“Kuwa Jibu kwa Sala ya Mtu,” Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana, Julai 2023.
Njoo, Unifuate
Kuwa Jibu kwa Sala ya Mtu
Kufuata misukumo kunaweza kutusaidia tulete tofauti.
Yawezekana unahisi huna kikubwa cha kutoa. Lakini unayo imani katika Yesu Kristo, na imani yako Kwake inatosha kukuongoza kwenye mambo makubwa zaidi.
Muda mfupi baada ya kifo na Ufufuko wa Yesu Kristo, Petro na Yohana walikwenda hekaluni, ambapo mtu aliyekuwa hawezi kutembea aliketi nje na kuomba msaada.
Petro alimwambia mtu yule, “Mimi sina fedha wala dhahabu; lakini nilichonacho ndicho nikupacho: Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti simama uende” (ona Matendo ya Mitume 3:6; msisitizo umeongezwa).
Petro alimwinua mtu yule asimame kwa miguu yake. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, mtu yule aliweza kusimama. Alitembea na hata kuruka ruka kwa shangwe. Imani ya Petro katika Kristo ilimpa ujasiri wa kumponya yule mtu kwa nguvu ya ukuhani.
Acha tuwe waaminifu. Pengine hutakwenda kumponya kila mtu maradhi yake ya kimwili wakati wote. Lakini imani yako inaweza kusaidia katika njia zingine. Kama vile Petro, unaweza kutoa ulichonacho.
Kuleta Tofauti
Je, umewahi kusali ili usihisi upweke? Au kwamba mtu fulani awe rafiki yako?
Je, kuna mtu aliwahi kujitokeza, alipiga simu, au kutuma ujumbe kwako katika wakati ule? Yawezekana walikuwa wakifuata msukumo na kujaribu kuwa bora, kama vile wewe. Yote waliyofanya ni kwa uaminifu kutumia muda wao mdogo, sehemu ya ujasiri wao, na ukarimu wao kidogo—kwa maneno mengine, kile walichokuwa nacho. Wewe pia unaweza kuruhusu imani yako ikusukume kufanyia kazi misukumo.
Mzee Ronald A. Rasband wa akidi ya Mitume Kumi na Wawili amefundisha: “Tunao wajibu mtakatifu wa kujifunza kutambua ushawishi wa [Roho Mtakatifu] katika maisha yetu na kuitikia ushawishi huo.”1
Siyo daima utatambua lini au ikiwa umeleta tofauti katika siku ya mtu, hivyo inaweza kuwa vigumu kuona kusudi la kufuata misukumo.
Hata hivyo, kujaribu kuhudumu—kufanya kile unachoweza kufanya—kutakufanya uhisi furaha na ukamilifu hata kama huwezi daima kuona matokeo yake. Unaposikiliza misukumo, Roho Mtakatifu atakusaidia ujifunze jinsi ya kuwahudumia wengine, hata pamoja na ratiba yenye shughuli nyingi. Kama vile Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alivyofundisha: “Maombi hujibiwa … mara nyingi … Mungu akiwatumia watu wengine. Basi, ninaomba kwamba yeye atutumie sisi. Ninaomba kwamba tuwe jibu la maombi ya watu.”2
Shangwe kwa Kila Mtu
Kupitia kufanya mema, unaweza kuwa jibu la sala za wengine na kupata shangwe njiani—na milele yote. Kama Mzee Rasband alivyofundisha: “Shangwe inakuja kama amani katikati ya ugumu au uchungu. Inatoa faraja na ujasiri, inafunua kweli za injili, na inapanua upendo wetu kwa ajili ya Bwana na watoto wote wa Mungu.3 Kwa maneno mengine, wewe pia unakuwa zaidi kama Kristo.
Toa tu kile unachoweza, ukianzia na muda kidogo na utiifu.
Wakati mwingine, ndiyo, wewe ndiye unayehitaji msaada kidogo wa ziada. Hapa pia, Baba wa Mbinguni mwenye upendo anatuma misukumo kwa watu wengine. Wanaweza kupata shangwe wakati wakiwa jibu la sala zako, kama vile wewe unavyoweza kuwa jibu kwa sala zao. Hiyo inamaanisha kuna mabilioni ya majibu yamkini, na mtu mwingine anaweza kuwa anatembea mtaani, na si kitambo atakusalimia.