Liahona
Kazi kubwa ya Bwana na Fursa yetu Kubwa
Julai 2024


“Kazi Kubwa ya Bwana na Fursa Yetu Kubwa,” Liahona, Julai 2024.

Kazi Kubwa ya Bwana na Fursa Yetu Kubwa

Tunapopenda, kushirikina na kualika tunafanya kazi pamoja na Bwana ili kusaidia kila nafsi yenye thamani kuja kwake.

wanawake wawili wanaongea wakati wakitembea mtaani

Kila nabii katika kipindi hiki kikuu cha mwisho amewafundisha waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kushiriki injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Katika maisha yangu, mifano kadhaa huja akilini mwangu:

Rais David O. McKay (1873–1970), nabii wa ujana wangu, alitamka, “Kila Muumuni ni mmisionari.”

Raisi Spencer W. Kimball (1895–1985) alifundisha, “Siku ya kuipeleka injili sehemu mbali mbali na kwa watu imewadia na ni sasa” na “ni lazima tuzirefushe hatua” katika kushiriki injili na wengine.

Rais Gordon B. Hinckley (1910–2008) alisema: “Kazi yetu ni kubwa, jukumu letu ni kubwa katika kusaidia kutafuta watu wa kufundisha. Mungu ameweka juu yetu jukumu la kufundisha injili kwa kila kiumbe. Hii itahitaji juhudi [zetu] za dhati.”

Na Rais Russell M. Nelson amefundisha: “Kazi ya umisionari ni sehemu ya muhimu ya kusanyiko kuu la Israeli. Kusanyiko hilo ni kazi muhimu sana inayofanyika ulimwenguni leo. Hakuna kitu kingine cha kulinganishwa katika ukubwa. Hakuna kitu kingine cha kulinganishwa katika umuhimu. Wamisionari wa Bwana—wanafunzi Wake—wamejikita katika changamoto hii kuu, kusudi hili kuu, kazi hii kuu zaidi duniani leo.”

Nilikuja kulifahamu hili mimi mwenyewe kama kijana mmisionari katika Misheni ya Uingereza. Nina uhakika mkubwa zaidi juu ya hili leo hii. Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, ninashuhudia kwamba fursa zipo kila mahali kuwasaidia wengine kuja kwa Kristo kwa kuonyesha upendo wetu, kushiriki imani yetu na kuwaalika kuuungana nasi kupata shangwe ya injili ya Yesu Kristo.

Kazi Inasonga Mbele

Nilipata bahati ya kuwa kwenye jukumu katika Idara ya Wamisionari ya Kanisa wakati toleo la kwanza la Hubiri Injili Yangu lilipotambulishwa mnamo 2004, na tena wakati toleo la pili lilipotolewa mnamo 2023. Ninaamini kwamba Hubiri Injili Yangu imebariki kazi ya umisionari katika njia isiyo na kifani.

Toleo jipya la Hubiri Injili Yangu linajumuisha kila kitu tulichojifunza tangu 2004, mwelekeo wa kiungu kutoka kwa kila Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na wawili na mabadiliko yamefanywa kwa ajili ya kushiriki Injili katika zama hizi za kidijitali. Baadhi ya mabadiliko haya yamesababisha mafanikio makubwa.

Tumegundua kwamba kushiriki injili kwa urahisi, kawaida na kwa njia za asili kupitia kanuni za “penda, shiriki, alika” hubariki ufalme kwa kiasi kikubwa. Yesu Kristo alishiriki injili kwa njia hii alipoishi duniani. Alishiriki maisha Yake na upendo Wake na kuwaalika wote kuja Kwake (ona Mathayo 11:28). Kupenda, kushiriki na kualika kama alivyofanya Yeye ni baraka maalumu na wajibu kwa kila muumini wa Kanisa.

Anza na Upendo

Katika Bustani ya Gethsemane na msalabani, Yesu Kristo alijichukulia juu Yake dhambi za ulimwengu na kuteseka huzuni yote na “maumivu na mateso na majaribu ya kila aina” (Alma 7:11). Hii “ilisababisha [Yeye], … mkuu wa vyote, kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutoka damu kwenye kila kinyweleo” (Mafundisho na Maagano 19:18). Kupitia Upatanisho Wake na Ufufuko, Yesu Kristo amefanya wokovu na kuinuliwa kuwezekane kwa wote.

Kumgeukia Mwokozi na kutafakari juu ya yote ambayo Yeye ameyafanya kwa ajili yetu kutaujaza moyo wako na upendo kwa ajili Yake. Kisha Yeye huigeuza mioyo yetu kwa wengine na kutuamuru tuwapende (ona Yohana 13:34–35) na kushiriki injili Yake pamoja nao (ona Mathayo 28:19; Marko 16:15). Kama wale wanaotuzunguka wanaweza kuhisi kwamba tunawapenda kwa dhati na kuwajali, wao wanaweza kuifungua mioyo yao kwa ajili ya ujumbe wetu, kama vile Mfalme Lamoni alivyoufungua moyo wake na kuipokea Injili kwa sababu ya upendo na huduma ya Amoni ( Ona Alma 17–19).

