2021
Tatizo la Sherehe
Januari 2021


Tatizo la Sherehe

Mwandishi anaishi Corrientes, Argentina.

Sehemu ya Luz ilitaka kwenda kwenye sherehe. Lakini bado alihisi uzito.

“Chunguza katika akili yako; ndipo … uniulize kama ni sahihi.” (Mafundisho na Maagano 9:8). Tukio hili limetokea Corrientes, Agentina.

Picha
girl talking with her parents on couch

Luz alihisi furaha. Mwaka wa masomo ulikuwa unaelekea kuisha, na vitu vingi vya kufurahisha vilikuwa vinatendeka. Punde angehitimu darasa la sita. Mwaka unaofuata angekuwa anaingia shule ya upili!

Ilimshangaza kujua ni kwa jinsi gani alikuwa amekua. Alikuwa mrefu, na hakuwa mtoto tena. Mabadiliko hayo yalikuwa ya kuvutia, lakini pia alihisi woga kidogo.

Aliamua kuzungumza kuhusu hilo na wazazi wake.

“Huu ni wakati wa kuvutia sana katika maisha yako, Luz,” Baba alisema. “Ni wakati kwa ajili yako kujifunza, kufanya kadiri uwezavyo, na kufikia malengo ambayo yatakusaidia kuwa aina ya mtu ambaye Mungu anajua unaweza kuwa.”

“Lakini maisha huja siku hadi siku,” Mama alisema. “Utakua na kuwa aina ya mtu huyo kwa kila uchaguzi mdogo, mzuri unaofanya.”

Hiyo ilimfanya Luz kujisikia vizuri. Alifurahi kwamba hakutakiwa kukua mara moja.

Siku moja shuleni, rafiki za Luz walimwambia kwamba wanakwenda kwenye sherehe ya mahafali. Walikuwa wenye hamasa sana. Kungekuwa na chakula cha usiku, muziki, taa, na hata dansi!

Lakini kadiri Luz alivyowasikiliza rafiki zake wakizungumzia kuhusu sherehe, alianza kuhisi kutokuwa sawa. Haikuonekana kama aina ya sherehe ambapo angeweza kumhisi Roho Mtakatifu.

“Utakuja, si ndio, Luz?” mmoja wa rafiki zake aliuliza.

“Huna budi kuja!” rafiki mwingine alisema. “Nitawaambia wazazi wangu wazungumze na wazazi wako. Kisha watakuruhusu kuja.”

“Labda.” Tumbo la Luz lilianza kusokota. “Ni … nitawajulisha.”

Luz alitumia wiki nzima akitafakari kuhusu sherehe. Aliifikiria wakati akifanya mazoezi ya kinanda. Aliifikiria wakati akicheza na kaka yake mdogo. Licha ya chochote alichofanya, bado ilikuwa akilini mwake.

Sehemu ya nia yake ilitaka kwenda kwenye sherehe. Lakini bado alihisi uzito. Hisia za woga ndani ya tumbo lake hazikuondoka.

“Uko SAWA, hija?” Mama aliuliza Jumapili mchana. Alipitisha vidole vyake kwenye nywele ndefu, nyeusi za Luz.

“Ni kwamba …,” Luz alisema.

“Bado unatafakari kuhusu sherehe?”

“Sijui nini cha kufanya,” Luz alisema. “Nataka kwenda. Lakini najua sitakuwa na hisia nzuri huko.”

Mama alitabasamu. “Ninajua utachagua kilicho sahihi,” mama alisema. “Fikiria kuhusu hilo, fanya uamuzi wako, na mwambie Baba wa Mbinguni kile ulichoamua. Yeye atakusaidia kujua kama ni sahihi. Utahisi moyoni mwako.”

Luz aliitikia kwa kutikisa kichwa. Alivuta pumzi kwa nguvu kisha akaenda chumbani kwake kusali.

“Baba wa Mbinguni,” Luz alinong’ona. “Rafiki zangu walinialika kwenye sherehe, lakini sihisi vizuri kuhusu hilo. Nitawaambia kwamba siwezi kwenda. Je, hiki ni sahihi kufanya?”

Hisia za mwako zilikuja kwa Luz. Hakuhisi mkanganyiko tena. Alihisi kama vile amejawa na mwangaza! Alijua kwamba alikuwa anafanya uchaguzi sahihi.

Wakati Luz alipotoka chumbani kwake, alimkumbatia Mama yake.

“Nimeamua kutokwenda,” Luz alimwambia.

“Ninafurahi juu yako,” Mama alisema.

Baba pia alimkumbatia Luz. “Nina wazo,” Baba alisema. “Acha tufanye sherehe yetu wenyewe ya mahafali. Tunaweza kuwa na ice cream na kusherehekea kama familia!”

Luz alitabasamu. Alipenda ice cream! Na alipenda kujua kwamba angeweza kufanya jambo sahihi, hata wakati ilikuwa vigumu. Kwa kila uchaguzi mdogo mzuri alioufanya, angeweza kukua kuja kuwa mtu ambaye Mungu alijua angeweza kuwa. ●

Picha
Friend Magazine, 2021/01-02 Jan/Feb

Vielelezo na Tammie Lyon

Chapisha