2010–2019
Utumishi wenye Mwongozo wa Kiungu
Aprili 2018


2:3

Utumishi wenye Mwongozo wa Kiungu

Tunampokea vyema sana Roho wa Mungu tunapozingatia katika kuwatumikia wengine. Hiyo ndiyo sababu kwa nini tunayo majukumu ya ukuhani ya tuhudumu kwa ajili ya Mwokozi.

Wapendwa ndugu zangu katika ukuhani, ninayo shukrani nyingi kwa nafasi hii ya kuongea nanyi katika mkutano huu mkuu wa kihistoria. Tumemkubali Rais Russell M. Nelson kama Rais wa 17 wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Kama vile mimi nilivyopata baraka ya kufanya naye kazi kila siku, nimesikia uthibitisho wa Roho Mtakatifu kwamba Rais Nelson ameitwa na Mungu kuliongoza Kanisa la kweli la Bwana.

Ni ushahidi wangu pia kwamba Bwana amemwita Mzee Gerrir W. Gong na Mzee Ulisses Soares kuhudumu kama washiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Ninawapenda na kuwaidhinisha. Wao, kwa utumishi wao, watabariki maisha ya watu ulimwenguni kote.

Mkutano huu bado ni wa kihistoria kwa sababu nyingine moja zaidi Rais Nelson ametangaza hatua ya kusonga mbele yenye mwongozo wa kiungu katika utaratibu wa mpango wa Bwana kwa ajili ya Kanisa Lake. Mpango huo unajumuisha muundo mpya kwa ajili ya akidi za ukuhani katika kata na vigingi ili kwamba tuweze kwa ufanisi zaidi kutimiza majukumu yetu ya ukuhani. Majukumu hayo yote yanahusiana na uangalizi wetu wa kikuhani kwa watoto wa Baba Yetu.

Mpango wa Bwana kwa ajili ya Watakatifu Wake wa kutoa matunzo kwa upendo umechukua sura nyingi kwa miaka mingi sasa. Katika siku za mwanzoni za Nauvoo, Nabii Joseph Smith alihitaji utaratibu mzuri kwa ajili ya kutoa matunzo kwa watakatifu waliofurika hapo wengi wao wakiwa hawana kitu wakati wakija jijini humo. Wanne kati ya mababu wa baba zangu walikuwa miongoni mwa hao—wakina Eyring, Bennion, Romney, na Smith. Nabii alitengeneza utaratibu wa kuwahudumia Watakatifu hao kwa jiografia. Huko Illinois ile migawanyiko ya maeneo ya jiji ilikuwa ikiitwa “kata.”

Watakatifu walipokuwa wakisafiri nyikani, huduma na matunzo kwa kila mmoja vilikuwa vikipatikana kwa utaratibu wa “kombania” Mmoja wa mababu wa baba zangu wa upande wa baba yangu alikuwa anarejea kutoka misheni yake ambako sasa kunaitwa Oklahoma alikutana na kombania ikiwa safarini. Alikuwa amedhoofu sana kwa maradhi kiasi kwamba yeye na mwenzake walikuwa wamelala chali katika mkokoteni mdogo.

Kiongozi wa kombania aliwatuma wasichana wadogo wawili wakamsaidie ye yote ambaye angekuwa kwenye mkokoteni ule. Mmoja wao, dada mdogo ambaye alikuwa ameongolewa huko Switzerland, akamtazama mmoja wa wale wamisionari na akaona huruma. Akaokolewa na ile kombania ya Watakatifu Akapona kiasi cha kutosha hata kuweza kutembea njia yote mpaka kufika Bonde la Salt Lake na mwokoaji wake kijana akiwa pembeni mwake. Walipendana na wakaoana. Akaja kuwa babu wa baba yangu Henry Eyring, na yeye akawa bibi wa mama yangu Maria Bommeli Eyring

Miaka kadhaa baadaye, watu walipotoa maoni yao juu ya ugumu mkubwa wa kuvuka bara kwenda upande mwingine, yeye alisema, “Ah hapana, haikuwa vigumu. Wakati tukitembea, tulikuwa tukiongea njia nzima juu ya muujiza ulioje kwamba sote tumegundua injili ya kweli ya Yesu Kristo. Ulikuwa ni wakati wa furaha ambao siwezi kusahau.

Toka hapo, Bwana ametumia njia mbali mbali ili kuwasaidia Watakatifu Wake kutunzana. Sasa Ametubariki sisi kwa akidi zilizoimarishwa na zenye umoja katika ngazi za kata na vigingi—akidi ambazo hufanya kazi kwa uratibu na makundi yote ya kata.