Tunaposhiriki injili, hebu tuanze na upendo. Tunapowafikia wengine kwa upendo—tukikumbuka kwamba wao ni kaka na dada zetu na watoto wapendwa wa Baba yetu wa Mbinguni—fursa zitafunguka kwa ajili yetu za kushiriki kile tunachojua kuwa ni kweli.

Jishughulishe Kwa Bidii na Ushiriki

Hakuna aliyekuwa amejitolea zaidi kushiriki injili kuliko Rais M. Russell Ballard (1928–2023). Katika hotuba yake ya mwisho ya mkutano mkuu, alishuhudia, “Moja ya vitu vitukufu na vizuri ambavyo mtu yeyote ulimwenguni anaweza kujua [ni] kwamba Baba yetu wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo wamejionesha Wenyewe katika siku hizi za mwisho na kwamba Joseph [Smith] alikuzwa ili kurejesha utimilifu wa injili isiyo na mwisho ya Yesu Kristo.”

Katika maisha yake yote, na sehemu kubwa ya ulimwengu wote, Rais Ballard alikuwa amejikita kushiriki ujumbe huu wa thamani na kila mmoja. Alituhimiza sisi kufanya vivyo hivyo. Alifundisha kwamba tunashiriki injili “kwa kuwa majirani wema na kwa kujali na kuonyesha upendo.” Kwa kufanya hivyo, “tunaangaza injili katika maisha yetu wenyewe, na … kuangaza kwa wengine baraka ambazo injili inatoa.” Pia kwa “kutoa ushuhuda juu ya kile [sisi] tunachokijua na kukiamini na kile ambacho [sisi] tunakihisi.” Rais Ballard alifundisha, “Ushuhuda safi … unaweza kubebwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu hadi ndani ya mioyo ya wengine ambayo iko wazi kuupokea.”

Kushiriki injili ya urejesho ya Yesu Kristo ilikuwa hamu kuu zaidi ya moyo wa Rais Ballard. Tunaweza kujishughulisha kwa bidii—kama vile yeye alivyokuwa—katika kushiriki injili kwa maneno na vitendo. Kamwe hatujui ni nani miongoni mwetu angeweza kuwa anatafuta nuru ya injili lakini hajui wapi pa kuipata (ona Mafundisho na Maagano 123:12).

watu wawili wakipanda ngazi

Toa Mialiko ya Dhati

Katika kuwasaidia wengine kuja kwa Kristo, tunawaalika wao kupata uzoefu wa shangwe ambayo Mwokozi na injili Yake huleta. Tunaweza kulifanya hili kwa kuwaalika kuja kwenye shughuli, kusoma Kitabu cha Mormoni au kukutana na wamisionari. Unaweza pia kutoa mwaliko wa dhati kwao wa kuhudhuria mkutano wa sakramenti pamoja na wewe.

Tunahudhuria mkutano wa sakramenti kila wiki ili “kumwabudu Mungu na kupokea sakramenti ili kumkumbuka Yesu Kristo na Upatanisho Wake.” Huu ni wakati maalumu kwa ajili ya watu kuhisi Roho, kuja karibu na Mwokozi na kuimarisha imani yao katika Yeye.

Tunapotafuta njia za kupenda, kushiriki na kualika, mpango wetu na nguvu lazima vijumuishe kuwasaidia watu kuhudhuria mkutano wa sakramenti. Kama watakubali mwaliko wetu na kuhudhuria mkutano wa sakramenti, kuna uwezekano wao wakaendelea kwenye njia ya ubatizo na uongofu. Ninaamini kwa moyo wangu wote kwamba mafanikio makubwa yatakuja tunapowaalika wengine kuhudhuria mkutano wa sakramenti na kuwasaidia kutambua baraka wanazoweza kupokea kwa kufanya hivyo.

Bwana Atatulinda

Kamwe hatujui mafanikio na changamoto tutakazopitia kwa kupenda, kushiriki na kualika. Watoto wa Mosia “walienda kutoka mji mmoja hadi mwingine, na kutoka kwenye nyumba moja ya ibada hadi nyingine, … kuhubiri na kufundisha neno la Mungu miongoni mwa Walamani; na hivyo walianza kufanikiwa kwa wingi.” Kupitia juhudi zao, “maelfu waliletwa kwenye ufahamu wa Bwana” na wengi “waliongoka … [na] kamwe hawakuanguka” (Alma 23:4–6).

Ingawa huu hautakuwa uzoefu wetu wa siku zote, Bwana ameahidi kwamba Yeye atatusaidia kwa sababu kila nafsi ina thamani Kwake. Tunapoweka tumaini letu katika Bwana na kujishughulisha katika huduma Yake, Yeye atatuongoza katika jinsi ya kushiriki injili Yake na wengine kwa kuwapenda, kushiriki maisha yetu na shuhuda pamoja nao na kuwaalika wao kujiunga nasi katika kumfuata Yeye.

“Shangwe [yetu] itakuwa kubwa” (Mafundisho na Maagano 18:15) tunapotumia fursa zinazotuzunguka ili kumsaidia Bwana Yesu Kristo katika kazi Yake kuu ya kuzileta nafsi Kwake.