“Maongezi ya Familia kuhusu Kujiua,” Liahona, Julai. 2024.
Maongezi ya Familia kuhusu Kujiua
Kama wazazi, tunataka kuwaandaa watoto wetu kwa ajili ya uwezekano wowote wa hatari zinazoweza kuwakabili. Japo yaweza kuwa haipendezi kuzungumza kuhusu hilo, kujiua ni mojawapo ya hatari hizo.
Maisha ya familia ni kama safari ya kupiga makasia kwenye maji meupe. Kama vile familia inapovalia majaketi na mahelmeti, wazazi ni kama viongozi ambao huelekeza njia ya mto ambao wamewahi kuupita hapo kabla. Watoto wanatuhitaji sisi ili tuwaonye juu ya mkondo mkali au mawe yaliyo mbele. Kama kule mbali chini ya mto kunaweza kuwa na maporomoko mabaya ya maji, je, tungewaonya watoto wetu kuhusu hili? Je, tungewaelekeza jinsi ya kupiga makasia hapo na wapi pa kupita ili kuepuka hayo, au tungesubiri hadi waning’inie karibu ya maporomoko ndio tuwaonye?
Kama wazazi, tunaweza tusihisi vyema kujadili mada isiyopendeza kama kujiua, lakini tunaweza kusaidia kuwalinda na kuwaandaa watoto wetu kabla hawajawa na mawazo haya hatarishi.
Wazazi wanaweza kuwasaidia watoto wajifunze kuwa imara kihisia na kujua wapi pa kugeukia wanapohitaji usaidizi wa kihisia. Reyna I. Aburto, Mshauri wa Pili wa zamani katika Urais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi, alifundisha kwamba “hii inaweza kujumuisha kuwa na taarifa kuhusu ugonjwa wa hisia, kutafuta nyenzo zinazoweza kusaidia kukabili mahangaiko haya, na hatimaye kujileta sisi na wengine kwa Kristo, ambaye ni Mponyaji Mkuu.”
Jambo Muhimu la Kulizungumzia
Baadhi ya kujiua kunatokea pasipo onyo lolote la wazi. Kwa baadhi kuna ishara ndogo tu au wakati mwingine ishara ni dhahiri. Hatuwezi kujua kwa hakika watoto wetu wanafikiria nini, hivyo tunahitaji kuwaandaa wakiwa bado wadogo—iwapo mawazo ya kujiua yataingia akilini mwao.
Dada Aburto alisisitiza, “Ni muhimu kuzungumza kuhusu mambo haya na watoto wetu, familia na marafiki katika nyumba zetu, kata na jumuiya zetu.”
Mzee Dale G. Renlund wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili amefundisha: “Kila mmoja wetu ana wanafamilia, marafiki wapendwa au jamaa ambao wamepitia mawazo ya kijitoa uhai, au wamejaribu kujiua, au wamekatisha uhai wao. … Kata nyingi, vigingi, [na familia] zimezingatia kuwa na mjadala kuhusu kuzuia kujiua baada ya mtu kuwa amejitoa uhai wake yeye mwenyewe. Swali langu ni hili—kwa nini tusubiri? Kwa nini tusifanye hivyo hivi sasa? Kwa sababu mtu fulani katika kata au kigingi anayo mawazo haya ya kujitoa uhai.”
Nilikaa na watoto wangu mwenyewe miaka kadhaa iliyopita baada ya janga hili kutokea katika eneo letu. Nilihisi kulazimika kushiriki pamoja nao kwamba kupitia Yesu Kristo, kuna njia daima ya kusonga mbele. Hakuna chochote ambacho wangeweza kufanya au kushindwa kufanya, ambacho kingefanya kujiua kuwa ndilo jibu. Katika umri wao mdogo, sikuwa na sababu ya kufikiri walikuwa katika hatari, lakini nilijua kulikuwa na mengi ya kufanya ili kuwaandaa watoto wangu kwa ajili ya kuyashughulikia mawazo hatarishi, yenye uwezekano wa kujitoa uhai.
Kuzungumza kuhusu Kujiua Kunazuia Kujiua
Nyenzo za Kanisa za mwongozo kuhusu kuzuia kujiua zinaarifu kuwa: “Kuzungumza kuhusu kujiua hakutamfanya mtu ajaribu kujiua. Kwa kweli, kuzungumza wazi kuhusu kujiua ni njia ya kufaa kusaidia kuzuia kujiua.”
Kulingana na John Ackerman, meneja wa kliniki ya kuzuia kujiua mwenye PhD kwenye Hospitali ya Kitaifa ya Watoto, “Kutengeneza nafasi salama ya kuzungumza kuhusu kujiua kunaweza kuokoa maisha ya mtoto.” Kwa kweli, anaongeza, “Kama mtoto amekuwa akipambana na mawazo ya kujiua, kujua kwamba mtu mzima mwenye kujali yuko tayari kuwa na maongezi ya wazi daima ni faraja.”