Kata za manisipaa, kombania na akidi zilizoimarishwa zote zinahitaji angalau mambo mawili ili kufanikiwa katika kusudi la Bwana la kuwafanya Watakatifu Wake kutunzana katika namna ambayo Yeye huwatunza. Wanafaulu wakati Watakatifu wanapouona upendo wa Kristo kwa ajili ya kila mmoja zaidi ya maslahi yao binafsi. Maandiko yanaiita “hisani” … upendo safi wa Kristo” (Moroni 7:47). Na wanafaulu pale Roho Mtakatifu anapomwongoza mtoa matunzo ili kujua kile ambacho Bwana anajua kuwa ni bora kwa mtu Yeye anayejaribu kumsaidia.

Muda baada ya muda katika wiki zilizopita, waumini wa Kanisa wametenda mbele yangu kana kwamba kwa kiasi fulani walikuwa wakitarajia kile ambacho Bwana atafanya, kama ilivyotangazwa hapa leo. Acha nikupeni mifano hii miwili. Moja, mazungumzo katika mkutano wa kawaida wa sakramenti ya mwalimu wa miaka 14 katika Ukuhani wa Haruni ambaye anaelewa kile ambacho mwenye ukuhani anaweza kutimiza katika huduma yao kwa ajili ya Bwana. Pili, mwenye Ukuhani wa Melkizedeki ambaye, kwa upendo wa Kristo, alipata mwongozo wa kiungu kuihudumia familia.

Kwanza, acha niwapeni maneno ya yule kijana akiongea kwenye mkutano wa sakramenti. Nilikuwa pale Jaribu kukumbuka wewe ulikuwaje ulipokuwa na umri wa miaka 14 na sikiliza ili umsikie akisema zaidi ya kijana wa umri wake anavyoweza kujua.

“Hakika nimefurahia kuwa mshiriki wa akidi ya walimu katika kata yangu tangu nilipofikisha miaka 14 mwaka jana. Mwalimu bado anayo majukumu yale yote ya shemasi na mengine mapya.

“Kwa vile baadhi yetu ni walimu, wengine watakuwa siku moja, na kila mmoja katika Kanisa anabarikiwa kwa ukuhani, hivyo basi ni muhimu kwetu sote kujua zaidi juu ya kazi za mwalimu.

“Kwanza kabisa, Mafundisho na Maagano 20:53 inasema, ‘Kazi ya mwalimu ni kuliangalia Kanisa daima, na kuwa nalo, na kuwaimarisha.’

“Inayofuata, Mafundisho na Maagano 20:54–55 inasema:

“Na kuona kwamba hakuna uovu katika kanisa, wala kuzozana baina yao, wala kudanganya, kusengenya, wala kusemana mabaya;

“Na kuona kwamba kanisa linakutana pamoja mara kwa mara, na pia kuona kwamba waumini wote wanatimiza wajibu wao.’”

Yule kijana aliendelea

“Bwana anatuambia kuwa ni wajibu wetu si tu kuliangalia Kanisa bali pia kuwaangalia watu ndani ya Kanisa kwa njia ile ambayo Kristo angewaangalia kwa sababu hili ni Kanisa Lake. Kama tunajaribu kushika amri, kuwa wa karimu kwa kila mmoja wetu, kuwa waaminifu, kuwa marafiki wema, na kufurahia katika kuwa pamoja, hapo tutaweza kuwa na Roho Mtakatifu pamoja nasi na kujua kile Baba yetu wa Mbinguni anachotaka tufanye. Kama hatufanyi hivi, hatutaweza kutimiza wajibu wetu.”

Aliendelea kusema:

“Mwalimu anapochagua kuonyesha mfano kwa kuwa mwalimu mzuri wa nyumbani, akiwasalimu waumini kanisani, akiandaa sakramenti, akisaidia nyumbani, na kuwa mtunza amani, anachagua kuheshimu ukuhani wake na kutimiza wito wake.

“Kuwa mwalimu mzuri haimaanishi tu kuwajibika tunapokuwa kanisani au katika shughuli za Kanisa. Mtume Paulo alifundisha, ‘Uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi, na mwenendo, katika upendo,na imani, na usafi’ (1 Timotheo 4:12).”

Kisha mvulana huyo alisema :

“Bila kujali mahali tulipo au tunafanya nini, tunaweza kuwa kielelezo cha haki wakati wote na mahali pote.

“Baba yangu na mimi tunawafundisha wakina Brown nyumbani.1 Kila wakati tuendapo huko, ninakuwa na muda mzuri wa kuongea nao na kuwajua vizuri. Jambo moja ambalo nalipenda sana juu yao ni kwamba wakati wowote tuendapo kwao, wote wanakuwa tayari kusikiliza na daima wana hadithi nzuri za kushiriki nasi.

