“Kutoka Gizani Hadi kwenye Furaha,” Liahona, Julai 2024.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Kutoka Gizani Hadi kwenye Furaha
Nilipokuwa nikirudia maneno ya ibada za hekaluni akilini mwangu, kitu cha ajabu kikatokea.
Mnamo 1988, nilienda pamoja na walimu wengine wa Uingereza kufundisha shule huko Sudani. Watoto wale walikuwa wenye furaha, na sisi kwa haraka tukajizoeza mazingira magumu ya kuishi katika nchi inayoendelea. Mwajiri wetu, hata hivyo, aligeuka kuwa kiongozi mkandamizaji aliyemtesa mtu yeyote aliyemdhania kuwa mpinzani wake katika njia yoyote. Alinichukia kutoka siku ile niliposimama kumtetea mtu aliyemnyanyasa.
Siku moja aliniita ndani ya ofisi yake. Kwa zaidi ya nusu saa, alinitesa kwa namna zote za maneno ya unyanyasaji na vitisho. Niliondoka chumbani humo katika hali ya mshtuko. Sina kumbukumbu ya namna gani niliimaliza siku iliyosalia pale shuleni. Jioni yote sikuweza kuyatoa kichwani mwangu maneno yale ya kutisha.
Wakati wa kulala, nilikaa kitandani kwangu na kusoma maandiko. Kisha nilipiga magoti na kwa dhati nilisali kwa ajili ya faraja na msaada, lakini sikuhisi chochote. Nilipanda kitandani lakini sikuweza kulala. Zaidi ya mara mbili niliamka, kusoma, kupiga nagoti, na kusali, lakini bila mafanikio.
“Ee, ndiyo,” niliwaza, “Baba wa Mbinguni siyo daima anajibu sala zetu kwa namna na kwa wakati tunaotaka.” Nilijiachia kwenye usiku mchovu na usio na usingizi.
Lakini nilipolala tena, niliwaza, “Kuna kitu kimoja zaidi ninachoweza kufanya.” Nilianza kurudia mwenyewe maneno ya ibada za hekaluni akilini mwangu. Nilipofanya hili, muujiza wa ajabu ulitokea. Vyote, huzuni na giza vilitoweka kwangu, na amani ya ajabu na shangwe zaidi vikaingia ndani na kukijaza kiwiliwili changu chote.
Niliinuka na kusali, nikitoa shukrani kwa machozi kwa Baba wa Mbinguni. Kisha nikarudi kitandani na kulala. Siku iliyofuata, ambayo ilipaswa kuwa iliyojaa woga na huzuni; ilikuwa siku yenye furaha zaidi ambayo sijapata kuipitia nikiwa na watoto darasani.
Nilitambua kwamba Bwana alinitaka nitafakari juu ya ibada za hekaluni. Kwa Watakatifu waliovuka nyanda tambarare baada ya kupokea baraka zao katika Hekalu la Nauvoo, Rais Brigham Young (1801–1877) alisema, “Acha moto wa agano ambalo mlilifanya katika nyumba ya Bwana, uwake mioyoni mwenu, kama mwale usiozimika.” Kadiri maagano ya hekaluni yanavyowaka ndani ya mioyo na akili zetu, tutapata pia nguvu, amani na faraja.