Makala
Ameniachia Amani
Mwanzilishi mwaminifu wa Kanisa huko Rwanda anashinda janga.
Kati ya 1990 na 1994 Rwanda ilikuwa imeraruliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilisababisha mamia ya maelfu ya mauaji kati ya Aprili na Julai 1994. Matukio haya ya huzuni yaliathiri maisha ya takriban kila mtu katika nchi. katika kipindi hiki, Agnes Twagiramariya aliyekuwa na miaka 11 alimshuhudia jirani akiwaua wazazi wake, ndugu zake wanne na wengi wa ndugu zake wengine. Kwa miaka 12 iliyofuatia, Agnes alipambana na maumivu ya vifo vya wanafamilia wake. “Kupoteza familia yangu, hasa wazazi wangu,” Agnes alisema, “ni kitu kibaya sana katika maisha yangu na kilisababisha tabia kama kuwa mpweke, kuchukia watu, kutokuwa na furaha kwa muda fulani pamoja na kuvunjika moyo.”
Mnamo 2006, alipokuwa akisoma Chuo Kikuu cha Kigali, Agnes alihamia kwenye nyumba pamoja na binamu yake Yvonne, ambaye alikuwa muumini wa Kanisa. Wakiwa wanaishi pamoja, Yvonne alianza kushiriki video za Kanisa kuhusu Yesu Kristo na Urejesho wa injili Yake kupitia Joseph Smith. Hatimaye, Yvonne alimwalika Agnes kusoma Kitabu cha Mormoni na kuhudhuria Kanisani pamoja naye. “Kitu cha kwanza kilichonivutia kilikuwa mafundisho,” Agnes alisema baadaye. “Kitu kingine ni tabia ya baadhi ya waumini wa Kanisa; walionesha tabia kama za watoto wa Bwana.”
Agnes alibatizwa mnamo Juni 13, 2010. Punde aliitwa kufundisha watoto wa Tawi la Kigali katika darasa la Msingi lililokuwa likikua kwa kasi. Shangwe yake kwenye injili ilipokuwa inaongezeka, Agnes aliendelea kujiuliza ikiwa angeiona familia yake tena, ikiwa bado walikuwa na maumivu, na maisha baada ya kifo yalikuwaje kwao. Mnamo 2012 Agnes alisafiri kwenda Johannesburg, Afrika Kusini, ili kuhudhuria hekaluni kwa mara ya kwanza—na kuunganishwa milele yote kwa wazazi wake na ndugu waliokufa.
Wakati upotevu daima utakuwa sehemu ya maisha yake, Agnes alipata uponyaji kupitia injili ya urejesho. “Nimeanza kutabasamu na kuzungumza tena,” Agnes alisema. “Nilifanya mabadiliko katika maisha yangu, na ninaweza kuwa na furaha kwa muda mrefu. Nina amani kuwa na moyo wa kusamehe.”
“Ninaweza kuwasamehe wale wauaji wa familia yangu,” alisema. “Kwangu mimi, msamaha ni tunu niliyopokea baada ya kuielewa injili.” Kristo, aliyeteseka katika nyumba ya rafiki zake (ona Zekaria 13:6), alijua jinsi ya kumfikia katika mapambano yake. “Kanisa la kweli la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lilikuwa daraja langu la kuachana na maisha ya mkanganyiko kwenda maisha ya ukweli, kutoka kwenye huzuni kwenda kwenye furaha halisi, kutoka kwenye majonzi kwenda kwenye shagwe, kutoka kwenye hasira mpaka kwenye msamaha,” alisema. “Ninashuhudia kwamba Mwokozi wetu Yesu Kristo anatupenda, na anataka tuwe na furaha na tuwe na shangwe halisi.”