“Kusanya—Usitawanye,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2023.
Njoo, Unifuate
Kusanya—Usitawanye
Mungu haoneshi upendeleo miongoni mwa watu na wala sisi hatupaswi kuonesha upendeleo.
Wiki chache baada ya kuwasili Ujerumani kama mmisionari, mimi na mwalimu wangu tulibisha hodi kwenye mlango wa mwanamke mmoja mzee, ambaye alikubali tumfundishe.
Wakati wa somo letu la kwanza, tulimwalika asome andiko kwa sauti. Kupitia miwani yenye kioo kizito, alisoma kwa shida, akitatizwa na maneno. Na majibu yake kwa maswali yetu yalikuwa mafupi sana. Hatukuwa na uhakika ni kwa kiasi gani alielewa.
Tulimwomba asome vifungu kadhaa vya maneno katika Kitabu cha Mormoni kabla ya kurudi kwetu mara ya pili. Tuliporudi tena, alikuwa amevisoma lakini haikuonekana kama alikuwa ameelewa. Tulijiuliza ikiwa yawezekana ana changamoto za kujifunza. Tulijiuliza ikiwa tuendelee kumfundisha. Lakini tuliendelea kwenda.
Kwenye matembezi yetu yaliyofuata, tulishangazwa aliposema alitaka kubatizwa. Kisha, kadiri tulivyoendelea kumfundisha, tuligundua kwamba kusoma kwake kulikuwa bora zaidi. Majibu yake kwa maswali yetu bado yalikuwa mafupi lakini yalionekana kuwa bora na yenye uhakika zaidi.
Punde nilihamishwa kwenda mji mwingine, lakini mkufunzi wangu aliniandikia baadae kusema kwamba mwanamke huyu alikuwa amebatizwa na alikuwa akisaidiwa na washiriki wa tawi. Kama ungetuuliza wiki kadhaa kabla kati ya wote tuliokutana nao yupi angekuwa na uwezekano mkubwa wa kubatizwa na kupata nafasi katika Kanisa, yeye asingekuwa juu kwenye orodha yetu.
Na hivyo tulijifunza somo hili la zamani—somo sawa na lile Mtume Petro alilojifunza zamani na ambalo kila mmoja wetu anahitaji kuendelea kujifunza: “Mungu hana upendeleo” (Matendo ya Mitume10:34).
Badiliko Kubwa
Petro aliliongoza Kanisa wakati wa hatari. Mwokozi alikuwa amewaambia Mitume Wake, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe” (Marko 16:15). Lakini hadi wakati huo walikuwa wakifundisha na kubatiza miongoni mwa Wayahudi pekee.
Kisha mambo kadhaa yalitokea. Akida wa Kirumi aliyeitwa Kornelio—Mtu wa Mataifa, au asiye Myahudi, askari aliyevaa sare ile ile kama ya wale waliomsulubisha Yesu Kristo—alimwona malaika katika ono. Malaika alimwambia Kornelio amtafute mtu aliyeitwa Petro ili amfundishe. Siyo muda mrefu baada ya hapo, Petro alipata ono ambapo ndani yake aliona chakula kilichokuwa kimekatazwa chini ya sheria za Kiyahudi, na bado yeye aliambiwa akile kwa sababu Mungu alikitakasa. Mara baada ya Petro kuona ono, watumishi wa Kornelio walifika na wakamwomba aende pamoja nao. Roho alimwambia Petro aende.
Baada ya kukutana na Kornelio na kumwona jinsi alivyo mwema na mkweli, Petro alielewa maana ya ono lake. Injili ilihitajika kwenda kwa Watu wa Mataifa kama Kornelio pia. Hapo ndipo Petro aliposema, “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo: bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye” (Matendo ya Mitume 10:34–35). Petro alimfundisha Kornelio kuhusu Yesu Kristo na alimwalika yeye na nyumba yake wabatizwe. (Ona Matendo ya Mitume 10.)
Kuileta injili kwa Watu wa Mataifa kulileta badiliko kubwa kwa Kanisa la awali. Baadhi ya watu walikuwa na wakati mgumu kukubali badiliko hili. Lakini lilikuwa jambo sahihi, na lilifundisha ukweli wa msingi kuhusu Mungu na wanadamu wenzetu.
Hakuna Upendeleo
Anapowabariki watoto Wake, Mungu haoneshi upendeleo kutokana na utaifa, rangi, jinsia, elimu, uwezo, mwonekano au tofauti nyingine yoyote ambayo inawagawa watu.1 Yeye “anawapenda watu wote sawa sawa; yule ambaye ni mtakatifu anapendelewa na Mungu” (1 Nephi 17:35). Wote wanaweza kuja Kwake, kwani “wote ni sawa kwa Mungu” (2 Nefi 26:33). Yeye “huutazama moyo” (1 Samueli 16:7). Yeye anawakubali wale “wanaotenda haki, … wanaopenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu” (Mika 6:8).
Mtu yeyote anaweza kuchagua kuja kwa Yesu Kristo, kufanya maagano na Baba wa Mbinguni, na kufuata njia Zao. Na ukweli huu unapaswa kuongoza jinsi gani tunavyoshiriki injili ya Bwana na upendo Wake.
Hatuwezi tu kuangalia tabia za mtu za nje na kudhani wao siyo “wa aina” ya injili. Hatuwezi kutumia vibandiko vya kiulimwengu kwa watu na kudhani vibandiko hivyo vinawafanya wasistahili kujumuishwa kanisani. Hatuwezi kuamua tu kutomhudumia mtu kwa sababu tu wana maoni tofauti ya kisiasa, mapendeleo, au vionjo tofauti na vyetu.
Mungu hamwoni mtu kama lundo la vibandiko vinavyowakilisha makundi au tabia mbalimbali. Yeye anamwona mtu—mtoto Wake. Na hivyo ndivyo tunavyopaswa kumwona kila mtu—kama mtu wa kipekee mwenye nafasi na uwezo ulio sawa wa kuja kwa Mungu.
Kuwa Mkusanyaji
Rais Russell M. Nelson ametuhimiza tushiriki katika kuikusanya Israeli.2 Lakini kama sisi, tofauti na Mungu, tunachagua kuwa “wenye upendeleo” inapokuja kwenye kushiriki injili na kuwajumuisha watu kanisani, yawezekana tukawa watawanyaji au wenye kugawa zaidi kuliko wenye kukusanya na kuunganisha.
Acha kila mtu aazimie: hakuna kutawanya tena. Kuwa mkusanyaji. Penda, shiriki, alika.
Mimi na mmisionari mwenza hatukuwa na uhakika kama mwanamke yule tuliyekuwa tukimfundisha huko Ujerumani angeweza kubatizwa. Hatukuujua moyo wake, lakini Mungu aliujua. Ninafurahi kuwa tulipata uvuvio wa kuendelea kumfundisha.
Unapojaribu kumfuata Roho na kujaribu kutokuwa na upendeleo, utaongozwa kuwasaidia wale wanaokuzunguka waje kwa Kristo, bila kujali tofauti zao.