Siku ya Kwanza ya Jaechen
Je hii ilikuwa ni njia sahihi? Jaechen alihisi mkanganyiko.
“Nalimtafuta Bwana, nae akanisikia” (Zaburi 34:4). Tukio hili limetokea huko Gyeonggi-do, Korea ya Kusini.
Muziki wa kufurahisha ulichezwa wakati Jaechan na Mama wakinyanyuka kutoka kwenye viti vyao kwenye chumba cha mazoezi cha shule. Maputo mengi yenye rangi angavu yalielea ukutani wakati watoto wengine na wazazi wao wakizungumza kwa hamasa.
Kesho ingekuwa siku ya kwanza shuleni, na huko Korea ya Kusini wanafunzi wapya mara zote walipitia programu maalum kusherehekea shule kuanza. Wakati akisikiliza nyimbo na wazungumzaji Jaechan alihisi hamasa. Hakutaka kuchelewa kuanza kujifunza!
Baada ya programu, Mama na Jaechan walitembea wakipita kwenye kumbi za shule. Walipofika kwenye darasa lake, Jaechan alikutana na mwalimu wake. Alionekana kuwa mwalimu mkarimu kweli.
Baadae Mama na Jaechan walitembea nje kwenye jua la uvuguvugu la majira ya kuchipua. Hata jua na anga vilionekana kuwa na furaha kwa shule kuanza.
Asubuhi iliyofuata, Mama alimpeleka Jaechan mpaka kwenye geti la shule. Alimkumbatia kwa nguvu. “Ninakupenda,” mama alisema. “Uwe na siku njema ya kwanza.”
“Sawa,” alisema Jaechan. “Nakupenda pia!” Jaechan alipunga mkono wa kwaheri na aligeuka na kutembea kuelekea darasani kwake, kama walivyoonyeshwa.
Wakati Jaechan akitembea kuelekea ukumbini, alianza kuhisi woga. Je, hii ni njia sahihi? Jaechan alisimama na kuangalia mazingira yanayomzunguka. Aligeuka na kutembea kuelekea ukumbi mwingine. Punde kila kitu kilionekana kama mkanganyiko.
Jaechan alivuta pumzi kwa nguvu. Aligundua kuwa alikuwa amepata kuwa kwenye njia hiyo jana. Aliendelea kutembea na aliingia kwa kupitia seti ya milango mikubwa.
Lakini Jaechan hakuliona darasa lake, lenye madawati na marafiki na mwalimu wake mkarimu. Aliona chumba cha mazoezi. Na sasa hakikuwa na watu wala maputo. Kilikuwa ni chumba kikubwa kilicho wazi.
Machozi yalijaa katika macho ya Jaechan. Alijaribu kutohamaki, lakini alikuwa na hofu. Hakujua jinsi ya kulipata darasa lake. Alipiga magoti kusali. “Baba wa Mbinguni, nimepotea. Tafadhali msaidie Mama aje kunitafuta na kunisaidia kufika kwenye darasa langu.”
Jaechan alisimama. Akavuta pumzi kwa nguvu mara kadhaa. Kisha akasubiri.
Dakika chache baadae, Mama alitokea kwenye kona. “Jaechan!” Mama alimkimbilia na kuwa naye karibu. “Nini kimetokea?”
Jaechan alitirirkwa na machozi mengi. Alikuwa amefarijika kumuona Mama. “Sikuweza kulipata darasa langu,” alisema. “Hivyo nilisali kwamba ungekuja na kunipata.”
Mama alifuta machozi kutoka mashavuni mwa Jaechan. “Nashukuru ulisali,” mama alisema. “Nilikuwa njiani kuelekea nyumbani. Kisha nilipata hisia kwamba nirudi na kuhakikisha umelipata darasa lako. Nilipokukosa huko, niliangalia kila sehemu. Ndipo nikakupata!”
Jaechan alishika mkono wa Mama wakati wakitembea kwenye njia sahihi. Jaechan alikuwa ameacha kulia. Alijua Baba wa Mbinguni alikuwa amejibu sala yake, na kila kitu kilikuwa SAWA. Wakati walipofika kwenye darasa, alisikia watoto wengine waliokuwa ndani wakicheka na kufurahia.
“Jaechan! Tunafurahi kukuona,” mwalimu wa Jaechan alisema wakati Jaechan akiingia.
“Asante,” Jaechan alisema huku akiinama kidogo. Alimkumbatia mama kwa mara nyingine tena. Hatimaye itakuwa ni siku nzuri ya kwanza shuleni.