“Tunapowajua watu vizuri katika kata yetu kwa sababu ya ualimu wa nyumbani, hufanya iwe rahisi kwa mwalimu kufanya kazi inayofuata, na hiyo ni kuwasalimia waumini kanisani. Kuwasaidia watu kujisikia wanakaribishwa na wanajumuishwa kanisani inawasaidia washiriki wote wa kata wajisikie kupendwa na kujiandaa kupokea sakramenti.

“Baada ya kuwasalimia waumini ambao wamefika kanisani, walimu husaidia kila Jumapili kwa kuandaa sakramenti. Hakika ninafurahia kupitisha na kuandaa sakramenti katika kata hii kwa sababu kila mmoja anakuwa mtulivu sana. Daima ninamsikia Roho wakati ninapotayarisha na kupitisha sakramenti. Hakika hii ni baraka kwangu mimi kwa kuweza kufanya hilo kila Jumapili.

“Huduma nyingine kama kupitisha sakramenti ni kitu ambacho watu wanaona na kutushukuru kwa kufanya hilo, lakini baadhi ya huduma kama kutayarisha sakramenti kwa kawaida hufanyika bila mtu yeyote kutambua. Hiyo si muhimu kama watu wanatuona sisi tukihudumu; kile cha muhimu ni kwamba Bwana anajua kwamba tumemtumikia Yeye.

“Kama walimu, tunapaswa daima kuliimarisha Kanisa hili, marafiki zetu, na familia zetu kwa kutimiza wajibu wetu wa ukuhani. Si rahisi daima, lakini Bwana hatoi amri kwetu isipokuwa awatayarishie njia [sisi ili] kutimiza kitu ambacho amewaamuru1 Nefi 3:7

Mvulana yule alipomaliza, niliendelea kustaajabia ukomavu na hekima yake. Alifanya muhtasari kwa kusema, “ninajua tutakuwa bora zaidi endapo tutachagua kumfuata [Yesu Kristo].”

Hadithi nyingine juu ya huduma ya ukuhani ilihadithiwa mwezi mmoja uliopita katika mkutano wa sakramenti wa kata. Tena, nilikuwa hapo. Huyu kuhani mzoefu hakujua wakati huo akiwa anaongea kwamba alikuwa akielezea kile kile ambacho Bwana anakitaka kitokee kwa akidi za ukuhani zilizoimarishwa. Hiki ndicho kiini cha hadithi yake:

Yeye na mwenza wake katika ualimu wa nyumbani walipangiwa kuzitumikia familia saba. Karibia wote hawakutaka kutembelewa. Walimu wa nyumbani walipokwenda katika makazi yao, walikataa kufungua milango. Walipowapigia simu, hawakujibiwa. Walipoacha ujumbe, hawakurudisha majibu. Mwenza huyu mwandamizi hatimaye aliishia kwenye huduma ya uandishi-wa barua Alianza hata kutumia bahasha za rangi kali ya manjano akitumaini kupata majibu.

Mmoja katika zile familia saba alikuwa dada mmoja ambaye hajaolewa alikuwa amehamia kutoka Ulaya. Alikuwa na watoto wawili wadogo.

Baada ya majaribio mengi ya kuwasiliana naye, alipokea ujumbe wa simu. Kwa ghafla akamjulisha ya kuwa ana shughuli nyingi sana hawezi kukutana na walimu wa nyumbani Alikuwa anafanya kazi mbili na alikuwa jeshini vile vile. Kazi yake ya msingi ilikuwa ni ile ya afisa wa polisi, na lengo lake la kitaaluma ni kuwa mpelelezi na ndipo arudi katika nchi yake ya asili na kuendelea na kazi yake hiyo huko.

Walimu wa nyumbani katu hawakuweza kukutana naye nyumbani mwake. Kipindi baada ya kipindi mwalimu alikuwa akimtumia ujumbe wa simu. Kila mwezi alimpelekea barua iliyoandikwa kwa mkono, ikiongezewa kwa kadi za sikukuu kwa kila mtoto.

Hakupokea majibu. Lakini yeye alijua walimu wake wa nyumbani walikuwa wakina nani, namna ya kuwapata, na kwamba wataendelea kuwepo katika huduma hii ya ukuhani.

Kisha siku moja alipokea ujumbe wa dharura kutoka dada huyu. Alihitaji msaada wa haraka sana. Hakumjua askofu wake alikuwa nani lakini aliwajua walimu wake wa nyumbani.

