2023
Hadithi Fupi Sana 11 kuhusu Kushiriki Injili
Julai 2023


“Hadithi Fupi Sana 11 kuhusu Kushiriki Injili,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2023

Hadithi Fupi Sana 11 kuhusu Kushiriki Injili

Na jinsi wewe unavyoweza kushiriki pia!

msichana; watoto wakisali

Onesha Jinsi Injili Inavyoweza Kusaidia

Nilikuwa darasani siku moja nimekaa pembeni ya rafiki yangu. Tulikuwa tukijiandaa kufanya mtihani, na aliniambia alikuwa na wasiwasi sana. Nilihisi kwamba nilihitaji kumfundisha jinsi ya kusali. Kisha sote tuliinamisha vichwa vyetu na kimya kimya tukasali tupate msaada kwenye mtihani huo. Ninashukuru kwamba sala iliweza kusaidia kumtuliza rafiki yangu.

Abigail, Uruguay

mvulana; vijana wakimtembelea mwanamke mzee

Wahudumie Watu Wenye Shida

Tulikuwa na bibi kizee katika kata yetu ambaye hakuweza kuja mwenyewe kwenye mkutano wa sakramenti kwa sababu ya matatizo ya kiafya. Mimi na baba yangu tulimwomba askofu ikiwa tungeweza kumpelekea sakramenti nyumbani kwake kila wiki. Mume wake, ambaye alikuwa hahudhurii kikamilifu kanisani, alianza pia kupokea sakramenti. Kukusanya Israeli kunamaanisha tunahitaji kuwaalika wengine waje karibu zaidi na Yesu Kristo. Kuhudumu ni sehemu kubwa ya hili.

Shion, Utah, Marekani

wavulana, watoto wakicheza

Alika kwenye Shughuli

Nilikuwa ninaendesha baiskeli karibu na kanisa wakati nilipowaona watu wengi hapo wakicheza dansi. Nilimwita mvulana mmoja (jina lake Courage) na kumwuliza kile ambacho walikuwa wakifanya. Alisema walikuwa wamehudhuria madarasa yanayoitwa seminari Aliniambia kungekuwa na shughuli hapo kanisani na aliniuliza ikiwa nitakwenda naye. Courage, kama rafiki yangu, hakika alibadilisha maisha yangu kwa kunisaidia nijue kuhusu injili.

David, Ghana

mvulana; vijana wakipanda ngazi

Kuwa Mfano

Ninajifunza mengi ninapomwangalia kaka yangu mkubwa. Ninapenda michezo ya video na soka, na, kusema kweli, ningeweza pengine kufanya mambo hayo muda wote kama isingelikuwa yeye. Anapenda mambo hayo pia, na muda mwingi sana tunacheza pamoja, lakini daima anatenga muda wa kukua na kuwa bora. Sitasahau nilipoalikwa kutumia madawa ya kulevya shuleni. Mara moja nilimfikiria kaka yangu na nilijua kile ambacho yeye angechagua; kwa sababu ninataka kuwa kama yeye, nilifanya uchaguzi sahihi na nikasema hapana.

Emilio, Tennessee, Marekani

msichana; wasichana wakikumbatiana

Wasaidie Wangine Wahisi Upendo wa Kristo

Wakati wa mkutano wa KNV, nilijihisi mpweke sana. Nilisali kila siku, nikitumaini kuhisi Roho na upendo wa Yesu Kristo. Baada ya moja ya hotuba, msichana ambaye sikuwa ninamjua vizuri alikuja na kunipa kumbatio. Nilihisi upendo wa Kristo katika kumbatio lake, kana kwamba Yeye alikuwa akiniambia Ananipenda.

Natalie, Chile

Msichana; wasichana wakiwa na simu

Fuata Misukumo

Siku moja nilipata msukumo wa kiroho kwamba ninapaswa kumwalika rafiki yangu wa shuleni kwenye ibada fupi. Nilitaka kupuuza msukumo ule, lakini mwishowe nilimtumia ujumbe mfupi kwa simu siku moja kabla. Tulipokuwa tumekaa pamoja kwenye ibada ile fupi, nilikuwa na wasiwasi. Lakini mkutano ulipokwisha, alikuwa na tabasamu kubwa usoni mwake. Ilikuwa ukumbusho kwangu kwamba Mungu anawajua watoto Wake vizuri zaidi kuliko mimi na kwamba daima ninapaswa kufuata misukumo ya kushiriki injili ya Yesu Kristo.

Eliza, Minnesota, Marekani

Mvulana; vijana kwenye bustani

Sali kuhusu Nini cha Kusema

Mimi na dada yangu ni waumini pekee wa Kanisa katika shule yetu. Watu wanatambua kuwa tuko tofauti na daima wanauliza maswali. Mwanzoni nilikuwa na wasiwasi kuzungumza nao, lakini nilisali ili niweze kusema kitu sahihi, nao wamenisikiliza na kuheshimu chaguzi zangu.

Ruben, Norway

msichana; msichana akiwa na chombo cha kidigitali

Shiriki Kweli za Injili Mtandaoni

Kwa ajili ya lengo, nilipitia Njoo, Unifuate na nilipata maandiko na nukuu za kushiriki kwenye Mitandao ya Kijamii. Nilipokea maoni kadhaa kutoka kwa watu wakisema walimhisi Roho kupitia posti zangu. Kushiriki injili kunaweza kuwasaidia wengine katika njia tusizoweza kudhania katika wakati huo.

Raquel, Brazili

Msichana; watoto wakiwa shuleni

Kuwa Mbunifu

Katika moja ya madarasa yangu shuleni, tulikuwa tukisoma kitabu ambacho kilikuwa kinalikosoa Kanisa. Nilijua nilihitajika kuzungumza kuhusu ukweli juu ya injili ya urejesho. Hivyo niliinua mkono wangu. Mwalimu aliniruhusu, lakini sikujua cha kusema. Kwa sababu fulani, nilianza kuimba nyimbo za Makala ya Imani. Kwa mshangao wangu, ukimya mkubwa ulijaa chumbani. Baada ya hapo mkanganyiko ulipungua, na mwalimu wangu na wanadarasa wenzangu walitenda kwa heshima kwenye mjadala na kwangu mimi.

Monique, Massachusetts, Marekani

Msichana; familia wakiwa nyumbani

Kuwa Nuru

Nilipokuwa na miaka 15, niliamua kutafuta kanisa la kuhudhuria. Siku chache baadaye, nilikuwa rafiki na msichana shuleni ambaye alionekana kuwa na nuru imemzunguka. Wiki kadhaa baadaye, alinialika nyumbani kwao. Nilipofika huko, familia yake ilinialika niungane nao kwa ajili ya jioni ya nyumbani. Nilipendezwa na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, zaidi kutokana na jinsi familia ya rafiki yangu ilivyokuwa na furaha jioni ile.

McKaylie, Colorado, Marekani

mvulana; wavulana wakizungumza

Shiriki kwa Sababu ya Upendo

Binamu yangu alinihimiza nikutane na wamisionari, nadhani, kwa sababu alitaka nifurahie baraka alizokuwa akizifurahia wakati huo. Nilihisi kwamba binamu yangu na rafiki yangu, Enoch, walinipenda na walitaka kitu chema kwa ajili yangu. Ilinifanya nihisi faraja sana kuja kanisani.

Eric, Ghana