2023
Shiriki Kitu Unachokipenda
Julai 2023


“Shiriki Kitu Unachokipenda,” Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2023.

Shiriki Kitu Unachokipenda

Upendo wako kwa injili, kwa watu wengine, na kwa Bwana unakupa nguvu ya kushiriki injili.

Picha
Yesu Kristo, origami, simujanja, sindano na uzi, daraja, Kitabu cha Mormoni

Kwa Kusudi Hili, na Yongsung Kim, Havenlight.com

Kwa mara ya kwanza nilitembelea Mto Ribble karibu na Preston, Uingereza, wakati nikihudumu kama mmisionari kijana katika Misheni ya British. Hapo, Mtume na mmisionari Heber C. Kimball alibatiza waongofu wa kwanza kwenye Kanisa la Urejesho la Yesu Kristo nje ya Amerika ya Kaskazini mnamo Julai, 1837.

Nilipokuwa nimesimama darajani nikitazama ng’ambo ya mto na nikifikiria kuhusu kile kilichokuwa kimetokea mahali hapo, nilipokea ushahidi wenye nguvu juu ya Yesu Kristo na injili Yake ya urejesho.

Misheni yangu ilikuwa uzoefu wa kupendeza, wenye kuleta maana katika maisha yangu. Leo, mara nyingi ninatafakari juu ya shangwe iliyoje kwangu kutumia sehemu kubwa ya maisha yangu nikishiriki injili ya Yesu Kristo. Siwezi kufikiria kitu kingine chochote kilicho muhimu zaidi ya hicho.

Hitaji la Kushiriki injili

Fikiria umekuwa mfuasi wa Yesu Kristo wakati wa Kufufuka Kwake. Jinsi gani ingependeza wewe kumwona Yeye na kusikia ujumbe Wake?

Ujumbe mzito wa Bwana aliyefufuka ulikuwa mwaliko na amri ya kuhubiri injili Yake. Alisema, “Basi, enendeni, na kuwafundisha mataifa yote” (Mathayo 28:19), na “enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe” (Marko 16:15).

Rais Russell M. Nelson ametamka kwamba “injili ya Yesu Kristo kamwe haijawahi kuhitajika zaidi kama ilivyo leo. … Tuna jukumu takatifu la kushiriki nguvu na amani ya Yesu Kristo kwa wale wote ambao watasikiliza na kuacha Mungu ashinde katika maisha yao.”1

Bwana Anakuhitaji Wewe Sasa

Unaishi katika wakati wa kipekee na muhimu—kipindi cha mwisho cha maongozi ya Mungu kabla ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo. Nabii Joseph Smith alitoa unabii kwamba kabla ya kuja tena kwa Bwana, ukweli wa Mungu utasonga mbele kwa ujasiri, uadilifu, na kwa uhuru, hadi utakapopenya kila bara, kutembelea kila tabia ya nchi, kufagia kila nchi, na kusikika katika kila sikio, hadi pale makusudi ya Mungu yatakapokuwa yamekamilika, na Yehova Mkuu atakaposema kazi imekwisha.”2

Ni nani atakwenda kusaidia kukamilika kwa hili? Wewe!

Huhitaji kuwa mmisionari ili kushiriki injili. Bwana anakuhitaji wewe sasa ili kufanya kushiriki injili Yake ya furaha, na ya upekee wa milele katika maneno na matendo kuwe njia ya maisha na sehemu ya wewe ulivyo.

Fokasi kwenye Upendo

Sababu muhimu zaidi ya sisi kushiriki injili ni kwamba Bwana ametuamuru tufanye hivyo. Wakati mwingine hii inaweza kuwa changamoto, lakini ninakuahidi kwamba kadiri unavyofokasi juu ya Mwokozi Yesu Kristo na jinsi unavyompenda Yeye na jinsi Yeye anavyokupenda wewe, utaongozwa katika juhudi zako hizo.

Picha
kioo cha kukuza picha kikiwa juu ya picha ya Yesu Kristo.

Amefufuka, na Greg Olsen

Upendo wako kwa injili, kwa watu wengine, na muhimu zaidi, upendo wako kwa Bwana unakupa nguvu ya kukubali wito Wake mtakatifu wa kushiriki injili Yake.

Ipende Injili

Bwana amesema, “Jifunzeni kwangu” (Mafundisho na Maagano 19:23; Mathayo 11:29). Kadiri unavyojifunza zaidi injili na kujifunza juu ya Yesu Kristo na misheni Yake takatifu kama Mwokozi na Mkombozi, ndivyo zaidi upendo wako kwa injili utakavyokua.

Unashiriki upendo wako wa injili kadiri unavyoiishi. Mtume Paulo alifundisha, “Uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi, na mwenendo, katika upendo, na imani, na usafi” (1 Timotheo 4:12). Mara nyingi watu wanaipokea injili kwa sababu wameona mambo chanya kwa waumini wa Kanisa. Tafadhali usiishi maisha ya kujificha kwa njia ya kudanganya kiroho. “Nuru yenu na iangaze” (Mathayo 5:16) na waoneshe wengine kuwa injili ni sehemu muhimu ya wewe ulivyo na kile unachofanya.

Wapende Wengine

Fikiria kuhusu rafiki zako. Je, unashiriki pamoja nao sinema, muziki na chakula ukipendacho? Je, unashiriki pamoja nao vipaji na mapendeleo yako? Pengine umekuwa ukijiuliza kama wataipokea injili ikiwa utashiriki nao. Huwezi kujua isipokuwa umejaribu kufanya hivyo. Rais Nelson amefundisha, “Kila mtu anastahili fursa ya kujua kuhusu injili ya urejesho ya Yesu Kristo.”3

Wafikie kwa upendo marafiki, washiriki wa familia, majirani, wanafunzi wenzako darasani, na wengine—ukikumbuka kwamba hao ni kaka zako na dada zako na watoto wapendwa wa Baba wa Mbinguni—nawe utaona ni rahisi zaidi kushiriki injili pamoja nao.

Mpende Bwana

Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ujumbe wetu kwa ulimwengu ni kwamba Yesu Kristo yu hai! Amefanya iwezekane kwa kila mmoja wetu kupata wokovu na kuinuliwa.

Utauhisi upendo wa Bwana kwako wakati unapotafakari yale yote aliyofanya kwa ajili yako. Nafsi yako itajawa na upendo Kwake, na utaona kwamba huwezi kujizuia kushiriki ukweli huu wa kupendeza uliopokea kutoka Kwake.

Shangwe Yako Itakuwa Kubwa

Tukio langu la kutia moyo kiroho pale darajani juu ya Mto Ribble kama mmisionari kijana limeniletea shangwe ya milele iliyoahidiwa kwa wale wanaoshiriki injili (ona Mafundisho na Maagano 18:15).

Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, ninao uhakika zaidi leo kwamba kushiriki injili ni shangwe na dhihirisho la kina la upendo wetu kwa injili ya urejesho, kwa watoto wa Mungu, na kwa Bwana.

Picha
Quentin L. Cook pamoja na vijana

Mzee Cook anazungumza na vijana waliohamishwa kutoka Volkano ya Taal huko Batangas, Ufilipino, mnamo Januari 15, 2020.

Ninashuhudia kwamba unapoukubali mwaliko wa Bwana na kushiriki kile unachokipenda, unamsaidia Yeye kujenga Kanisa Lake na kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya kurudi Kwake, wakati “Atakapo tawala kama Mfalme wa Wafalme na … Bwana wa Mabwana.”4 Ninaomba kwamba mtamfuata Yeye na kushiriki injili Yake maisha yenu yote.

Chapisha