Ndani ya siku chache, alihitajika kuondoka jimboni kwa ajili ya mazoezi ya mafunzo ya kijeshi kwa mwezi mmoja. Hangeweza kwenda na watoto wake. Mama yake, ambaye angewatunza watoto wake, amesafiri tu hivi karibuni kwenda Ulaya kumwuguza mume wake, ambaye amepata dharura ya kiafya.

Dada huyu asiye hudhuria kikamilifu alikuwa na fedha ya kutosha tu kununua tiketi ya Ulaya kwa mtoto wake mdogo lakini siyo mwanawe wa kiume wa miaka 12, Eric.2 Alimwomba mwalimu wake wa nyumbani kama angeweza kumtafutia familia ya WSM ili wakae na Eric nyumbani mwao kwa hizo siku 30 zijazo!

Mwalimu wa nyumbani alimrudishia ujumbe wa simu kwamba angejitahidi kwa uwezo wake wote. Kisha mwalimu akawasiliana na viongozi wake wa ukuhani. Askofu, ambaye alikuwa ndiye kuhani mkuu msimamizi, akampa idhini ya kuwaendea washiriki wa baraza la kata, ikiwa ni pamoja na rais wa Muungano wa Usaidizi wa Wakina Mama.

Rais wa Muungano wa Usaidizi wa Wakina Mama haraka akapata familia nne za WSM, wenye watoto wa umri wa Eric, ambao wangemkaribisha nyumbani mwao kwa wiki moja moja. Kwa zaidi ya mwezi mmoja, familia hizi walimlisha Eric, walimtafutia nafasi katika nyumba zao ambazo tayari zilikuwa zimejaa au ni nyumba ndogo, walikwenda naye katika shughuli za majira ya kiangazi ambazo tayari zilikuwa zimepangwa, walimleta kanisani, walimjumuisha katika jioni ya familia nyumbani, na kuendelea.

Familia kadhaa zilikuwa na wavulana wa umri wa Eric, na walimjumuisha katika mikutano na shughuli za akidi za mashemasi. Katika kipindi hiki cha siku 30, Eric alikuwa kanisani kila Jumapili kwa mara ya kwanza katika maisha yake.

Baada ya mama yake kuja nyumbani baada ya mafunzo yake, Eric aliendelea kuhudhuria Kanisani, kwa kawaida alikuwa pamoja na moja ya familia hizi za WSM waliojitolea au wengine ambao walifanya urafiki naye, ikiwa ni pamoja na walimu wa kumtembelea mama yake. Wakati ulipofika, alitawazwa kuwa shemasi na akaanza kupitisha sakramenti mara kwa mara.

Sasa na tuangalie siku za usoni za Eric. Hatutashangaa kama atakuwa kiongozi katika Kanisa katika nchi ya mama yake familia yake itakaporudi huko—yote haya ni kwa sababu ya Watakatifu waliofanya kazi kwa pamoja chini ya maelekezo ya askofu, kuhudumu kutokana na hisani katika mioyo yao na kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Tunajua kwamba hisani ni muhimu kwetu sisi ili kuokolewa katika ufalme wa Mungu. Moroni aliandika “Isipokuwa una upendo huwezi kuokolewa katika ufalme wa Mungu” (Moroni 10:21; ona pia Etheri 12:34).

Tunajua pia kwamba hisani ni zawadi tunayotunukiwa baada ya kutenda yote tunayoweza. Ni lazima “tuombe kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba [tujazwe] na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwanawe, Yesu Kristo” (Moroni 7:48).

Kwangu inaonekana kana kwamba tunampokea vyema sana Roho wa Mungu tunapokuwa tumezingatia katika kuwatumikia wengine. Hiyo ndiyo sababu kwa nini tunayo majukumu ya ukuhani ya tuhudumu kwa ajili ya Mwokozi. Tunapokuwa tumejishughulisha katika huduma kwa wengine, hatujifikirii wenyewe, na Roho Mtakatifu kwa utayari zaidi anaweza kuja kwetu na kutusaidia katika kutafuta kwetu maisha yote ili zawadi ya hisani itunukiwe juu yetu

Ninawapa ushahidi wangu kwamba Bwana amekwisha anza kupiga hatua kubwa mbele katika mpango Wake kwa ajili yetu ili tuweze kuwa wenye mwongozo wa kiungu na wenye hisani zaidi katika huduma ya utumishi wetu wa ukuhani. Ninashukuru kwa upendo Wake, ambao anatupa kwa ukarimu sana. Nashuhudia hivi, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Jina limebadilishwa

  2. Jina limebadilishwa