Lake kamwe hawatashindwa.”

Lolote unalokabiliwa nalo katika maisha yako, iwe matarajio yasiyofikiwa, mashinikizo kutokana na sauti za ulimwengu, matatizo ya kifamilia, mapambano ya afya ya akili, kuyumba kifedha, kuvunjika moyo, maamuzi yasiyo haki au changamoto nyingine yoyote. ningekualika kuendelea kuweka matumaini yako katika Bwana. Yeye kwa ukamilifu anafahamu hali zako. Yeye anakujua. Ana baraka za kupendeza ghalani kwa ajili yako. Hata katika nyakati zile unapokuwa hutaki kumtumainia Yeye, chagua tu kufanya hivyo. Ahadi Zake ni za uhakika. Yeye atakuongoza kwenye shangwe, tumaini na miujiza katika wakati muafaka.

Anafanya hivyo kwangu ninapoendelea kumtumaini Yeye.