Liahona
Mungu Alinionyesha kuwa Nilikuwa na Dhumuni
Julai 2024


“Mungu Alinionyesha Kuwa Nilikuwa na Dhumuni,” Liahona, July 2024.

Taswira za Imani

Mungu Alinionyesha kuwa Nilikuwa na Dhumuni

Nilianguka kutoka juu ya mti, lakini Bwana aliniokoa ili niweze kuyageuza maisha yangu na kuwasaidia watu wenye ulemavu kama wangu.

mwanamume katika kiti mwendo akiwa na familia yake

Picha na Christine Hair

Nilikuwa nikihudhuria mkutano wa dini pamoja na dada yangu wakati aliponitaka nipande mti na kuangua kicha cha nazi kwa ajili ya mkutano ule. Nilipokuwa natoa zile nazi kwenye kilele cha mti, ghafla nilipoteza fahamu na kuanguka. Niliangukia vibaya mgongo wangu na sikuweza tena kuihisi miguu yangu.

Nilipelekwa hospitali, ambapo madaktari waliiweka sawa mifupa ya mgongo wangu. Kwa miezi mitatu, nililalia mgongo wangu hospitalini, sikuweza kukaa. Huu ulikuwa wakati wa hisia kali na msongo wa mawazo. Ningelala tu hapo na kujiuliza itakuwaje kwangu na ningekuja kufanya nini baada ya hili.

Shauriana na Bwana

Baada ya miezi mitatu, niliambiwa nitaenda New Zealand kwa ajili ya upasuaji wa mgongo wangu. Upasuaji ulifanyika ili niweze kukaa badala ya kulala tu. Wakati nikiwa hospitali huko New Zealand, nilikutana na msichana ambaye alikuwa akifanya kazi hapo. Aliniuliza, “Ninakufahamu? Unaonekana si mgeni kwangu.”

Tulianza kuongea. Alishiriki nami injili ya Yesu Kristo na alinipatia Kitabu cha Mormoni. Mwanzoni, sikukisoma. Nilikiacha bila kukigusa pembeni ya kitanda changu. Siku moja, hata hivyo, nilikuwa peke yangu na hapakuwa na kitu chochote cha kupendeza kuangalia kwenya runinga. Kisha nikakiona kile Kitabu cha Mormoni juu ya meza yangu. Nilikifungua na kuanza kukisoma na kusoma.

Nilipokuwa ninakisoma, nilipata hisia kuwa kulikuwa na kitu fulani tofauti kuhusu Kitabu cha Mormoni na kwamba ni lazima kina injili ya kweli ya Yesu Kristo. Yule msichana pale hospitali aliwekea alama aya kadhaa, moja ya hizo ilikuwa Alma 37:37: “Shauriana na Bwana kwenye matendo yako yote, na atakuongoza kwa yale mema.”

Maneno yale yaliruka na kunifanya nifikirie. Ili kujua kama Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ndilo Kanisa la Kweli, nilijua nilihitaji kushauriana na Bwana. Pia nilitaka kwenda kuliona kanisa hili mimi mwenyewe.

Kutokuwa Kwangu na Tumaini Kumeondoshwa Mbali

Nilipofika nyumbani kutoka New Zealand, niliwaalika wamisionari kunifundisha. Kadiri nilivyoendelea kujifunza, nilipata ushuhuda kwamba hili ni Kanisa la Kristo. Nina shukrani kwa wamisionari walionifundisha. Kwenye ubatizo wangu, walipata nguvu za kunibeba na kuniingaza ndani ya maji—mmoja akinishika katika mikono yake wakati mwingine akifanya ubatizo wangu.

Kwa ubatizo wangu, hisia zote za msongo wa mawazo na kutokuwa na tumaini nilizokuwa navumilia ziliondoshwa mbali. Nilijua nilikuwa na dhumuni katika maisha na kwamba Mungu alinipenda.

Kabla sijabatizwa, nilihisi aibu kuhusu mimi mwenyewe kwa sababu ya kiti mwendo changu. Baada ya kuwa nimebatizwa, hata hivyo, nilianza kuja kwenye kata kila Jumapili na kushiriki katika shughuli za vijana wakubwa. Hata nilienda kwenye dansi za kigingi, nikicheza kwenye kiti mwendo changu kila wimbo. Pia nilijiunga na mtandao wa Wasamoa wenye madhara ya uti wa mgongo.

Nilitambua kwamba nilikuwa nimeponywa kutokana na hisia ambazo nilihitaji kuzificha. Kupitia Kanisa, nilipata kujiamini kwenda miongoni mwa watu tena.