“Kuzungumza kuhusu kujiua katika njia sahihi kwa kweli kunasaidia kuzuia kuliko kuhimiza,” alifundisha Dada Aburto. Baba yake alikufa kwa kujiua. Kwa miaka mingi , amekuwa akijizuia kuzungumza kuhusu kifo cha baba yake kwa familia yake. Hata hivyo, sasa amejifunza thamani ya kuzungumza kuhusu hilo kwa uaminifu na kwa uwazi. “Sasa kwa wazi nimejadili na watoto wangu kuhusu kifo cha baba yangu na kushuhudia uponyaji ambao Mwokozi anaweza kuutoa kwenye pande zote za pazia.
Maongezi ya wazi kuhusu kujiua yanaweza kuwapa nguvu watoto ya kuja kwa wazazi na watu wazima wengine wanaowaamini badala ya kujaribu kutafiti mawazo ya kujitoa uhai wao wenyewe, endapo yataibuka.
Watoto wadogo hata wakiwa na miaka sita au saba wamewahi kutoa taarifa ya mawazo ya kujitoa uhai wao. “Imekuwa kwamba … wataalamu wa tiba na watafiti na wazazi hawakuamini kwamba watoto wadogo chini ya miaka 10 au 11 walikuwa na mawazo ya kujiua,” Dk. Ackerman anasema. “Tunajua kwamba hakika hiyo siyo kweli.” Yeye anaonyesha kwamba hata watoto wadogo zaidi wanaweza kuunganisha dhana ya kujitoa uhai na hisia kama kuwa mzigo, kuwa katika uchungu wa kihisia au kupitia hali ya kukosa tumaini.
Dada Aburto alitoa hakikisho: “Kujua jinsi ya kutambua ishara na dalili kwetu wenyewe na kwa wengine inaweza kusaidia. Tunaweza pia kujifunza kugundua mpangilio wa kufikiri usio sahihi au usio na afya na jinsi ya kuubadilisha kuwa mpangilio sahihi zaidi na wenye afya.”
Kujiua Kunatokea Mara kwa Mara Kuliko Tunavyodhani
Kwa ulimwengu mzima, karibia kifo kimoja kwa kujiua kinatokea kila baada ya sekunde 40, na ni chanzo cha pili kinachoongoza cha vifo katika ulimwengu kwa watu wa umri wa miaka 15–24. Katika uchunguzi wa hivi karibuni uliofanyika miongoni mwa maelfu ya vijana wa miaka ya kumi na kitu hivi katika Utah, Marekani, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Brigham Young waligundua kwamba karibia asilimia 12 ya vijana Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa uzito mkubwa walifikiria kujiua, na aslimia 4 walifanya jaribio hilo.
Kwa muktadha huu, katika kikundi cha vijana 25, 3 kati yao, tukiongea kitakwimu, kwa uzito mkubwa wamefikiria kujiua, na mmoja wao amejaribu kujiua.
Kama tunaweza kuwasaidia watoto wetu kupata usaidizi wanaohitaji kabla hawajafikia upeo wa mgogoro—wakati wazo linapogeuka kuwa mpango—tunaweza kuwasaidia kuchepusha njia kabla hawajachelewa sana.
Wapi pa Kuanzia
Katika umri mdogo sana, watoto wanaweza kuanza kuelewa hisia, lakini tunaweza kuwapa lugha ambayo kwa usahihi wanaweza kuelezea hisia zao. Hatua ya kwanza yaweza kuwa kuwasaidia watoto wadogo wajenge msamiati wa kihisia. Tunaweza kuwafundisha watoto waelewe tofauti kati ya ukichaa, huzuni, kukanganyikiwa na kadhalika. Kama mtoto anaweza kuelezea anahisije, tunaweza kufanya kazi pamoja kuanzia hapo. Katika umri na njia inayofaa, tunaweza kujadili hisia zao kali pamoja na watoto wadogo kabisa wa miaka sita na kuwasaidia watambue na waelezee hisia hizi.
Maongezi haya ya mapema yatawasaidia pia wazazi kufahamu aina mbalimbali za hisia za watoto wao. Watoto wengi wanapitia kwenye milima na mabonde katika ustawi wa hisia. Hii ni kawaida. Kuwa na mazungumzo mapema na mara kwa mara pamoja na watoto wadogo inaweza kuwapatia wazazi kipima joto cha hisia ili kutambua tofauti kati ya milima na mabonde ya utoto na mawazo hatarishi.
Maongezi ya kukinga kuhusu kujiua ni kama mafunzo yoyote ya kujikinga yanayotolewa na wazazi. Tunaweza kuwaandaa watoto na vijana kwa ajili ya uwezekano wa kupitia mawazo ya kujitoa uhai katika njia ile ile ambayo tungeweza kuwaanda wao kwa ajili ya kuendesha gari na nini cha kufanya katika tukio la ajali. “Tunataka kuwaandaa watoto wetu waelewe kile kinachoweza kutokea kihisia na nini wanaweza kukiona kwa marafiki zao,” anasema DK. Ackerman.
