Siri na Mambo ya kushtukiza
Mwandishi anaishi lowa, Marekani
Je ilikuwa sahihi kutunza siri ya Kate?
“Roho ya Kristo imetolewa kwa kila mtu, ili ajue mema na maovu” (Moroni 7:16).
“Jamani, Tazama!” Kate alichukua mwanasesere wa karatasi aliyekunjamana kutoka sakafuni katika duka. “Hapa, mweke mfukoni mwako.”
“Unataka nimchukue” Maddy aliuliza.
“Duka haliwezi kumwuza hata hivyo,” Kate alisema. “Watamtupa tu kwenye taka. Hili ni jukumu la uokozi. Tunamwokoa mwanasesere huyu!”
Kate alimtabasamia Maddy. Maddy akatabasamu pia.
“SAWA.” Maddy alimweka mwanasesere kwenye mfuko wake. Lilionekana jambo la kipekee kuwa kwenye jukumu la uokozi!
Bado, walipotembea kutoka dukani, mwanasesere wa karatasi alionekana kuwa jabali zito kwenye mfuko wake. Je, hivyo ndivyo jukumu la uokozi lilivyopaswa kuwa?
Waliporudi nyumbani kwao Maddy, Kate alimwekea utepe na kumtandaza mwanasesere kwa makini kadri ya uwezo wake.
“Ni nguo za aina gani ninapaswa kumtayarishia?” aliuliza, huku akichukua penseli ya rangi. “Unaonaje gauni maridadi la mpira?”
Maddy aliitikia kwa kichwa. “Kisha tumwonyeshe mama yangu!”
“Hapana! Hatuwezi kumwambia yeyote,” Kate alisema. “Kamwe. Ni siri yetu, Sawa? Niahidi kuwa hutasema.”
“Oh … Sawa. Ninaahidi,” Maddy alisema. “Lakini kwa nini tusiseme?”
“Ukisema, mama yako atakasirika na huenda asituruhusu kucheza pamoja tena.”
“Kwa nini akasirike?” Maddy aliuliza. Tumbo lake lilianza kupapatika na kuwa na wasiwasi.
Kate aliweka chini penseli yake ya rangi. “Usiposema, nitakuruhusu umchukue mwanasesere na nguo zote ninazomchorea.”
Sasa Maddy alijua sababu ya yeye kuwa na wasiwasi. “Sisi … tulimwiba, sivyo?” alinong’oneza.
“Wewe ndiwe uliyemweka kwenye mfuko wako na kumpenyeza nje ya duka.”
“Kwa sababu uliniambia nifanye hivyo!”
“Sikukuambia!” Kate alisema. “Ninaenda nyumbani kabla hujanitia matatani.” Alisimama na kukimbilia nje ya mlango.
Kisha Mama akaingia chumbani. “Kwa nini Kate aliondoka haraka vile?” Aliona mwanasesere wa karatasi mikononi mwa Maddy. “Huyo ametoka wapi?”
Maddy alijiuma midomo. Hakuhisi vizuri kuhusu kumficha mama siri. Lakini vipi ikiwa Kate alikuwa sahihi na Mama alikasirika?
Hisia za woga ndani ya tumbo lake hazikuondoka. Alivuta pumzi kwa nguvu kisha kuropoka hadithi yote.
“Kate aliniambia niahidi kuiweka siri,” alisema. “Lakini ilionekana kuwa si sawa.”
Mama alikaa kando yake kitandani. “Siri nyingi ni makosa. Hasa ukiambiwa usimwambie mtu yeyote. Kwa upande mwingine, jambo la kushtukiza, kama zawadi au karamu, linaweza kuwa jambo zuri. Linakusudia kuleta raha kwa kila mtu.”
Maddy aliitikia kwa kichwa. “Asante kwa kutonikasirikia,” alisema. “Kate alisema kuwa ungekasirika.”
Mama alimkumbatia kwa nguvu. “Ninaona fahari kwa ajili yako kwa kusikiliza Roho Mtakatifu na kuniambia ukweli.”
“Unaweza kunisindikiza hadi dukani ili kurejesha mwanasesere?” Maddy aliuliza.
“Bila shaka!” Mama alitabasamu. “Na tukirudi, unaweza kunisaidia kuoka keki ili kumshtukiza Baba.”
Maddy alicheka. “Sasa hilo ni jambo linalonifurahisha!”