Bwana pia alinisaidia niweke malengo makubwa na nikue wakati nilipotiwa moyo kuhudhuria programu ya miaka mitatu kwenye Shule ya Kambodia ya Prosthetics na Orthotics (CSPO). Sikuwa na uhakika ningeweza kujiunga na programu hii kwa sababu hakuna mtu aliye katika kitimwendo aliyeomba kujiunga. Hata hivyo, hali mwishowe iliniruhusu kuweza kuhudhuria hiyo CSPO huko Kambodia. Nilihitimu huko kama mwanafunzi wa kwanza mwenye ulemavu katika historia ya programu hiyo.

mwanamume akiwa ameshika mkono bandia

Kabla hajabatizwa, Posenai alihisi aibu kuwa katika kitimwendo. Lakini baada ya ubatizo wake, anasema, “nilipata kujiamini kwenda miongoni mwa watu tena.”

Baada ya kurejea Samoa, nilizungumza kwenye ibada ya VWW kuhusu afya. Baada ya mkutano, mwanamke mmoja alinifuata kunishika mkono na kuniambia alipenda mazungumzo yale. Lagimanofia alikuwa amerejea punde kutoka katika misioni yake. Kutoka muda ule nilipokutana naye, nilihisi kwamba yeye ananikamilisha mimi. Nilikuwa nikisali ili kumpata mtu ambaye angekuwa mwenza wangu na ambaye angenipenda na kunikubali.

Wakati Lagimanofia na mimi tulipoanza miadi, alinitunza na kunikubali, na familia yake ilisaidia. Tulioana, na maisha yetu yalibadilika milele tulipomuasili Posenai Mdogo. Mungu alituandaa ili tumuasili. Kuwa na yeye katika maisha yetu kumetufanya tuwe na furaha sana.

Je, ninaweza Kuhudumu?

Kanisani, niliitwa kama karani wa kata na baadae kama mshauri katika uaskofu. Sikuweza kuamini kwamba mtu aliye katika kitimwendo angeweza kuhudumu. Ajali yangu ilinifanya nihisi kutokuweza, lakini kufanya kazi Kanisani kulinifanya nihisi mwenye kuhitajika na ilinisaidia nitambue kwamba ningeweza kuchangia. Ninapenda fursa ya kuwa karibu zaidi na Yesu Kristo pale ninapohudumu.

Kama mshauri katika uaskofu, nilitaka kuongozwa ili niweze kuwa bora kwenye wito wangu. Hiyo ilinifanya nitake kujiandaa zaidi kwa ajili ya kila Jumapili. Niliingia katika tabia ya kujisomea maandiko yangu, na nilipata fursa za kutoa ushuhuda wangu. Kuwa kiongozi kanisani kulinisaidia pia kuwa kiongozi mahali pangu pa kazi. Nilijijengea hisia kwamba ningeweza kuongoza na kuzungumza, ikiniruhusu kuongoza katika maeneo mengine.

Sasa ninafanya kazi kama Mkuu wa Idara ya Mikono Bandia na Mifupa katika hospitali kuu ya Tupua Tamasese Meaole, Samoa. Idara yangu inawavalisha takribani watu 500 kwa mwaka vifaa vya msaada wa kutembea na vitimwendo. Kanisa, kupitia Wizara ya Afya ya Samoa, inasaidia kutoa vitimwendo vinavyohitajika na vifaa kwa ajili ya kutengeneza mikono bandia.(ona philanthropies.ChurchofJesusChrist.org/humanitarian-services). Misaada hii inawasaidia watu kurudi kufanya kazi na kuweza kujitegemea. Pia inawapa watu matumaini na njia ya kurudi katika maisha waliyofikiria wameyapoteza.

mwanaume kwenye kitimwendo akimsaidia mwanaume mwingine mwenye mguu wa bandia.

“Kufanya kazi Kanisani kulinifanya nijihisi mwenye umuhimu na kutambua kwamba ningeweza kuchangia,” anasema Posenai “Napenda fursa ya kuwa karibu zaidi na Yesu Kristo pale ninapohudumu.”

Mtegemee Bwana

Kama ningekuwa natoa ushauri kwa mtu mwingine mwenye ulemavu, ningesema, “Usiache ulemavu wako ukuzuie kufanya kile unachokiamini. Mimina moyo wako katika kile unachotaka kukipata na fanya bidii ukipate. Unapotafuta usaidizi wa Bwana, Yeye atakubariki [ona 2 Nefi 32:9].”

Kwa kuamini huko, ninaendelea kusonga, na inanifanya niwe jinsi nilivyo leo. Ninaamini, nimewekwa hapa na niliokolewa kwa madhumuni. Nilianguka kutoka juu ya mti, lakini Bwana aliniokoa ili niweze kuyageuza maisha yangu na kufanya kazi hii ambayo inawasaidia watu hawa wote. Bwana amenifundisha kwamba ninaweza kuwasaidia wengi—siyo licha ya ulemavu wangu bali kwa sababu hiyo.