Kuendeleza Maongezi
Kadiri watoto wanavyokua, maongezi tuliyofanya pamoja nao pia yatakomaa. Tunaweza kuwauliza maswali ya wazi zaidi na halafu kuwaruhusu watoto wayajibu kwa uwazi. Watie moyo watoto kuwa waaminifu kwa hisia zao kali. Utafiti unaonyesha kwamba kuelezea hisia kali kunaweza kupunguza nguvu ya hisia hizo na muda.
Kupitia mawasiliano ya wazi kuhusu msongo wa mawazo, kujiua au hisia za kukata tamaa, watoto wanajifunza kwamba wanaweza kushiriki mawazo yao ya dhati na kwamba wako salama kihisia wakiwa nasi. “Wao pia wanapata ujumbe usio na shaka kwamba wewe kwa kina unawajali, na furaha yao na ustawi wao ni kitu muhimu kwako,” anasema mshauri mmoja wa afya ya akili.
Upendo na msaada wetu kwa ajili ya watoto wetu unaweza kuwa mfano wa upendo wa Baba yetu wa Mbinguni kwa kila mmoja wetu. “Baba yako wa Mbinguni anakupenda—kila mmoja wenu,” alifundisha Rais Thomas S. Monson (1927–2018). “Upendo huo haubadiliki. … Upendo huo uko hapo kwa ajili yako uwapo na huzuni au furaha, umekata tamaa au mwenye tumaini. Upendo wa Mungu upo hapo kwa ajili yako iwe unahisi au hauhisi kustahili upendo. Upendo huo uko hapo tu daima.”
Mara baada ya kujadili kuhusu kujiua na watoto wangu, mwana wangu wa miaka tisa aliniuliza kama angeweza kuzungumza nami faraghani. Aliniambia kuhusu nyakati ambazo amekuwa akifikiria kutoa uhai wake mwenyewe, akimalizia na jinsi ambavyo angefanya hivyo. Kamwe nisingeweza kudhani kuwa angekuwa na mawazo haya. Nilimkumbatia na kumshukuru kwa ujasiri wake katika kuniambia, na nikamwambia kwamba bila kujali lolote alilowahi kulifanya au kulifikiria, yeye ni mtu anayethaminiwa na anayehitajika katika familia yetu. Na nilijitolea kumchunga kwa dalili yoyote zaidi ya mawazo ya kujitoa uhai au maradhi ya afya ya akili.
Kujiua Siyo Jibu
Baadhi ya vijana wanaweza kuogopa kwamba kujiua ndio njia pekee kwao kuondokana na kukosa tumaini. Rais Jeffrey R. Holland, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, anatuhakikishia: “Hata kama unahisi umefanya makosa mengi kiasi gani … , au hata kama unahisi umeenda mbali na nyumbani na familia na Mungu ninashuhudia kwamba wewe hujasafiri kupita upendo wa Mungu unapoweza kukufikia. Huwezi kuzama chini zaidi ya pale mwangaza wa nuru isiyo na mwisho ya Upatanisho wa Kristo inapoangaza.”
Katika ziada ya kuzungumza na watoto wetu wadogo, tunaweza kuzungumza na vijana tukifuata mfano wa Rais Holland: “Kwa kijana wetu yeyote huko aliko ambaye anapitia magumu, bila kujali shida au magumu yako, kifo kwa kujiua ni dhahiri siyo jibu. Hakitapoza maumivu unayohisi au yale unayodhani umeyasababisha. Katika ulimwengu ambao unahitaji sana kila nuru unayoweza kupata, tafadhali acha kupunguza nuru ya milele ambayo Mungu ameiweka nafsini mwako kabla ya ulimwengu huu kuwepo. … Tafadhali acha kuangamiza uhai ambao ilimgharimu Kristo kuutoa uhai Wake ili kuulinda. Unaweza kukabiliana na changamoto za maisha haya kwa sababu sisi tutakusaidia ukabiliane nazo. Una nguvu zaidi kuliko unavyofikiria. Msaada unapatikana, kutoka kwa wengine na hususani kutoka kwa Mungu. Wewe unapendwa na kuthaminiwa na unahitajika. Sisi tunakuhitaji wewe!”
Wewe na mwenzi wako wa ndoa mnaweza kujadiliana lini ni wakati mzuri wa kuanza kuzungumza kuhusu hili—mapema kabla ya mgogoro, wowote ule kama upo haujatokea. Kwa sala mnaweza kumtafuta Roho ili awasaidie kuongoza muda sahihi na maneno ya kuongea na watoto wenu.
Kamwe hatuwajibiki kwa uchaguzi wa mtu mwingine kukatisha maisha yake, lakini kuna mambo tunayoweza kufanya ili kusaidia kuzuia hili. Kama Rais Holland alivyofundisha:
“Mwana Pekee wa Mungu alikuja kutupatia uhai kwa kukishinda kifo.
“Ni lazima tujitolee kikamilifu kwenye zawadi hii ya uhai na kukimbilia kuwasaidia wale walio katika hatari ya kuitoa zawadi hii takatifu.”