2021
Géoffroy Koussemou
Januari 2021


Waasisi Katika Kila Nchi

Géoffroy Koussemou

Mmisionari wa kwanza kutoka Benin

Géoffroy alijua kwamba Mungu alikuwa tayari kumsaidia kama angefanya sehemu yake.

missionary in Benin

Géoffroy alitoka darasani akiwa na rafiki yake aitwaye Théodore. Wavulana wote wawili walikuwa na miaka 16, na waliishi huko Benin, nchi iliyoko Afrika. Walikuwa wakienda kwenye shule mpya kujifunza kuhusu kilimo. Ilikuwa ni mara yao ya kwanza kuwa mbali na familia zao. Walitakiwa kusoma na kufanya kazi kwa muda mrefu kila siku.

Géoffroy alivuta begi lake la mgongoni na kuliweka begani mwake. “Nafikiri sitamaliza. Masomo haya ni magumu sana.”

“La!” Théodore alisema. “Usiache. Unatakiwa kumtegemea Mungu. Kama utafanya hivyo, utafanikiwa.”

Maneno ya Théodore yalibaki kwa Géoffroy kwa siku nzima iliyosalia. Géoffroy alikuwa amelelewa kama Mkristo, lakini hakuwahi kujaribu kumtegemea Mungu. Alipiga magoti sakafuni lakini hakuanza kusali. Alikuwa akiogopa. Lakini kama asingepata msaada kutoka sehemu fulani, kamwe asingeweza kufaulu masomo yake. Taratibu Géoffroy aliinamisha kichwa chake.

“Baba wa Mbinguni,” alisema, “tafadhali nionyeshe jinsi ya kukutegemea. Je, utanisaidia kufaulu masomo yangu? Ninaahidi kukutumikia kadiri niwezavyo maisha yangu yote.”

Toka wakati huo na kuendelea, Géoffroy alihisi ushujaa zaidi na mwenye nia zaidi. Masomo bado yalikuwa magumu, lakini alijua kwamba Mungu alikuwa tayari kumsaidia kama angefanya sehemu yake. Géoffroy aliweka kando woga wake na kufanya kazi kwa bidii.

Alifanya vyema shuleni. Miezi kumi na nane baade, hatimaye alikuwa tayari kuhitimu. Alikuwa ameweza!

Baada ya kumaliza shule, Géoffroy aliendelea kufanya kazi kwa bidii. Punde akawa na shamba lake mwenyewe.

Kisha siku moja alimuona rafiki ambaye alikuwa ni muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Rafiki yake alimpa Kitabu cha Mormoni. Géoffroy alisoma Kitabu cha Mormoni na kusali. Alihisi hisia za mwako na amani ndani yake na alijua kwa hakika kwamba Kanisa ni la kweli.

Alikuwa tayari amekwishajua nini cha kufanya baada ya hapo. Alifanya kazi, alisali, na kumtegemea Mungu. Kwanza alibatizwa. Kisha alishiriki ushuhuda wake na wale waliomzunguka. Baadhi ya rafiki zake walibatizwa pia. Kile ambacho kilianza kama kundi dogo la waumini punde lilikuwa na kuwa tawi. Alikuwa akisaidia Kanisa kukua huko Benin!

Géoffroy alitaka kwenda misheni. Hakuwa na fedha za kutosha, hivyo aliuza shamba lake. Miezi michache baadae, alipokea wito wake wa misheni kwenda Ivory Coast. Alikuwa mmisionari wa kwanza kutoka Benin kupata wito wa kwenda misheni.

Kujitoa kwake kulimsaidia kwa miaka mingi. Kwa sababu ya imani yake, na ile ya waumini wengine, wengi zaidi walibatizwa. Tawi lake likawa kata. Kata hiyo kwa sasa ni sehemu ya kigingi cha kwanza huko Benin!

Géoffroy Koussemou anaendelea kufanya kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu. Anajua kwamba vitu vikuu vinaweza kufanyika kwa msaada wa Mungu. ●

Friend Magazine, 2021/01-02 Jan/Feb

Vielelezo na Isabel Muñoz